Yohanani Anawaokoa Mateka na Kukimbilia Misri

Yohanani anawaokoa mateka kutoka kwa Ishmaeli. Kinyume na amri za Mungu zilizotolewa kupitia Yeremia, anapata hifadhi huko Tahpanhesi nchini Misri.

587 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 41:11–43:7

11 Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye waliposikia juu ya uhalifu wote ambao Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa ameufanya, 12 waliwachukua watu wao wote kwenda kupigana na Ishmaeli mwana wa Nethania. Wakakutana naye karibu na bwawa kubwa huko Gibeoni. 13 Ikawa watu wote waliokuwa na Ishmaeli walipomwona Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wa jeshi waliokuwa pamoja naye, wakafurahi. 14 Watu wote ambao Ishmaeli alikuwa amewachukua mateka huko Mispa wakageuka na kumfuata Yohanani mwana wa Karea. 15 Lakini Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na watu wake wanane wakamtoroka Yohanani na kukimbilia kwa Waamoni.

16 Ndipo Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye wakawaongoza wote walionusurika kutoka Mispa, ambao walipona kutoka mikononi mwa Ishmaeli mwana wa Nethania baada yake kumuua Gedalia mwana wa Ahikamu: walikuwa askari, wanawake, watoto na matowashi aliowaleta kutoka Gibeoni. 17 Kisha wakaenda mbele na kutua Geruth-Kimhamu karibu na Bethlehemu wakiwa njiani kwenda Misri 18 ili kuwatoroka Wakaldayo. Waliwaogopa kwa sababu Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa amemuua Gedalia mwana wa Ahikamu, ambaye alikuwa amewekwa na mfalme wa Babeli kuwa mtawala wa nchi.

42:1 Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia 2 Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu. 3 Omba ili Bwana Mungu wako atuambie twende wapi na tufanye nini.”

4 Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba Bwana Mungu wenu kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho Bwana, wala sitawaficha chochote.”

5 Kisha wakamwambia Yeremia, “Bwana na awe shahidi wa kweli na mwaminifu kati yetu kama hatutafanya sawasawa na kila kitu Bwana Mungu wako atakachokutuma utuambie. 6 Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii Bwana Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii Bwana Mungu wetu.”

7 Baada ya siku kumi, neno la Bwana likamjia Yeremia. 8 Kwa hiyo akawaita pamoja Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana. 9 Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: 10 ‘Kama mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. 11 Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Bwana, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mikononi mwake. 12 Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma nanyi na kuwarudisha katika nchi yenu.’

13 “Hata hivyo, kama mkisema, ‘Hatutakaa katika nchi hii,’ hivyo mkaacha kumtii Bwana Mungu wenu, 14 nanyi kama mkisema, ‘Hapana, tutakwenda kuishi Misri, mahali ambapo hatutaona vita au kusikia sauti ya tarumbeta au kuwa na njaa ya chakula,’ 15 basi sikieni neno la Bwana, enyi mabaki ya Yuda. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Ikiwa mmekusudia kwenda Misri na kufanya makazi huko, 16 basi ule upanga mnaouogopa utawapata huko, na njaa mnayoihofia itawafuata huko Misri, nanyi mtafia huko. 17 Naam, wote waliokusudia kwenda kuishi Misri watakufa kwa upanga, njaa na tauni; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika au kuokoka maafa nitakayoyaleta juu yao.’ 18 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyomwagwa juu ya wale walioishi Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu mtakapokwenda Misri. Mtakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha kulaumia na cha kushutumia, nanyi kamwe hamtaona mahali hapa tena.’

19 “Enyi mabaki ya Yuda, Bwana amewaambia, ‘Msiende Misri.’ Hakikisheni jambo hili: Ninawaonya leo 20 kwamba mmefanya kosa kubwa mioyoni mwenu mliponituma kwa Bwana Mungu wenu na kusema, ‘Mwombe Bwana Mungu wetu kwa ajili yetu, nawe utuambie kila kitu atakachosema, nasi tutafanya.’ 21 Nimewaambieni leo, lakini bado ninyi hamtaki kumtii Bwana Mungu wenu katika yote aliyonituma niwaambie. 22 Basi sasa, hakikisheni jambo hili: Mtakufa kwa upanga, njaa na tauni mahali ambapo mnataka kwenda kuishi.”

43:1 Yeremia alipomaliza kuwaambia watu maneno yote ya Bwana Mungu wao, yaani kila kitu Bwana alichokuwa amemtuma kuwaambia, 2 Azaria mwana wa Hoshaya, na Yohanani mwana wa Karea, na watu wote wenye kiburi wakamwambia Yeremia, “Wewe unasema uongo! Bwana Mungu wetu hajakutuma kusema, ‘Kamwe msiende Misri kukaa huko.’ 3 Lakini Baruku mwana wa Neria anakuchochea dhidi yetu ili ututie mikononi mwa Wakaldayo, ili watuue au watuchukue uhamishoni Babeli.”

4 Basi Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi, na watu wote wakakataa kutii amri ya Bwana ya kukaa katika nchi ya Yuda. 5 Badala yake, Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi wakawaongoza mabaki yote ya Yuda waliokuwa wamerudi kuishi katika nchi ya Yuda kutoka mataifa yote ambayo walikuwa wametawanywa. 6 Pia wakawaongoza wanaume wote, wanawake na watoto, na binti za mfalme ambao Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme alikuwa amewaacha na Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, na nabii Yeremia, na Baruku mwana wa Neria. 7 Kwa hiyo wakaingia Misri kwa kutokumtii Bwana, wakaenda mpaka Tahpanhesi.