Kuangamizwa kwa Tiro
587 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, kwa sababu Tiro amesema kuhusu Yerusalemu, ‘Aha! Lango la kwenda kwa mataifa limevunjika, nayo milango yake iko wazi mbele yangu, sasa kwa kuwa amekuwa magofu nitastawi.’ 3 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi niko kinyume na wewe, ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi dhidi yako, kama bahari inayovurumisha mawimbi yake. 4 Watavunja kuta za Tiro na kuibomoa minara yake, nitakwangua udongo wake na kuufanya mwamba mtupu. 5 Itakuwa huko katikati ya bahari patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki, kwa maana nimenena, asema Bwana Mwenyezi. Atakuwa nyara kwa mataifa, 6 nayo makao yake huko bara yataangamizwa kwa upanga. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.
7 “Kwa maana hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kutoka kaskazini nitamleta dhidi ya Tiro Mfalme Nebukadneza wa Babeli, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi na magari ya vita, wapanda farasi na jeshi kubwa. 8 Atayaharibu makao yako huko bara kwa upanga, ataweka jeshi kukuzingira, atakuzingira mpaka kwenye kuta za ngome zako na kuinua ngao zake dhidi yako. 9 Ataelekeza mapigo ya vyombo vyake vya kubomolea dhidi ya kuta zako na kubomoa minara yako kwa silaha zake. 10 Farasi zake zitakuwa nyingi sana kiasi kwamba utafunikwa na mavumbi watakayotimua. Kuta zako zitatikisika kwa mshindo wa farasi wa vita, magari makubwa na magari ya vita wakati aingiapo malango yako kama watu waingiao mji ambao kuta zake zimebomolewa kote.
11 “Kwato za farasi zake zitakanyaga barabara zako zote, atawaua watu wako kwa upanga na nguzo zako zilizo imara zitaanguka chini. 12 Watateka utajiri wako na kuchukua nyara bidhaa zako, watazivunja kuta zako na kuzibomoa nyumba zako nzuri, watatupa baharini mawe yako, mbao zako na kifusi chako. 13 Nitakomesha kelele za nyimbo zako, na uimbaji wako wa kinubi kamwe hautasikika tena. 14 Nitakufanya mwamba mtupu, nawe utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za kuvulia samaki. Kamwe hutajengwa tena, kwa maana Mimi Bwana nimenena, asema Bwana Mwenyezi.
15 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa Tiro: ‘Je, nchi za pwani hazitatetemeka kwa kishindo cha anguko lako, wakati majeruhi wanapolia kwa maumivu makali na wakati mauaji yanaendelea ndani yako? 16 Ndipo wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka kutoka kwenye viti vyao vya enzi na kuweka kando majoho yao na kuvua nguo zao zilizotariziwa. Wakiwa wamevikwa hofu kuu, wataketi chini ardhini, wakiwa wanatetemeka kila dakika na wakikustajabia. 17 Ndipo wao watakuombolezea na kukuambia:
“ ‘Tazama jinsi ulivyoharibiwa,
ee mji uliokuwa na sifa,
wewe uliyekaliwa na mabaharia!
Ulikuwa na nguvu kwenye bahari,
wewe na watu wako;
wote walioishi huko,
uliwatia hofu kuu.
18 Sasa nchi za pwani zinatetemeka
katika siku ya anguko lako;
visiwa vilivyomo baharini
vinaogopa kwa kuporomoka kwako.’
19 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitakapokufanya uwe mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa tena na watu, nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako na maji yake makuu yatakapokufunika, 20 ndipo nitakapokushusha chini pamoja na wale washukao shimoni, kwa watu wa kale, nami nitakufanya uishi katika pande za chini za nchi kama katika magofu ya kale, pamoja na wale washukao shimoni, nawe hutarudi au kurejea kwenye makao yako katika nchi ya walio hai. 21 Nitakufikisha mwisho wa kutisha wala hutakuwepo tena. Watu watakutafuta, lakini kamwe hutaonekana tena, asema Bwana Mwenyezi.”
27:1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro. 3 Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Ee Tiro, wewe umesema,
“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”
4 Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari,
wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.
5 Walizifanya mbao zako zote
kwa misunobari itokayo Seniri;
walichukua mierezi kutoka Lebanoni
kukutengenezea mlingoti.
6 Walichukua mialoni toka Bashani
wakakutengenezea makasia yako;
kwa miti ya msanduku
kutoka pwani ya Kitimu
wakatengeneza sitaha yako
na kuipamba kwa pembe za ndovu.
7 Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako,
nacho kilikuwa bendera yako;
chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau
kutoka visiwa vya Elisha.
8 Watu kutoka Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako;
watu wako wenye ustadi, ee Tiro,
walikuwa ndio mabaharia wako.
9 Wazee wa Gebali pamoja na mafundi stadi
walikuwa mafundi wako melini.
Meli zote za baharini na mabaharia wao
walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.
10 “ ‘Watu wa Uajemi, Ludi na Putu
walikuwa askari katika jeshi lako.
Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako,
wakileta fahari yako.
11 Watu wa Arvadi na wa Heleki
walikuwa juu ya kuta zako pande zote;
watu wa Gamadi
walikuwa kwenye minara yako.
Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako;
wakaukamilisha uzuri wako.
12 “ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali zako.
13 “ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, walibadilisha watumwa na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.
14 “ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali zako.
15 “ ‘Watu wa Dedani walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.
16 “ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe na akiki nyekundu.
17 “ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe, walibadilishana kwa ngano kutoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri ya kuponyeshea.
18 “ ‘Dameski, kwa sababu ya wingi wa kazi za mikono yako na ukuu wa utajiri wa mali, walifanya biashara nawe wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.
19 “ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali, walikuletea mali za biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.
20 “ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.
21 “ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako waliobadilishana bidhaa zako na wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi.
22 “ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezi, vito vya thamani na dhahabu.
23 “ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. 24 Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara.
25 “ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo
zinazokusafirishia bidhaa zako.
Umejazwa shehena kubwa
katika moyo wa bahari.
26 Wapiga makasia wako wanakupeleka
mpaka kwenye maji makavu.
Lakini upepo wa mashariki umekuvunja vipande vipande
katika moyo wa bahari.
27 Utajiri wako, bidhaa zako na mali zako,
mabaharia wako, manahodha wako,
mafundi wako wa meli,
wafanyabiashara wako na askari wako wote,
na kila mmoja aliyeko melini
atazama kwenye moyo wa bahari
siku ile ya kuvunjika kwa meli yako.
28 Nchi za pwani zitatetemeka
wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.
29 Wote wapigao makasia
wataacha meli zao,
mabaharia wote na wanamaji wote
watasimama pwani.
30 Watapaza sauti zao
na kulia sana kwa ajili yako;
watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao
na kujivingirisha kwenye majivu.
31 Watanyoa nywele zao kwa ajili yako,
nao watavaa nguo za magunia.
Watakulilia kwa uchungu wa moyo
na kwa maombolezo makuu.
32 Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako,
watafanya maombolezo kukuhusu wakisema:
“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro,
katika moyo wa bahari?”
33 Wakati bidhaa zako zilipotoka baharini,
ulitosheleza mataifa mengi;
kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako
ulitajirisha wafalme wa dunia.
34 Sasa umevunjavunjwa na bahari,
katika vilindi vya maji,
bidhaa zako na kundi lako lote
vimezama pamoja nawe.
35 Wote waishio katika nchi za pwani
wanakustaajabia;
wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu,
nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.
36 Wafanyabiashara miongoni mwa mataifa wanakucheka;
umefikia mwisho wa kutisha
nawe hutakuwepo tena.’ ”