Yeremia Anatabiri Dhidi ya Misri

587 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 43:8–13

8 Huko Tahpanhesi neno la Bwana likamjia Yeremia kusema: 9 “Wayahudi wakiwa wanaona, chukua baadhi ya mawe makubwa na kuyazika katika udongo wa mfinyanzi katika njia iliyojengwa kwa matofali katika ingilio la jumba la kifalme la Farao huko Tahpanhesi. 10 Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Nitamtumania mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, nami nitakiweka kiti chake cha enzi juu ya haya mawe niliyoyazika hapa, naye atatandaza hema yake ya ufalme juu yake. 11 Atakuja na kuishambulia Misri, akiwaua wale waliokusudiwa kuuawa, awateke mateka wale waliokusudiwa kutekwa, na upanga kwa wale waliokusudiwa upanga. 12 Atachoma moto mahekalu yao ya miungu ya Misri, atachoma mahekalu yao na kuteka miungu yao. Kama vile mchungaji ajizungushiavyo vazi lake ndivyo atakavyojizungushia Misri na kuondoka mahali hapo bila kudhurika. 13 Humo ndani ya hekalu la jua nchini ya Misri atabomoa nguzo za ibada, na kuteketeza kwa moto mahekalu ya miungu wa Misri.’ ”

Yeremia 46:13–28

13 Huu ndio ujumbe Bwana aliomwambia nabii Yeremia kuhusu kuja kwa Nebukadneza mfalme wa Babeli ili kuishambulia Misri:

14 “Tangaza hili katika Misri, nawe ulihubiri katika Migdoli,

hubiri pia katika Memfisi na Tahpanhesi:

‘Shikeni nafasi zenu na mwe tayari,

kwa kuwa upanga unawala wale wanaokuzunguka.’

15 Kwa nini mashujaa wako wamesombwa

na kupelekwa mbali?

Hawawezi kusimama, kwa maana Bwana

atawasukuma awaangushe chini.

16 Watajikwaa mara kwa mara,

wataangukiana wao kwa wao.

Watasema, ‘Amka, turudi

kwa watu wetu na nchi yetu,

mbali na upanga wa mtesi.’

17 Huko watatangaza,

‘Farao mfalme wa Misri ni makelele tu,

amekosa wasaa wake.’

18 “Kwa hakika kama niishivyo,” asema Mfalme,

ambaye jina lake ni Bwana Mwenye Nguvu Zote,

“mmoja atakuja ambaye ni kama Tabori miongoni mwa milima,

kama Karmeli kando ya bahari.

19 Funga mizigo yako kwenda uhamishoni,

wewe ukaaye Misri,

kwa kuwa Memfisi utaangamizwa

na kuwa magofu pasipo mkazi.

20 “Misri ni mtamba mzuri,

lakini kipanga anakuja dhidi yake kutoka kaskazini.

21 Askari wake waliokodiwa katika safu zake

wako kama ndama walionenepeshwa.

Wao pia watageuka na kukimbia pamoja,

hawataweza kuhimili vita,

kwa maana siku ya msiba inakuja juu yao,

wakati wao wa kuadhibiwa.

22 Misri atatoa sauti kama ya nyoka anayekimbia

kadiri adui anavyowasogelea na majeshi,

watakuja dhidi yake wakiwa na mashoka,

kama watu wakatao miti.

23 Wataufyeka msitu wake,”

asema Bwana,

“hata kama umesongamana kiasi gani.

Ni wengi kuliko nzige,

hawawezi kuhesabika.

24 Binti wa Misri ataaibishwa,

atatiwa mikononi mwa watu wa kaskazini.”

25 Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asema: “Nakaribia kuleta adhabu juu ya Amoni mungu wa Thebesi, na juu ya Farao, Misri na miungu yake, na wafalme wake, pamoja na wale wanaomtegemea Farao. 26 Nitawatia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wao, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na maafisa wake. Hatimaye, hata hivyo, Misri itakaliwa kama nyakati zilizopita,” asema Bwana.

27 “Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,

usifadhaike, ee Israeli.

Hakika nitakuokoa kutoka nchi za mbali,

uzao wako kutoka nchi ya uhamisho wao.

Yakobo atakuwa tena na amani na salama,

wala hakuna hata mmoja atakayewatia hofu.

28 Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,

kwa maana mimi niko pamoja nawe,”

asema Bwana.

“Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote

ambayo miongoni mwake nimekutawanya,

sitakuangamiza wewe kabisa.

Nitakurudi, lakini kwa haki tu,

wala sitakuacha kabisa bila kukuadhibu.”

Tabiri za Mwisho za Yeremia dhidi ya Waabudu Sanamu

Tabiri za mwisho za Yeremia dhidi ya Wayahudi waabudu sanamu, na dhidi ya Misri.

Yeremia 44

1 Neno hili lilimjia Yeremia kuhusu Wayahudi wote waishio Misri, huko Migdoli, Tahpanhesi na Memfisi, katika nchi ya Pathrosi kusema: 2 “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Mliona maangamizi makubwa niliyoyaleta juu ya Yerusalemu na juu ya miji yote ya Yuda. Leo imeachwa ukiwa na magofu 3 kwa sababu ya uovu waliokuwa wameufanya. Walinikasirisha kwa kufukiza uvumba na kwa kuabudu miungu mingine ambayo kamwe wao, wala ninyi, wala baba zenu hawakuifahamu. 4 Tena na tena, niliwatuma watumishi wangu manabii ambao walisema, ‘Msifanye jambo hili la kuchukiza ambalo nalichukia!’ 5 Lakini hawakusikiliza wala hawakujali, hawakugeuka ili kuuacha uovu wao, wala hawakuacha kufukiza uvumba kwa miungu mingine. 6 Kwa hiyo hasira yangu kali ilimwagika, ikawaka dhidi ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, na kuifanya ukiwa na magofu kama ilivyo leo.

7 “Basi hili ndilo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Kwa nini kujiletea maafa makubwa kama haya juu yenu kwa kujikatilia mbali kutoka Yuda wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, hata kujiacha bila mabaki? 8 Kwa nini kuichochea hasira yangu kwa kile ambacho mikono yenu imekitengeneza, mkaifukizia uvumba miungu mingine huko Misri, mahali mlipokuja kuishi? Mtajiangamiza wenyewe na kujifanya kitu cha kulaania na shutumu miongoni mwa mataifa yote duniani. 9 Je, mmesahau uovu uliotendwa na baba zenu, na wafalme na malkia wa Yuda, na uovu uliofanywa na ninyi na wake zenu katika nchi ya Yuda na barabara za Yerusalemu? 10 Mpaka leo hawajajinyenyekeza au kuonyesha heshima, wala hawajafuata sheria yangu na amri nilizoweka mbele yenu na baba zenu.

11 “Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Mimi nimekusudia kuleta maafa juu yenu, na kuiangamiza Yuda yote. 12 Nitawaondoa mabaki ya Yuda waliokusudia kwenda Misri kukaa humo. Wote wataangamia huko Misri, wataanguka kwa upanga au kufa kwa njaa. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana, watakufa kwa upanga au njaa. Watakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha laumu na shutumu. 13 Nitawaadhibu wale waishio Misri kwa upanga, njaa na tauni kama nilivyoiadhibu Yerusalemu. 14 Hakuna hata mmoja wa mabaki ya Yuda ambaye amekwenda kuishi Misri atakayeepuka au kunusurika ili kurudi katika nchi ya Yuda, ambayo wanaitamani sana kurudi na kuishi ndani yake, hakuna hata mmoja atakayerudi isipokuwa wakimbizi wachache.”

15 Kisha wanaume wote ambao walijua kwamba wake zao walikuwa wakifukiza uvumba kwa miungu mingine, pamoja na wanawake wote waliokuwako, yaani, kusanyiko kubwa na watu wote walioishi nchi ya Misri na Pathrosi, wakamwambia Yeremia, 16 “Hatutausikiliza ujumbe uliotuambia katika jina la Bwana! 17 Hakika tutafanya kila kitu tulichosema tutakifanya: Tutafukiza uvumba kwa Malkia wa Mbinguni na tutammiminia sadaka zetu za kinywaji kama vile sisi na baba zetu, wafalme wetu na maafisa wetu tulivyofanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Wakati ule tulikuwa na chakula tele, tulikuwa matajiri wala hatukupata dhara lolote. 18 Lakini tangu tulipoacha kumfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka za kinywaji, hatupati chochote, na tumekuwa tukiangamizwa kwa upanga na njaa.”

19 Wanawake wakaongeza kusema, “Wakati tulipomfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka zetu za kinywaji, je, waume zetu hawakujua kwamba tulikuwa tukitengeneza maandazi kwa mfano wake, na kummiminia yeye sadaka za kinywaji?”

20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake waliokuwa wakimjibu, 21 “Je, Bwana hakukumbuka na kufikiri juu ya uvumba uliofukizwa katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu na ninyi pamoja na baba zenu, wafalme wenu, maafisa wenu na watu wa nchi? 22 Bwana alipokuwa hawezi kuendelea kuvumilia matendo yenu maovu na mambo ya machukizo mliyoyafanya, nchi yenu ilikuwa kitu cha kulaania na kuachwa ukiwa pasipo wakazi, kama ilivyo leo. 23 Kwa sababu mmefukiza uvumba na kufanya dhambi dhidi ya Bwana, nanyi hamkumtii wala kufuata sheria yake au amri zake au maagizo yake, maafa haya yamekuja juu yenu, kama mnavyoona sasa.”

24 Kisha Yeremia akawaambia watu wote, pamoja na wanawake, “Sikieni neno la Bwana, enyi watu wote wa Yuda mlioko Misri. 25 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Ninyi na wake zenu mmeonyesha kwa matendo yenu kile mlichoahidi mliposema, ‘Hakika tutatimiza nadhiri tulizoziweka za kumfukizia uvumba na kummiminia sadaka za kinywaji Malkia wa Mbinguni.’

“Endeleeni basi, fanyeni yale mliyoahidi! Timizeni nadhiri zenu! 26 Lakini sikieni neno la Bwana, enyi Wayahudi wote mnaoishi Misri: ‘Ninaapa kwa Jina langu lililo kuu,’ asema Bwana, ‘kwamba hakuna hata mmoja atokaye Yuda anayeishi popote Misri ambaye kamwe ataomba tena kwa Jina langu au kuapa, akisema, “Hakika kama Bwana Mwenyezi aishivyo.” 27 Kwa maana ninawaangalia kwa ajili ya madhara, wala sio kwa mema. Wayahudi walioko Misri wataangamia kwa upanga na njaa, hadi wote watakapoangamizwa. 28 Wale watakaonusurika upanga na kurudi katika nchi ya Yuda kutoka Misri watakuwa wachache sana. Ndipo mabaki wote wa Yuda waliokuja kuishi Misri watakapojua ni neno la nani litakalosimama, kwamba ni langu au lao.

29 “ ‘Hii itakuwa ndiyo ishara kwenu kwamba nitawaadhibu mahali hapa, asema Bwana, ili mpate kujua kuwa onyo langu la madhara dhidi yenu hakika litatimizwa.’ 30 Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nitamtia Farao Hofra mfalme wa Misri mikononi mwa adui zake wanaoutafuta uhai wake, kama vile nilivyomtia Sedekia mfalme wa Yuda mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, adui aliyekuwa akiutafuta uhai wake.’ ”

Matukio ya Nebukadneza Kuwapeleka Wayahudi Uhamishoni Yanasimuliwa

Muhtasari mfupi wa matukio ya Wayahudi kupelekwa uhamishoni na Nebukadneza.

Yeremia 52:28–30

28 Hii ndiyo hesabu ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua kwenda uhamishoni:

katika mwaka wa saba,

Wayahudi 3,023;

29 katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza,

watu 832 kutoka Yerusalemu;

30 katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake,

Wayahudi 745 walichukuliwa kwenda uhamishoni na Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme.

Jumla ya watu wote walikuwa 4,600.