Sehemu ya 7: Utawala wa Athalia

Ufalme wa Yuda

884 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 22:10–12

10 Wakati Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuiangamiza jamaa yote ya mfalme ya nyumba ya Yuda. 11 Lakini Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala. Kwa kuwa Yehosheba, aliyekuwa binti wa Mfalme Yehoramu, na pia alikuwa mke wa kuhani Yehoyada, alikuwa dada yake Ahazia, akamficha huyo mtoto ili Athalia asimuue. 12 Alibaki amefichwa pamoja nao katika Hekalu la Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.

2 Nyakati 24:7–11

7 Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Bwana kwa mabaali.

8 Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Bwana. 9 Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu kwamba inapasa wamletee Bwana kodi ile ambayo Mose, mtumishi wa Bwana alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani. 10 Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha mpaka likajaa. 11 Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana.

2 Nyakati 23:1–15

1 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akaonyesha nguvu zake. Alifanya agano na wakuu wa vikosi vya mamia: yaani Azaria mwana wa Yerohamu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri. 2 Wakazunguka katika Yuda yote na kukusanya Walawi na viongozi wa jamaa za Israeli kutoka miji yote. Walipofika Yerusalemu, 3 kusanyiko lote likafanya agano na mfalme katika Hekalu la Mungu.

Yehoyada akawaambia, “Mwana wa mfalme atatawala, kama Bwana alivyoahidi kuhusu wazao wa Daudi. 4 Basi hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Theluthi yenu makuhani na Walawi ambao mnaingia zamu siku ya Sabato mtalinda milangoni, 5 theluthi yenu mtalinda jumba la kifalme, na theluthi nyingine mtalinda Lango la Msingi. Walinzi wengine wote mwe ndani ya nyua za Hekalu la Bwana. 6 Hakuna mtu yeyote ataingia katika Hekalu la Bwana isipokuwa makuhani na Walawi walioko kwenye zamu. Wao wanaweza kuingia kwa sababu ni watakatifu, lakini watu wengine wote itawapasa kulinda kile walichoamriwa na Bwana. 7 Walawi watajipanga kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha zake mkononi. Mtu mwingine yeyote aingiaye Hekaluni lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”

8 Walawi na watu wote wa Yuda wakafanya kama vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, kwa sababu kuhani Yehoyada hakuruhusu kikosi chochote kiondoke. 9 Kisha akawapa wakuu wa vikosi vya mamia mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu. 10 Akawapanga walinzi wote kumzunguka mfalme, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.

11 Yehoyada na wanawe wakamtoa Yoashi mwana wa mfalme nje na kumvika taji. Wakampa nakala ya agano na kumtangaza kuwa mfalme. Wakamtia mafuta na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”

12 Athalia aliposikia kelele za watu wakikimbia na kumsifu mfalme, akawaendea watu katika Hekalu la Bwana. 13 Athalia akaangalia, tazama alikuwepo mfalme akiwa amesimama karibu na nguzo yake kwenye ingilio. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta na waimbaji wakiwa na vyombo vya uimbaji, walikuwa wakiongoza nyimbo za sifa. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kupiga kelele, akisema, “Uhaini! Uhaini!”

14 Kuhani Yehoyada akawatuma majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, na kuwaambia: “Mleteni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Msimuulie ndani ya Hekalu la Bwana.” 15 Kwa hiyo wakamkamata alipofika kwenye ingilio la Lango la Farasi katika viwanja vya jumba la mfalme wakamuulia hapo.

2 Wafalme 11:1–16

1 Wakati Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuiangamiza jamaa yote ya mfalme. 2 Lakini Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa. 3 Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la Bwana kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.

4 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari, na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la Bwana. Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la Bwana. Ndipo akawaonyesha mwana wa mfalme. 5 Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi yenu inayolinda jumba la kifalme, 6 theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu, 7 nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme. 8 Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”

9 Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya kama vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada. 10 Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana. 11 Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.

12 Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakamtia mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”

13 Athalia aliposikia kelele iliyofanywa na walinzi pamoja na watu, akawaendea watu pale penye Hekalu la Bwana. 14 Akaangalia, na tazama alikuwako mfalme, akiwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa pembeni mwa mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wakifurahi na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”

15 Kuhani Yehoyada akawaagiza majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mleteni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la Bwana.” 16 Basi wakamkamata Athalia, na alipofika mahali ambapo farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuulia hapo.

Ufalme wa Israeli

2 Wafalme 10:29

29 Hata hivyo, Yehu hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, yaani kuabudu ndama za dhahabu huko Betheli ya Dani.