Sehemu ya 4: Matukio Huko Babeli Hadi Kurudi Kutoka Uhamishoni
Matukio huko Babeli, kuanzia kuharibiwa kwa Yerusalemu hadi kurudi kutoka uhamishoni.
Ezekieli Anasikia Habari za Kuanguka kwa Yerusalemu
Ezekieli, baada ya kuambiwa kuhusu kuangamizwa kwa Yerusalemu, anatabiri ukiwa kamili wa Uyahudi na hukumu za Mungu juu ya mataifa yanayozunguka ambayo ni maadui wa Wayahudi.
587 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
21 Mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mwezi wa kumi, siku ya tano, mtu aliyekuwa ametoroka kutoka Yerusalemu akanijia na kusema, “Mji wa Yerusalemu umeanguka!” 22 Basi jioni kabla mtu huyo hajaja, mkono wa Bwana, ulikuwa juu yangu, naye alifungua kinywa changu kabla ya mtu yule aliyenijia asubuhi hajafika. Basi kinywa changu kilifunguliwa na sikuweza tena kunyamaza.
23 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema: 24 “Mwanadamu, watu wanaoishi katika magofu hayo katika nchi ya Israeli wanasema hivi, ‘Abrahamu alikuwa mtu mmoja tu, hata hivyo akaimiliki nchi. Lakini sisi ni wengi, hakika tumepewa nchi kuwa milki yetu.’ 25 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa mnakula nyama pamoja na damu na kuinulia sanamu zenu macho na kumwaga damu, je, mtaimiliki nchi? 26 Mnategemea panga zenu, mnafanya mambo ya machukizo na kila mmoja wenu humtia unajisi mke wa jirani yake. Je, mtaimiliki nchi?’
27 “Waambie hivi: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Hakika kama niishivyo, wale waliobaki katika magofu wataanguka kwa upanga, wale walio nje mashambani nitawatoa wararuliwe na wanyama pori, nao wale walio katika ngome na kwenye mapango watakufa kwa tauni. 28 Nitaifanya nchi kuwa ukiwa na utupu na kiburi cha nguvu zake zitafikia mwisho, nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa ili mtu yeyote asipite huko. 29 Kisha watajua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapokuwa nimeifanya nchi kuwa ukiwa na utupu kwa sababu ya mambo yote ya machukizo waliyotenda.’
30 “Kwa habari yako wewe, mwanadamu, watu wako wanaongea habari zako wakiwa karibu na kuta na kwenye milango ya nyumba, wakiambiana kila mmoja na mwenzake, ‘Njooni msikie ujumbe ule utokao kwa Bwana.’ 31 Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali. 32 Naam, mbele yao umekuwa tu kama yeye aimbaye nyimbo za mapenzi kwa sauti nzuri za kuvutia na kupiga vyombo kwa ustadi, kwa kuwa wanasikia maneno yako lakini hawayatendi.
33 “Wakati mambo haya yote yatakapotimia, kwa kuwa hakika yatatokea, ndipo watakapojua kwamba nabii amekuwepo miongoni mwao.”
1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao. 3 Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa, na juu ya watu wa Yuda walipokwenda uhamishoni, 4 kwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao katikati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. 5 Nitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. 6 Kwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umepiga makofi yako na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli, 7 hivyo nitaunyoosha mkono wangu dhidi yako na kukutoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitakukatilia mbali kutoka kwenye mataifa na kukungʼoa katika nchi. Nitakuangamiza, nawe utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”
8 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Moabu na Seiri wamesema, “Tazama, nyumba ya Yuda imekuwa kama mataifa mengine yote,” 9 kwa hiyo nitaiondoa ile miji iliyo kando ya Moabu, kuanzia miji iliyoko mipakani, yaani: Beth-Yeshimothi, Baal-Meoni na Kiriathaimu, iliyo utukufu wa nchi hiyo. 10 Nitaitia Moabu pamoja na Waamoni mikononi mwa watu wa Mashariki kuwa milki yao, ili kwamba Waamoni wasikumbukwe miongoni mwa mataifa, 11 nami nitatoa adhabu kwa Moabu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”
12 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Edomu ulilipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda na kukosa sana kwa kufanya hivyo, 13 kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaunyoosha mkono wangu dhidi ya Edomu na kuua watu wake na wanyama wao. Nitaufanya ukiwa, kuanzia Temani hadi Dedani wataanguka kwa upanga. 14 Nitalipiza Edomu kisasi kwa mkono wa watu wangu Israeli, nao watawatendea Edomu sawasawa na hasira yangu na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana Mwenyezi.’ ”
15 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Wafilisti wamewalipiza kisasi kwa uovu wa mioyo yao na kwa uadui wa siku nyingi wakataka kuangamiza Yuda, 16 kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ninakaribia kuunyoosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi na kuwaangamiza wale waliosalia katika pwani. 17 Nitalipiza kisasi kikubwa juu yao na kuwaadhibu katika ghadhabu yangu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapolipiza kisasi juu yao.’ ”