Yoashi Anaacha Imani na Kufa

840 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 12:17–18

17 Wakati huu Hazaeli mfalme wa Aramu akapanda kuishambulia Gathi, akaiteka. Kisha akageuka ili kuishambulia Yerusalemu. 18 Lakini Yoashi mfalme wa Yuda akavichukua vyombo vyote vitakatifu vilivyowekwa wakfu na baba zake, yaani Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, wafalme wa Yuda, zawadi ambazo yeye mwenyewe alikuwa ameziweka wakfu pamoja na dhahabu yote iliyokutwa katika hazina za Hekalu la Bwana na katika jumba la kifalme, akazipeleka kwa Hazaeli mfalme wa Aramu, ambaye hatimaye aliondoka Yerusalemu.

2 Nyakati 24:15–26

15 Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku wakati alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka 130. 16 Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.

17 Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walikuja kumpa mfalme heshima, naye akawasikiliza. 18 Wakaacha Hekalu la Bwana, Mungu wa baba zao, wakaabudu nguzo za maashera na sanamu. Kwa sababu ya hatia yao, hasira ya Mungu ikawajia Yuda na Yerusalemu. 19 Ingawa Bwana aliwatuma manabii wawarudishe watu kwake na ingawa waliwaonya, hawakuwasikiliza.

20 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Bwana? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.’ ”

21 Lakini wakafanya shauri baya juu yake na kwa amri ya mfalme wakampiga kwa mawe mpaka akafa katika ukumbi wa Hekalu la Bwana. 22 Mfalme Yoashi hakukumbuka wema aliotendewa na Yehoyada baba yake Zekaria ila alimuua mwanawe, ambaye alisema wakati akiwa amelala akingojea kufa, “Bwana na alione hili na alipize kisasi.”

23 Mwishoni mwa ule mwaka, jeshi la Waaramu likaja dhidi ya Yoashi, likavamia Yuda na Yerusalemu na kuwaua viongozi wote wa watu. Wakapeleka nyara zao zote kwa mfalme wao huko Dameski. 24 Ingawa jeshi la Waaramu lilikuwa limekuja na watu wachache tu, Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa kuliko lao. Kwa sababu Yuda walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, hukumu ilitekelezwa juu ya Yoashi. 25 Waaramu walipoondoka, walimwacha Yoashi akiwa mgonjwa sana. Maafisa wake wakafanya hila dhidi yake kwa sababu alikuwa amemuua mwana wa Kuhani Yehoyada, nao wakamuulia kitandani mwake. Hivyo akafa na wakamzika katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.

26 Wale waliofanya hila mbaya dhidi yake walikuwa Zabadi, mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, Yehozabadi, mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabu.

2 Wafalme 12:20–21

20 Maafisa wake wakafanya shauri baya dhidi yake, nao wakamuulia Yoashi huko Beth-Milo, kwenye barabara iteremkayo kuelekea Sila. 21 Maafisa waliomuua walikuwa Yozabadi mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri. Akafa na akazikwa pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi. Naye Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

2 Nyakati 24:27

27 Kwa habari za wanawe, unabii mwingi kumhusu na kumbukumbu za kutengenezwa upya kwa Hekalu la Mungu, zimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme. Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

2 Wafalme 12:19

19 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yoashi na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

2 Nyakati 24:1–2

1 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba. 2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ya Yehoyada kuhani.

2 Wafalme 11:17–20

17 Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Bwana na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Bwana. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu. 18 Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu.

Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la Bwana. 19 Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la Bwana na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha enzi, 20 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani kwa mfalme.