Petro Anawaandikia Tena Wakristo Wayahudi na wa Mataifa
Petro, akitarajia kufa karibuni kama shahidi wa imani, anawaandikia Wakristo Wayahudi na Wakristo wa Mataifa waliotawanyika huko Ponto, Galatia, Kapadokia na nchi nyingine. Anaandika ili kuthibitisha mafundisho na maagizo ya barua yake ya awali, na kuwaonya dhidi ya makosa ya walimu wa uongo kwa kuwakumbusha hukumu za Mungu juu ya walioiasi imani. Anawatia moyo wanapoteswa kwa kuelekeza fikira zao kwenye wokovu wenye furaha wa wale waliomtumaini Mungu, na kwenye mwisho kabisa wa ulimwengu huu na wa mfumo wa kidini wa Wayahudi.
66 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Petro Anawasalimu Tena Wakristo Wayahudi na wa Mataifa
Salamu na baraka za Petro. Aliwekwa kuwa mtume kwa Wayahudi na watu wa Mataifa na Yesu Kristo, ambaye amewapa mitume nguvu za kimungu kupitia vipawa vya Roho Mtakatifu, ili waweze kuwaongoza watu kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. Haya hupatikana kwa kumjua Kristo Yesu (Yohana 17:3), ambaye amewaita kwenye utukufu wa kuwa mitume wake, akawajaza nguvu na ujasiri kwa kusudi hilo, na kuwakabidhi ahadi zote tukufu za injili, ili mwanadamu apate tena kushiriki katika asili takatifu isiyokufa, baada ya kuuepuka uharibifu uliomo duniani unaosababishwa na tamaa mbaya. Wanapaswa kuongeza kwenye imani yao ujasiri wa kweli na uthabiti wa nia wanapoteswa kwa sababu ya imani yao, huku wakizidi kuyajua mafundisho ya Kristo; kwenye ujuzi waongeze kiasi katika anasa zote za duniani, uvumilivu katika dhiki, na uchaji kwa Mungu; na kwenye uchaji wa Mungu waongeze upendo kwa ndugu zao Wakristo, na kwenye upendo kwa ndugu waongeze upendo kwa watu wote, bila kuwaacha hata maadui zao. Mambo haya yakizidi kuwa mengi ndani yao, hawatakuwa wavivu wala wasiokuwa na matunda katika matendo mema. Lakini yeyote asiye na matendo mema na fadhila za Kikristo zinazotendeka maishani ni kipofu kwa makusudi, anayeifumbia macho nuru na kuchagua kusahau nadhiri yake ya ubatizo ya kujitakasa kutokana na dhambi zake za zamani. Kwa kuwa hali hii inawahusu wengi, wanahimizwa kujitahidi hata zaidi kuthibitisha kuitwa na kuchaguliwa kwao kupitia injili kuwa wana wa Mungu na wa kanisa lake, kwa kutenda matendo mema kupitia imani. Wakiyatekeleza mambo haya, Mungu atawategemeza kwa neema yake na kuwajalia kuingia kwa heshima na ushindi katika ufalme wake wa milele.
1 Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo:
Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:
2 Neema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; 6 katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; 7 katika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo. 8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, na ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, 11 na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Petro Alishuhudia Ukuu wa Kristo
Kwa kuwa kutenda fadhila za Kikristo kwa imani ndiyo njia pekee ya kuingia katika ufalme wa Kristo, Petro anasema kwamba anaona inafaa kwa huduma yake ya kitume, maadamu yumo mwilini, kuwakumbusha kweli hizi, ambazo tayari wamesimama imara katika hizo, na kuwahimiza kuzitenda. Akijua kwamba kifo chake kinakaribia (Yohana 21:18–19), anajitahidi kwa kuwaandikia kuwasaidia kuendelea kuyakumbuka mambo haya daima baada ya yeye kuuacha mwili. Kwa maana walipowajulisha nguvu na kuonekana kwa Yesu Kristo, hawakutangaza “ngano zilizotungwa kwa werevu,” kama hadithi za wapagani kuhusu miungu yao kuonekana duniani katika umbo la binadamu. Petro mwenyewe, pamoja na Yakobo na Yohana, aliuona ukuu wake juu ya mlima mtakatifu, Mungu alipomtangaza kutoka katika utukufu wake mkuu kuwa ni Mwana wake. Sauti hiyo na kubadilika kwa sura yake vilithibitisha unabii mbalimbali wa Agano la Kale kuhusu Kristo. Wanapaswa kuuzingatia unabii huo kama nuru iliyowaongoza wanadamu katika hali yao ya kutojua mambo ya kiroho, mpaka siku ya injili itakapopambazuka na nyota ya asubuhi ya haki itakapozuka katika nafsi zao. Wanapaswa kujua kwamba hakuna unabii unaotokana na msukumo au utunzi wa mtu binafsi. Kwa maana zamani unabii haukuletwa katika akili za wale walioutamka kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu watakatifu wa Mungu walitangaza makusudi ya mapenzi yake wakiongozwa, au kuvuviwa, na Roho Mtakatifu.
12 Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo. 13 Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niwapo katika hema hili ambalo ni mwili wangu, 14 kwa sababu najua ya kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Yesu Kristo alivyoliweka wazi kwangu. 15 Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.
16 Tulipowafahamisha juu ya uweza na kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake. 17 Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.” 18 Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.
19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
Walimu wa Uongo na Hukumu ya Hakika ya Mungu
Petro anatabiri kwamba kama walivyokuwa manabii wa uongo miongoni mwa Wayahudi, waliowapotosha wengi, wakimkana Mungu aliyewakomboa kutoka utumwani Misri, vivyo hivyo kutakuwa na walimu wa uongo katika kanisa la Kikristo. Wataingiza kwa siri mafundisho yao ya uzushi yenye kuangamiza, wakimkana Bwana aliyewanunua kwa damu yake kutoka utumwani mwa dhambi na mauti (Kutoka 15:16; Kumbukumbu la Torati 32:6), na kujiletea maangamizi. Wengi watawafuata, nao kwa maisha yao maovu watafanya injili ikufuriwe, wakifanya biashara ya nafsi za watu. Adhabu yao, iliyotangazwa dhidi ya dhambi tangu mwanzo, haikawii, bali itawafikia upesi. Kwa maana Mungu hakuwaachilia malaika waliotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu, akiwashikilia mpaka siku ya hukumu katika mahali pa mateso na giza ambapo hawakuweza kutoroka. Hakuuachilia ulimwengu wa kale wala miji ya Sodoma na Gomora, bali aliifanya kuwa mfano wa adhabu itakayowapata wasiomcha Mungu siku ya mwisho. Kutokana na kuokolewa kwa Noa na Loti kimuujiza, Petro anathibitisha kwamba kwa hakika Mungu angewaokoa katika majaribu na hatari wale wanaomtumaini na walio watumishi wake waaminifu, kama vile ambavyo angewaangamiza walimu wa uongo na wasiotii kwa maangamizi ya milele.
1 Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. 2 Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. 3 Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.
4 Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; 5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; 6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; 7 na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu 8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): 9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu.
Walimu wa Uongo Katika Njia ya Balaamu
Petro anaeleza tabia ya walimu wa uongo. Kama wanyama wasio na akili, wanaofuata silika ya asili yao ya kinyama, walioumbwa kukamatwa na kuangamizwa kwa sababu wanaangamiza, wanayatukana mambo wasiyoyaelewa, nao wataangamia katika mafundisho na matendo yao wenyewe yaliyopotoka. Wanaonyesha maovu yao waziwazi. Wana hatia ya uasherati katika karamu zao za upendo. Wanazishawishi nafsi ambazo hazijaimarika katika imani kwa wazo kwamba Meza ya Bwana ilianzishwa ili kuendeleza mapenzi ya kimwili, nao ni wataalamu katika kila mbinu ya ushawishi wa dhambi na udanganyifu. Wanafuata njia ya Balaamu, ambaye (Hesabu 31:16; Ufunuo 2:14) alitenda kinyume na ujuzi na dhamiri yake ili apate ujira wa uovu alioahidiwa.
10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.
Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni. 11 Lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana. 12 Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.
13 Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki katika karamu zenu. 14 Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! 15 Wameiacha njia iliyonyooka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. 16 Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, akaongea akitumia sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.
Chemchemi Zisizo na Maji, Watumwa wa Uharibifu
Petro anawafananisha walimu wa uongo na chemchemi zisizo na maji, na mawingu yanayoahidi mvua lakini yanaishia kuwa dhoruba na kuharibu badala ya kutimiza matumaini ya watu. Kwa kuruhusu kila aina ya ufuska, wanawavuta wale waliojitenga na wapagani wawe wanafunzi wao. Wanaahidi uhuru wa kutimiza tamaa zao bila kizuizi, ilhali mwenendo wao wenyewe unaonyesha kwamba wao ni watumwa wa uharibifu. Kwa maana yeyote anayeshindwa na tamaa zake huwa mtumwa wa tamaa hizo. Kwa wale waliogeuzwa kwa ujuzi wa injili waache ibada ya sanamu na ufuska wa ulimwengu wa kipagani, kisha wakanaswa tena katika hayo, unajisi wao wa baadaye utakuwa wenye kuleta mauti zaidi kuliko ule wa kwanza, kwa maana wametenda dhambi dhidi ya nuru na mapendeleo makubwa zaidi ya kiroho.
17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18 Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi. 19 Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala. 20 Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. 21 Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. 22 Imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
Walimu wa Uongo Wanaokana Kuja kwa Kristo
Petro anaonyesha kwamba kusudi lake la kuandika barua zake mbili lilikuwa kuwakumbusha utabiri wa manabii wa kale (Zaburi 1:1; Danieli 12:2) na mafundisho na maagizo ya mitume yaliyojengwa juu ya utabiri huo. Anajua kwamba manabii walitabiri kutokea kwa walimu wa uongo ambao wangekana kwamba Kristo atakuja kuuhukumu ulimwengu (Yeremia 17:15; Ezekieli 12:22–27; Yuda 1:14–15; Danieli 12:2). Wanapuuza kwa makusudi kwamba anga, au tabaka la hewa, na dunia viliumbwa kwa neno la Mungu kutoka majini, na kwamba ulimwengu ulikuwa tayari umeangamizwa kwa maji hayo kwa sababu ya uovu wa mwanadamu. Dunia ya sasa na tabaka lake la hewa, vinavyoendelea kuwapo kwa njia hiyohiyo, vinaweza kukabiliwa na maangamizi yaleyale kwa sababu ileile. Lakini vimewekwa akiba na kuhifadhiwa visiangamizwe kwa gharika ya maji, ili viteketezwe kwa gharika ya moto siku ya kulipiza kisasi na hukumu.
1 Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. 2 Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.
3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya. 4 Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
Siku ya Bwana Itakuja Kama Mwizi
Petro anawahimiza ndugu Wakristo wasidanganywe na wenye kudhihaki, ambao walihitimisha kutokana na kukawia kwa Mungu kwamba hakuwa na nguvu au nia ya kutimiza ahadi zake. Wanapaswa kukumbuka kwamba hakuna kipindi cha wakati, hata kiwe kirefu kiasi gani, kinachoweza kulinganishwa na umilele wa Mungu, na kwamba hakuna kipindi cha wakati kinachoweza kubadili makusudi yake (Zaburi 90:4). Kuja kwa Bwana hakukawii kwa sababu iliyotolewa na walimu hao, bali kwa sababu ya uvumilivu wake na kwa kuwa hataki yeyote aangamie. Hata hivyo, siku ya Bwana, hata ikikawia kiasi gani, hakika itakuja kwa ghafla, ikiwavamia watu kama mwizi usiku (Mathayo 24:43). Ndipo anga lote pamoja na mivuke yake litatoweka kwa moto, kwa kishindo kikubwa na milipuko, na elementi zinazovifanyiza zitawashwa moto na kutenganishwa, na muundo wote wa vitu vinavyoonekana, pamoja na kazi zake zote za asili na za ustadi wa wanadamu, utateketezwa kabisa. Kwa kuwa vitu vyote vya duniani vitayeyushwa, wana sababu zenye nguvu kabisa za kuishi maisha matakatifu na kumcha Mungu, wakiitamani siku ya Mungu ije badala ya kuiogopa, wakati mfumo huu wa duniani utakapoyeyushwa. Kwa maana, kulingana na ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu na uzao wake wa kiroho (Warumi 4:13–16; Isaya 65:17–23; 66:22), wanapaswa kutazamia “mbingu mpya na dunia mpya” (Ufunuo 21:27; 22:14–15), makao ya milele ya roho zilizobarikiwa.
8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.
11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
Mkutwe Watakatifu Kristo Atakapokuja
Kwa kuwa Wakristo wote wameahidiwa urithi wa Kanaani ya milele, yaani mbingu mpya na dunia mpya (Luka 20:35), Petro anawahimiza wajitahidi kwa bidii ili Kristo, Hakimu wa walio hai na waliokufa, awakute wakiwa watakatifu, wasio na hatia na wenye manufaa katika maisha yao, na wakiwa na amani naye. Wanapaswa kuchukulia kuchelewa kwa kuja kwake kuwa uthibitisho wa kusudi lake kwamba watu wote waokolewe, kama Paulo alivyowaandikia kwa uvuvio wa kimungu (Waefeso 2:3, 4, 5; Wakolosai 1:21; 1 Wathesalonike 3:13; 4:14–18; 2 Wathesalonike 1:7–10; Tito 2:13). Paulo aliandika pia kuhusu ufufuo wa wafu (1 Wakorintho 15:22; Wafilipi 3:20–21), kuteketezwa kwa dunia kwa moto (2 Wathesalonike 1:8), nchi ya mbinguni ambako wenye haki hukaa (1 Wathesalonike 4:17; Waebrania 4:9; 12:14, 18, 24) na hukumu ya watu wote (Warumi 14:10). Baadhi ya mambo haya ni magumu kwa wanadamu kuyaelewa, na wasio na elimu na wale ambao hawajaimarika katika imani huyapotosha, kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko, kwa maangamizi yao wenyewe, wakiharibu maadili ya watu. Lakini wao, kwa kuwa wameonywa mapema na mitume na manabii kuhusu mafundisho haya ya uongo, wanapaswa kujilinda dhidi yake, wakikua kila siku katika ujuzi wa mafundisho ya Yesu Kristo, na kumpa utukufu sasa na hata siku ya milele.
14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari. 15 Hesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. 16 Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.
17 Basi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu. 18 Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.