Wajibu wa Wake na Waume Wakristo

Petro anaendelea kuwasisitizia wajibu wa juu zaidi katika mahusiano ya familia. Anawaambia wake Wakristo wawatii waume zao, hata kama waume zao walikuwa wapagani, ili kwa mwenendo wao mtakatifu wawavute kuipenda na kuitenda injili. Ili kupata upendo wa waume zao, hawapaswi kuishia kupamba mwonekano wao wa nje, bali waelekeze mapambo yao kwenye nafsi ya ndani, iliyofichika, wakifuata mfano wa Sara, aliyekiri kuwa chini ya Abrahamu kwa kumwita bwana. Wao ni binti zake maadamu wanatenda kulingana na tabia yao ya Kikristo. Waume Wakristo wanaamriwa kuwatendea wake zao kama inavyowapasa wale waliofundishwa wajibu wa dini ya Kikristo.

65 au 66 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Petro 3:1–7

1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu. 5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, 6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.

7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.

Lipizeni Uovu kwa Baraka

Kwa kumalizia, Petro anawahimiza wote, walio katika ndoa na wasio katika ndoa, kuwa na umoja wa Kikristo, huruma na upendo, wakilipiza mabaya na matusi kwa baraka. Wanapaswa daima kutenda kulingana na dhamiri zao, ili wale wanaowashtaki kwa uongo kwamba wanatenda maovu waaibishwe na mwenendo wao mwema katika Kristo. Ikiwa ni mapenzi ya Mungu wapate mateso, ni afadhali kuteseka kwa kutenda mema kuliko kwa kutenda maovu.

1 Petro 3:8–17

8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. 10 Kwa maana,

“Yeyote apendaye uzima

na kuona siku njema,

basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,

na midomo yake isiseme hila.

11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;

lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.

12 Kwa maana macho ya Bwana

huwaelekea wenye haki,

na masikio yake yako makini

kusikiliza maombi yao.

Bali uso wa Bwana uko kinyume

na watendao maovu.”

13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? 14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” 15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, 16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.

Mateso ya Kristo, Safina ya Noa na Ubatizo

Akikengeuka kidogo kutoka kwenye mada, Petro anawatia moyo kwa kutafakari mateso ya Kristo, ili wasione mateso yao kuwa ishara ya kutopendezwa kwa Mungu nao. Ingawa alikuwa mwenye haki mkamilifu, Kristo aliteseka kwa ajili ya dhambi za wengine, ili amlete mwanadamu kwa Mungu. Aliuawa katika hali yake ya kibinadamu, lakini akafufuliwa na Roho wa Mungu. Kwa Roho huyo, aliyempa Noa nguvu za kiroho, aliwahubiria roho ambazo sasa zilikuwa zimefungiwa, au kuwekwa kana kwamba gerezani chini ya haki ya Mungu, ili zipokee adhabu iliyostahili dhambi zao. Kwa subira yake, Mungu alingoja miaka 120 ili kuona kama wangetubu na kuokolewa, wakati safina ilipokuwa ikijengwa (Mwanzo 6:3). Kisha familia ya Noa, iliyoamini, ikaokolewa kwa maji. Hii ilikuwa mfano wa wokovu wa familia ya Kristo, ndani ya safina ya kanisa, kwa maji ya ubatizo, ambayo kwayo wanaingizwa katika hali mpya ya maisha na kuokolewa kutoka kaburini kupitia ufufuo wa Yesu Kristo. Amekwenda mbinguni, na malaika na viumbe vya kila daraja, mbinguni na duniani, wamewekwa chini ya mamlaka yake, ili awape wokovu wote wanaomwamini.

1 Petro 3:18–22

18 Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho. 19 Baada ya kufanywa hai, alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni: 20 roho hizo ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Noa, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika. 21 Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo. 22 Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote wametiishwa chini yake.

Wafu kwa Dhambi, Wanaoishi kwa Mapenzi ya Mungu

Kwa kuwa Kristo alikufa kifo chenye maumivu katika mwili kwa ajili ya mwanadamu, Petro anawahimiza wao pia wausulubishe mwili, kwa maana wale waliouua mwili wameacha kutenda dhambi, au wamekuwa wafu kwa dhambi. Wanaishi maisha yao yaliyobaki si kwa tamaa za mwili bali kwa mapenzi ya Mungu. Kwa maana walitumia muda mwingi mno wa maisha yao yaliyopita katika machukizo ya aibu na maovu ambayo wapagani walijitosa ndani yake. Sasa wapagani wanashangaa na kuwasingizia kwa sababu hawajiungi nao katika ufisadi uleule uliopindukia, wakisahau kwamba itawabidi kutoa hesabu kwa yule atakayewahukumu wenye haki na waovu pia. Kwa sababu hii injili ilihubiriwa kwa wapagani, waliokuwa wafu katika makosa na dhambi, ili wale walioamini wahukumiwe, au watiwe hatiani, na watu wanaotawaliwa na mwili, huku wao wakiishi kwa mapenzi ya Mungu katika roho.

1 Petro 4:1–6

1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu. 3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. 4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi. 5 Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. 6 Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.

Nguvu za Watesi Wao Zitaisha Hivi Karibuni

Petro anawafariji kwa kuwahakikishia kwamba nguvu za watesi wao wakatili zitaangamizwa hivi karibuni, katika maangamizi yanayokuja ya watu wa Wayahudi na taifa lao. Anawahimiza wajihadhari na kila aina ya uchafu na kusali ili waokolewe kutoka katika maangamizi hayo, wakiwa na upendo mwingi, unaovumilia au kufuta makosa ya kila mmoja wao. Katika wakati huu wa mateso wanapaswa kukaribishana bila kujali usumbufu unaotokana na hilo. Kila mmoja anapaswa kutumikia kulingana na vipawa alivyopokea kutoka kwa Bwana kwa njia ya uangalizi wake na neema yake. Yeyote anayenena kuhusu neno la Mungu anapaswa kunena “kama mtu anayewasilisha maneno ya Mungu.” Yeyote anayehudumia mahitaji ya maskini anapaswa kufanya hivyo kwa kutumia mali ambazo Mungu amempa, akimpa Mungu utukufu kupitia Yesu Kristo.

1 Petro 4:7–11

7 Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na akili tulivu na kiasi, mkikesha katika kuomba. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

Furahini Kushiriki Mateso ya Kristo

Petro anawaonya Wakristo wasishangae kwa sababu ya majanga na mateso yanayowapata, yaliyokusudiwa kuijaribu imani yao, bali wafurahi, kwa kuwa kupitia hayo wanashiriki mateso ya Kristo, ili watukuzwe pamoja naye. Wale wanaotukanwa kwa kuwa Wakristo wamebarikiwa, kwa maana Roho wa Mungu aliyekaa juu ya Yesu anakaa juu yao pia: watesi wao wanamkufuru Kristo, lakini kwa mateso yao yeye anaheshimiwa. Kwa sababu hii anawaonya wasiteseke kwa ajili ya kosa lolote lao wenyewe (akitaja makosa ambayo Wayahudi wasioamini walikuwa wamezoea kuyatenda), jambo lisiloleta utukufu wala thawabu. Lakini yeyote anayeteseka kwa kuwa Mkristo asione aibu, hata adhabu hiyo iwe ya aibu kiasi gani, bali amtukuze Bwana, ambaye pia aliteseka kwa sababu ya kuwa mtakatifu. Sasa wakati umefika wa kuadhibiwa kwa Wayahudi kama taifa, adhabu ambayo itaanzia katika nyumba ya Mungu (Yohana 16:2; Mathayo 23:35; Ezekieli 9:6). Ikiwa inaanza kwanza na Wayahudi wanaoamini, ni maangamizi gani ya kutisha yatakayowapata wale wasioitii Injili? Na ikiwa Wakristo wanaepuka hukumu ya Mungu juu ya Yerusalemu kwa shida kubwa tu, wasiomcha Mungu na wenye dhambi wanawezaje kutumaini kuokolewa? Petro anawaambia wapagani pamoja na Wayahudi wanaoteseka kwa ajili ya haki wayakabidhi maisha yao kwa Mungu kama kwa Muumba mwaminifu, ambaye atawatunza kama viumbe na watoto wake na kuwapa uzima wa milele, ikiwa wataendelea kutenda mema.

1 Petro 4:12–19

12 Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu. 15 Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine. 16 Lakini kama ukiteseka kwa kuwa Mkristo, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo. 17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje? 18 Basi,

“Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka,

itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?”

19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.

Wazee Walichunge Kundi la Mungu

Petro, akiwa shahidi aliyejionea mateso ya Kristo (bustanini, wakati wa kukamatwa kwake na katika ukumbi wa kuhani mkuu), na ambaye aliuona na kuushiriki utukufu wa Kugeuka Sura, anawahimiza wazee walilishe kundi la Kristo kwa uaminifu. Wanapaswa kufanya kazi ya maaskofu, au waangalizi, katika nyakati hizi za mnyanyaso, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, si kwa ajili ya kujipatia riziki bali kwa shauku ya kuendeleza utukufu wa Mungu. Hawapaswi kuyatawala kwa mabavu makundi, ambayo ni urithi wa Mungu, bali wawe mifano kwao ya unyenyekevu na kila fadhila ya Kikristo. Na Mchungaji Mkuu, ambaye makundi ni yake, atakapoonekana, wale waliotimiza wajibu wao watapokea kutoka kwake taji la utukufu.

1 Petro 5:1–4

1 Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: 2 lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. 3 Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi. 4 Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika.

Kuweni Wanyenyekevu na Mpingeni Ibilisi

Petro anawaagiza wale wenye nyadhifa za chini kanisani wawatii wazee, kisha anawaita wote kwa pamoja wajitiishe wao kwa wao, wakitumikiana kila mmoja katika nafasi yake, na kujivika unyenyekevu ili uwalinde na kuwahifadhi. Kwa kuwa Mungu huwapinga wenye kiburi, wanapaswa kujinyenyekeza na kukubali kwa saburi jinsi anavyowatendea katika kila hatari na dhiki, wakimtupia Mungu mahangaiko yao yote, kwa maana anawajali (Zaburi 55:22). Jambo pekee linalopaswa kuwahangaisha ni kudhibiti tamaa zao, wakijizuia na kujichunga daima, kwa sababu katika kipindi hiki cha majaribu na majanga yao, adui yao wa kiroho anazungukazunguka, “akitafuta mtu wa kummeza,” akitumaini kuwafanya waache imani. Wanapaswa kumpinga, wakiwa imara katika imani kwa Mwana wa Mungu, wakijua kwamba wanafunzi wa Kristo wamewekewa kuteswa na wanadamu na mashetani. Petro anamwomba Mungu awatie nguvu na kuwakamilisha katika imani ya Kristo.

1 Petro 5:5–11

5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,

“Mungu huwapinga wenye kiburi,

lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.

Petro Anatuma Barua Yake Kupitia Silvano

Petro anawaambia kwamba anatuma barua hii kupitia Silvano (ambaye ndiye Sila, Matendo 15:40; 16:19), na kwamba amewaandikia kwa ufupi, kama anavyoona yeye, akiwashuhudia kwamba walichohubiriwa ni injili ya kweli ya Kristo. Anawaomba wasalimiane kama ishara ya upendo wao wa Kikristo, na anamalizia kwa baraka yake ya kitume.

1 Petro 5:12–14

12 Kwa msaada wa Silvano, ambaye ninamhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.

13 Kanisa lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu. 14 Salimianeni kwa busu la upendo.

Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo.