Sehemu ya 9: Utawala wa Amazia
Ufalme wa Yuda
Amazia Anawaadhibu Wauaji wa Baba Yake
838 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu. 3 Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.
4 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
5 Baada ya ufalme kuimarika mikononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. 6 Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose ambako Bwana aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
Vita vya Amazia dhidi ya Edomu 827 KK
5 Amazia akawaita watu wa Yuda pamoja, akawaweka chini ya majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia kufuatana na jamaa zao katika Yuda yote na Benyamini. Kisha akawahesabu wale wenye umri wa miaka ishirini au zaidi na akakuta kwamba walikuwa wanaume 300,000 watu walio tayari kwa utumishi wa jeshi, walio na uwezo wa kutumia mkuki na ngao. 6 Akawaajiri pia watu 100,000 wapiganaji kutoka Israeli kwa talanta 100 za fedha.
7 Lakini mtu wa Mungu akamjia na kumwambia, “Ee mfalme, haya majeshi kutoka Israeli kamwe usiyaruhusu yaende pamoja na wewe kwa kuwa Bwana hayuko pamoja na Israeli, wala hayupo pamoja na yeyote wa watu wa Efraimu. 8 Hata kama ukienda na kupigana kwa ujasiri katika vita, Mungu atakufanya ukimbie mbele ya adui, kwa kuwa Mungu anao uwezo wa kusaidia au wa kuangusha.”
9 Amazia akamuuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta 100 za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?”
Yule mtu wa Mungu akajibu, “Bwana aweza kukupa zaidi sana ya hizo.”
10 Hivyo Amazia akayaondoa yale majeshi yaliyokuwa yamekuja kutoka Efraimu na kuyarudisha nyumbani. Waliwakasirikia sana Yuda, nao wakarudi nyumbani wakiwa na hasira kali.
11 Ndipo Amazia akajitia nguvu na kuliongoza jeshi lake kwenye Bonde la Chumvi, ambako aliua watu 10,000 wa Seiri.
7 Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.
12 Jeshi la Yuda pia likawateka watu 10,000 wakiwa hai, likawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini kwa nguvu hata wote wakavunjika vipande vipande.
13 Wakati huo yale majeshi Amazia aliyoyarudisha na ambayo hakuyaruhusu kushiriki katika vita, yalivamia miji ya Yuda kuanzia Samaria hata Beth-Horoni. Yakawaua watu 3,000 na kuchukua kiasi kikubwa sana cha mateka.
14 Amazia aliporudi kutoka kuwachinja Waedomu, alileta pia kutoka huko miungu ya watu wa Seiri. Akaisimamisha kama miungu yake mwenyewe, akaisujudia na kuitolea kafara za kuteketezwa. 15 Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Amazia, naye akamtuma nabii kwake, ambaye alisema: “Kwa nini unauliza kwa miungu ya hawa watu, ambayo haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mkononi mwako?”
16 Wakati nabii alipokuwa angali anazungumza, mfalme akamwambia, “Je, wewe tumekuchagua kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza, ya nini uuawe?”
Hivyo nabii akanyamaza lakini akasema, “Najua kuwa Mungu ameazimia kukuangamiza kwa sababu umefanya jambo hili na hukusikiliza shauri langu.”
Vita vya Amazia dhidi ya Israeli 826 KK
8 Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tuonane uso kwa uso.”
9 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. 10 Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
11 Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. 12 Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake. 13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400. 14 Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria.