Petro Awaandikia Wakristo Walio Wayahudi na Watu wa Mataifa
Petro anaandika barua yake ya kwanza kwa Wayahudi ambao, wakati wa mateso, walikuwa wamekimbilia katika nchi za kipagani zilizotajwa mwanzoni mwa barua hiyo, na pia kwa waongofu kutoka kwa watu wa Mataifa. Anaandika ili kuwatia moyo wavumilie mateso kwa furaha kwa ajili ya dini yao, na kuwasisitizia umuhimu wa kuishi maisha matakatifu yasiyo na lawama, ili wazifedheheshe kashfa za adui zao.
65 au 66 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Petro Awasalimu Wakristo Walio Wayahudi na Watu wa Mataifa
Salamu na baraka za Petro kwa Wayahudi na wapagani waliochaguliwa kulingana na ujuzi wa Mungu wa mambo kabla hayajatokea, uliofunuliwa na manabii, ili waitii injili kwa utendaji wa Roho Mtakatifu. Kwa njia hii wanashiriki katika baraka zote zinazotokana na damu ya Kristo inayofanya upatanisho.
1 Petro, mtume wa Yesu Kristo:
Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia. 2 Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utiifu kwa Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake:
Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.
Petro Amhimidi Mungu kwa Kuzaliwa Kwao Upya
Petro anamhimidi Mungu kwa kuzaliwa kiroho kwa Wayahudi na wapagani katika tumaini la uzima baada ya kifo kupitia ufufuo wa Yesu Kristo, ili washiriki urithi usioweza kuharibiwa. Katika tumaini la wokovu huu wanapaswa kufurahi sana, ingawa wanahuzunishwa na mateso mbalimbali. Mateso haya yanahitajika ili kuthibitisha imani yao, ambayo kujaribiwa kwake kuna thamani kubwa kuliko kujaribiwa kwa dhahabu, kwa kuwa kunawapatia utukufu na sifa za milele wakati wa kuja kwa Yesu Kristo. Wanamfurahia sana kama Mwokozi, ingawa hawamwoni, wakijua kwamba watapokea kutoka kwake thawabu ya imani yao, yaani wokovu wa nafsi zao. Manabii walitabiri wokovu huu, wakichunguza kwa makini ili kujua ni wakati gani na watu gani ambao Roho wa Mungu alikuwa akiwataja aliposhuhudia mapema mateso ya Kristo na utukufu na baraka ambazo zingefuata. Roho Mtakatifu pia aliwafunulia manabii kwamba hawakuwa wakijihudumia wenyewe bali watu wa wakati wa baadaye, katika mambo ambayo sasa yametangazwa kwa ulimwengu na mitume, waliopewa nguvu kwa kusudi hilo na Roho Mtakatifu huyohuyo. Siri hizi ndizo ambazo malaika, pamoja na wanadamu, “wanatamani kuzichunguza” (Kutoka 25:20).
3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.
10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, 11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. 12 Walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.
Ishini Katika Hofu Takatifu, Mkiwa Mmekombolewa kwa Damu ya Kristo
Kwa kuzingatia baraka zilizopatikana kwa mateso ya Kristo, Petro anawahimiza wawe na ujasiri katika majaribu yao yote, wakitegemezwa hadi mwisho wa maisha yao na tumaini la uzima wa milele walioahidiwa siku ile Kristo atakapofunuliwa. Wanapaswa kujiepusha na tamaa walizozifuata kabla ya kuongoka kwao, na kuiga utakatifu wa Mungu, aliyewaita wawe watoto wake, kama Mose alivyoandika (Mambo ya Walawi 19:2; 1 Petro 5:10; 2:21; 3:9). Kwa kuwa kila mtu atahukumiwa kulingana na matendo yake mwenyewe, bila upendeleo, wanahimizwa kuutumia muda wa kukaa kwao duniani katika hofu yenye heshima kwa Mungu. Wanapaswa kufanya hivyo hata zaidi kwa sababu walikombolewa kutoka katika ushirikina, mapokeo au taratibu potovu za ibada walizorithi kutoka kwa baba zao, kwa damu ya Kristo, kama damu ya sadaka ya dhambi isiyo na dosari. Kristo aliteuliwa katika kusudi la Mungu kabla ya kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu, na dhabihu za Sheria zilikuwa kivuli chake, lakini alifunuliwa katika kipindi cha mwisho cha mpango wa Mungu, yaani kipindi cha Injili, kwa wapagani pia. Kwa njia ya imani katika rehema ya Mungu iliyoonyeshwa katika dhabihu hii ya Kristo, wanamwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumwinua hadi utukufu wa mbinguni, ili, imani yao ikiimarishwa na kutimizwa kwa ahadi za Mungu, tumaini lao la utukufu wa milele kupitia Kristo liwe kwa Mungu.
13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.
Mkiwa Mmezaliwa Upya, Pendaneni
Petro anawahimiza wale ambao mioyo yao imetakaswa kutokana na tamaa za mwili kwa kumwamini Kristo Yesu wapendane, si kwa matendo na maneno ya kujifanya, bali kwa moyo safi usio na tamaa za mwili, kama ndugu waliozaliwa mara ya pili. Wamezaliwa mara ya pili si kwa ukoo wa wazazi wa kibinadamu, bali kutokana na chanzo cha kimungu na cha mbinguni, yaani mafundisho ya Mungu aliye hai, yanayodumu milele.
22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. 24 Maana,
“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao ni kama maua ya kondeni;
majani hunyauka na maua huanguka,
25 lakini neno la Bwana ladumu milele.”
Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.
Mawe Yaliyo Hai katika Hekalu la Kiroho la Mungu
Petro anawahimiza waache mielekeo yote mibaya ya asili yao ya zamani na, kama watoto wachanga waliozaliwa mara ya pili kwa neema ya Mungu, watamani maziwa safi ya injili, ili asili yao mpya ilishwe na kukua hadi kukomaa, kwa kuwa tayari wameonja wema na ubora wa Bwana katika kuzaliwa kwao kwa pili, kwa kiroho (Zaburi 34:8). Wanapomjia kwa imani kama jiwe la msingi lililo hai, wanajengwa juu yake na kushiriki uhai wake, ili wawe hekalu la kiroho na jamii ya makuhani (Kutoka 19:6; Ufunuo 1:6), waliowekwa kutoa dhabihu za maombi na sifa kupitia Kristo. Kwa hiyo Isaya alitangaza (Isaya 28:16) kwamba katika Sayuni lingewekwa “jiwe la pembeni lililochaguliwa na lenye thamani,” kuwa msingi wa hekalu jipya la Mungu, likiunganisha pande mbili za jengo, Wayahudi na wapagani, katika kanisa moja (Waefeso 2:21). Wale wanaoamini ni sehemu ya jengo hili. Lakini kuhusu wasiotii imeandikwa (Zaburi 118:22) kwamba jiwe hili la msingi lililokataliwa “limekuwa jiwe la pembeni” la hekalu jipya la Mungu, na “jiwe la kujikwaa” kwa wale ambao hawakumwamini Kristo, watakaoligonga, waanguke na kuvunjika, kama Isaya alivyotabiri (Isaya 8:14–15). Petro anaeleza mapendeleo makubwa ya Wakristo kwa kutumia majina ya heshima ambayo hapo zamani yalipewa kanisa la Wayahudi, yaani wote walioingizwa katika agano na Mungu.
1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, 3 ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.
4 Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake, 5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. 6 Kwa maana imeandikwa katika Maandiko:
“Tazama, naweka katika Sayuni,
jiwe la pembeni teule lenye thamani,
na yeyote atakayemwamini
hataaibika kamwe.”
7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hili ni la thamani. Lakini kwao wasioamini,
“Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni,”
8 tena,
“Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae,
na mwamba wa kuwaangusha.”
Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno, kama walivyowekewa tangu zamani.
9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.
Kama Wageni, Jitiisheni kwa Kila Serikali ya Wanadamu
Akiwarejelea Waisraeli wa zamani (Waebrania 11:13), Petro anawahimiza, wakiwa wageni na wasafiri wasio na urithi duniani (kama walivyokuwa kwa kweli huko Asia, Ponto na nchi nyingine), waitafute nchi ya mbinguni na wajiepushe na tamaa za mwili, ambazo huitia nafsi utumwani au kuiangamiza. Wanapaswa kuishi kwa namna ambayo matendo yao mema yatakanusha masingizio ya adui zao. Wanapaswa kuitii kila aina ya serikali ya wanadamu kwa ajili ya Bwana, ili kunyamazisha ujinga wa watu wapumbavu waliodai kwamba dini yao iliwafanya wasiwe tayari kuwatii wafalme na mahakimu. Wakiwa watu waliochaguliwa na Mungu, Wayahudi walijivunia kuwa watu huru, walioongozwa na sheria zao wenyewe. Akiwa na jambo hili akilini, Petro anawahimiza waongozwe kwa ndani na sheria za dini yao, lakini wasiutumie uhuru wao kama kifuniko cha uasi, kama Wayahudi walivyofanya, bali waishi kama watumishi wa Mungu.
11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.
13 Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14 au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. 16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu. 17 Mheshimuni kila mtu ipasavyo: Wapendeni jamaa ya ndugu waumini, mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme.
Watumishi Wavumilie Mateso Kama Kristo Alivyoteseka
Petro anawasihi watumwa na watumishi wa nyumbani wawatii mabwana zao kwa unyenyekevu na heshima, hata walio wakali na wasio waadilifu, bila kufanya utii wao utegemee tabia ya wale wanaowatumikia. Wanapaswa kuvumilia mateso kwa kutenda mema, wakifuata mfano wa Kristo, aliyeteseka kwa ajili yao ili wafuate nyayo zake. Ndani yake hakukuwa na dhambi (Isaya 53:6). Aliichukua adhabu iliyostahili dhambi, ili amweke mwanadamu huru kutoka katika nguvu zake.
18 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali. 19 Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu. 20 Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu.
21 Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.
22 “Yeye hakutenda dhambi,
wala hila haikuonekana kinywani mwake.”
23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa. 25 Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.