Ezekieli: Misri Inashuka Shimoni

Unabii dhidi ya Misri.

587 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 32:17–32

17 Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema: 18 “Mwanadamu, omboleza kwa ajili ya makundi ya wajeuri wa Misri na uwatupe kuzimu yeye na binti za mataifa yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao shimoni. 19 Je, ninyi mnamzidi nani kwa uzuri? Shukeni chini! Nanyi mkalazwe pamoja na hao wasiotahiriwa! 20 Wataanguka miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga. Upanga umefutwa, mwache aburutwe mbali pamoja na hao wajeuri wake wote. 21 Kutoka kuzimu viongozi hodari watanena kuhusu Misri pamoja na wale walioungana nao, ‘Wameshuka chini, nao wamelala kimya pamoja na hao wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.’

22 “Ashuru yuko huko pamoja na jeshi lake lote, amezungukwa na makaburi ya watu wake wote waliouawa, wale wote walioanguka kwa upanga. 23 Makaburi yao yako kwenye kina cha chini cha shimo na jeshi lake limelala kulizunguka kaburi lake. Wote waliokuwa wameeneza hofu kuu katika nchi ya walio hai wameuawa, wameanguka kwa upanga.

24 “Elamu yuko huko, pamoja na makundi yake yote ya wajeuri wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote wameuawa, wameanguka kwa upanga. Wote waliokuwa wameeneza hofu katika nchi ya walio hai walishuka kuzimu bila kutahiriwa. Wanaichukua aibu yao pamoja na wale washukao shimoni. 25 Kitanda kimetandikwa kwa ajili yake miongoni mwa waliouawa, pamoja na makundi yake yote ya wajeuri wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote ni watu wasiotahiriwa, wameuawa kwa upanga. Kwa sababu vitisho vyao vilienea katika nchi ya walio hai, wameichukua aibu yao pamoja na wale washukao shimoni, nao wamewekwa miongoni mwa waliouawa.

26 “Mesheki na Tubali wako humo, pamoja na makundi yao ya wajeuri wakiwa wameyazunguka makaburi yao. Wote hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga kwa sababu walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. 27 Je, hawakulala na mashujaa wengine wasiotahiriwa waliouawa, ambao wameshuka kaburini wakiwa na silaha zao za vita, ambao panga zao ziliwekwa chini ya vichwa vyao na uovu wao juu ya mifupa yao? Adhabu kwa ajili ya dhambi zao ilikuwa juu ya mifupa yao, ingawa vitisho vya mashujaa hawa vilikuwa vimeenea hadi kwenye nchi ya walio hai.

28 “Wewe pia, ee Farao, utavunjwa nawe utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.

29 “Edomu yuko humo, wafalme wake wote na wakuu wake wote, ambao ijapokuwa wana nguvu, wamelazwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga. Wamelala pamoja na wasiotahiriwa, pamoja na wale washukao shimoni.

30 “Wakuu wote wa kaskazini na Wasidoni wote wako huko, wameshuka chini pamoja na waliouawa kwa aibu ijapokuwa kuna vitisho vilivyosababishwa na nguvu zao. Wamelala bila kutahiriwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga na kuchukua aibu yao pamoja na wale washukao chini shimoni.

31 “Farao, yeye pamoja na jeshi lake lote, atakapowaona atafarijiwa kwa ajili ya makundi yake yote ya wajeuri, wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mwenyezi. 32 Ingawa nilimfanya Farao aeneze vitisho vyake katika nchi ya walio hai, Farao pamoja na makundi yake yote ya wajeuri watalazwa miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mwenyezi.”

Wito kwa Mateka Huko Babeli

Ezekieli 33:1–20

1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, sema na watu wako uwaambie, ‘Nitakapoleta upanga dhidi ya nchi, nao watu wa nchi wakamchagua mmoja wa watu wao na kumfanya awe mlinzi wao, 3 naye auonapo upanga unakuja dhidi ya nchi na kupiga tarumbeta kuonya watu, 4 kama mtu yeyote asikiapo sauti ya tarumbeta hakukubali kuonywa, basi upanga ujapo na kuutoa uhai wake, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. 5 Kwa kuwa alisikia sauti ya tarumbeta lakini hakukubali maonyo, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kama angekubali maonyo, angelijiokoa mwenyewe. 6 Lakini kama mlinzi akiona upanga unakuja na asipige tarumbeta kuonya watu na upanga ukija na kutoa uhai wa mmoja wao, yule mtu ataondolewa kwa sababu ya dhambi yake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.’

7 “Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu. 8 Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako. 9 Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.

10 “Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’ 11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’

12 “Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki, kama akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’ 13 Kama nikimwambia mtu mwenye haki kwamba hakika utaishi, lakini akategemea hiyo haki yake na kutenda uovu, hakuna tendo lolote la haki alilotenda litakalokumbukwa, atakufa kwa ajili ya uovu alioutenda. 14 Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, 15 kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. 16 Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi.

17 “Lakini watu wako wanasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini ni njia zao ambazo si sawa. 18 Kama mtu mwenye haki akigeuka kutoka uadilifu wake na kufanya uovu, atakufa kwa ajili ya huo uovu. 19 Naye mtu mwovu kama akigeuka kutoka uovu wake na kufanya lile lililo haki na sawa, kwa kufanya hivyo ataishi. 20 Lakini, ee nyumba ya Israeli, unasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini nitamhukumu kila mmoja wenu sawasawa na njia zake mwenyewe.”