Ufalme wa Israeli
Kifo cha Yehu
838 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
30 Bwana akamwambia Yehu, “Kwa kuwa umefanya vyema kwa kutimiza yaliyo sawa machoni pangu, na umetenda kwa nyumba ya Ahabu yale yote niliyokuwa nimekusudia kutenda, wazao wako wataketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli hadi kizazi cha nne.” 31 Lakini Yehu hakuwa mwangalifu kushika sheria za Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.
32 Katika siku hizo, Bwana akaanza kupunguza ukubwa wa Israeli. Hazaeli akawashinda Waisraeli sehemu zote za nchi yao 33 mashariki ya Yordani, katika nchi yote ya Gileadi (eneo la Gadi, Reubeni na Manase), kutoka Aroeri karibu na Bonde la Arnoni kupitia Gileadi hadi Bashani.
34 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yehu, yote aliyofanya na mafanikio yake yote, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
35 Yehu akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa huko Samaria. Naye Yehoahazi mwanawe akawa mfalme baada yake. 36 Muda Yehu aliotawala juu ya Israeli huko Samaria ilikuwa miaka ishirini na minane.
Utawala wa Yehoahazi wa Israeli 849 KK
1 Katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka kumi na saba. 2 Akafanya maovu machoni pa Bwana kwa kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, na wala hakuziacha. 3 Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli na kwa muda mrefu akawaweka chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa Aramu, na Ben-Hadadi mwanawe.
4 Ndipo Yehoahazi akamsihi Bwana rehema, naye Bwana akamsikiliza, kwa maana aliona jinsi mfalme wa Aramu alivyokuwa akiwatesa Israeli vikali. 5 Bwana akamtoa mwokozi kwa ajili ya Israeli, nao wakaokoka kutoka kwenye mamlaka ya Aramu. Hivyo Waisraeli wakaishi katika nyumba zao wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali. 6 Lakini hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, bali wakaendelea kuzitenda. Nguzo ya Ashera pia iliendelea kusimama katika Samaria.
7 Hapakubaki kitu chochote katika jeshi la Yehoahazi isipokuwa wapanda farasi hamsini, magari kumi ya vita na askari wa miguu elfu kumi, kwa kuwa mfalme wa Aramu alikuwa amewaangamiza hao wengine na kuwafanya kama mavumbi wakati wa kupura nafaka.
8 Matukio mengine ya utawala wa Yehoahazi yote aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 9 Yehoahazi akalala pamoja na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoashi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Yehoashi Anatawala, na Elisha Anakufa
10 Katika mwaka wa thelathini na saba wa utawala wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala Israeli huko Samaria, naye akatawala miaka kumi na sita.
14 Wakati huu, Elisha alikuwa anaumwa na ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!”
15 Elisha akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo. 16 Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuichukua, Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
17 Elisha akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Elisha akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Elisha akasema, “Mshale wa ushindi wa Bwana, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.” 18 Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Elisha akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha.
19 Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.”
20 Elisha akafa, nao wakamzika.
Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli. 21 Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Wakati ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake.