Kuangamizwa kwa Tiro (continued)

587 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 28

1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna

na umesema, “Mimi ni mungu;

nami ninaketi katika kiti cha enzi cha mungu

katika moyo wa bahari.”

Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,

ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.

3 Je, wewe una hekima kuliko Danieli?

Je, hakuna siri iliyofichika kwako?

4 Kwa hekima yako na ufahamu wako,

umejipatia utajiri,

nawe umejikusanyia dhahabu

na fedha katika hazina zako.

5 Kwa werevu wako mwingi katika biashara,

umeongeza utajiri wako

na kwa sababu ya utajiri wako

moyo wako umekuwa na kiburi.

6 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,

mwenye hekima kama mungu,

7 mimi nitawaleta wageni dhidi yako,

taifa katili kuliko yote;

watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,

na kuchafua fahari yako inayongʼaa.

8 Watakushusha chini shimoni,

nawe utakufa kifo cha kikatili

katika moyo wa bahari.

9 Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”

mbele ya wale wanaokuua?

Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,

mikononi mwa hao wanaokuua.

10 Utakufa kifo cha wasiotahiriwa

kwa mkono wa wageni.

Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

11 Neno la Bwana likanijia kusema: 12 “Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu,

ukiwa umejaa hekima

na mkamilifu katika uzuri.

13 Ulikuwa ndani ya Edeni,

bustani ya Mungu;

kila kito cha thamani kilikupamba:

akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi,

krisolitho, shohamu na yaspi,

yakuti samawi, almasi na zabarajadi.

Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake

kulifanywa kwa dhahabu;

siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.

14 Ulitiwa mafuta kuwa kerubi mlinzi,

kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu.

Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu;

ulitembea katikati ya vito vya moto.

15 Ulikuwa mnyofu katika njia zako

tangu siku ile ya kuumbwa kwako,

hadi uovu ulipoonekana ndani yako.

16 Kutokana na biashara yako iliyoenea,

ulijazwa na dhuluma,

nawe ukatenda dhambi.

Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu,

nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi,

kutoka katikati ya vito vya moto.

17 Moyo wako ukawa na kiburi

kwa ajili ya uzuri wako,

nawe ukaiharibu hekima yako

kwa sababu ya fahari yako.

Kwa hiyo nikakutupa chini;

nimekufanya kioja mbele ya wafalme.

18 Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma,

umenajisi mahali pako patakatifu.

Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako,

nao ukakuteketeza,

nami nikakufanya majivu juu ya nchi,

machoni pa wote waliokuwa wakitazama.

19 Mataifa yote yaliyokujua

yanakustajabia;

umefikia mwisho wa kutisha

na hutakuwepo tena milele.’ ”

20 Neno la Bwana likanijia kusema: 21 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake, 22 nawe useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Mimi ni kinyume chako, ee Sidoni,

nami nitapata utukufu ndani yako.

Nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana,

nitakapotekeleza hukumu zangu

na kuonyesha utakatifu wangu ndani yake.

23 Nitapeleka tauni ndani yake

na kufanya damu itiririke katika barabara zake.

Waliochinjwa wataanguka ndani yake,

kwa upanga dhidi yake kila upande.

Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.

24 “ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.

25 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka mataifa ambako wametawanyika, nitajionyesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo. 26 Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wao.’ ”

Maombolezo ya Ezekieli kwa Ajili ya Farao

Unabii dhidi ya Misri.

Ezekieli 32:1–16

1 Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema: 2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie:

“ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa,

wewe ni kama joka kubwa baharini,

unayevuruga maji kwa miguu yako

na kuchafua vijito.

3 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu

nitautupa wavu wangu juu yako,

nao watakukokota katika wavu wangu.

4 Nitakutupa nchi kavu

na kukuvurumisha uwanjani.

Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako

na wanyama wote wa nchi

watajishibisha nyama yako.

5 Nitatawanya nyama yako juu ya milima

na kujaza mabonde kwa mabaki yako.

6 Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka

njia yote hadi milimani,

nayo mabonde yatajazwa na nyama yako.

7 Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu

na kuzitia nyota zake giza;

nitalifunika jua kwa wingu,

nao mwezi hautatoa nuru yake.

8 Mianga yote itoayo nuru angani

nitaitia giza juu yako;

nitaleta giza juu ya nchi yako,

asema Bwana Mwenyezi.

9 Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi

nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa,

nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi

ambazo haujapata kuzijua.

10 Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie,

wafalme wao watatetemeka

kwa hofu kwa ajili yako

nitakapotikisa upanga wangu mbele yao.

Siku ya anguko lako

kila mmoja wao atatetemeka

kila dakika kwa ajili ya maisha yake.

11 “ ‘Kwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli

utakuja dhidi yako.

12 Nitafanya makundi yako ya wajeuri kuanguka

kwa panga za watu mashujaa,

taifa katili kuliko mataifa yote.

Watakivunjavunja kiburi cha Misri,

nayo makundi yake yote

ya wajeuri yatashindwa.

13 Nitaangamiza mifugo yake yote

wanaojilisha kando ya maji mengi,

hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu

wala kwato za mnyama

hazitayachafua tena.

14 Kisha nitafanya maji yake yatulie

na kufanya vijito vyake

vitiririke kama mafuta,

asema Bwana Mwenyezi.

15 Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa

na kuiondolea nchi kila kitu

kilichomo ndani yake,

nitakapowapiga wote waishio humo,

ndipo watakapojua kuwa

Mimi ndimi Bwana.’

16 “Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote ya wajeuri wataliimba, asema Bwana Mwenyezi.”