Sehemu ya 3: Wayahudi Wasiopelekwa Babeli

Historia ya sehemu ya taifa la Wayahudi ambayo haikupelekwa uhamishoni Babeli, baada ya kuangamizwa kwa hekalu.

Maelezo Mafupi ya Sehemu Hii

Maelezo mafupi ya matukio yanayosimuliwa katika sehemu hii.

588 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 25:23–26

23 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia kuwa mtawala, wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 24 Gedalia akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema, “Msiwaogope maafisa wa Kikaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.”

25 Hata hivyo, katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi, nao wakamuua Gedalia, na pia watu wa Yuda, pamoja na Wakaldayo waliokuwa naye huko Mispa. 26 Baada ya haya, watu wote kuanzia aliye mdogo sana hadi aliye mkubwa kabisa, pamoja na maafisa wa jeshi, wakakimbilia Misri kwa kuwaogopa Wakaldayo.

Gedalia Anawekwa Kuwa Gavana wa Uyahudi

Baada ya kuharibiwa kwa hekalu, Nebukadneza anamteua Gedalia kuwa gavana wa Uyahudi. Yeremia na watu wengine wote wanajiunga na Gedalia.

2 Wafalme 25:22

22 Nebukadneza mfalme wa Babeli akamteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, awe msimamizi wa watu aliowaacha Yuda.

Yeremia 40:1–12

1 Neno likamjia Yeremia kutoka kwa Bwana baada ya Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli. 2 Kiongozi wa walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “Bwana Mungu wako aliamuru maafa haya kwa mahali hapa. 3 Sasa Bwana ameyaleta haya, amefanya sawasawa na vile alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya Bwana na hamkumtii. 4 Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Twende pamoja mpaka Babeli ikiwa unataka, nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.” 5 Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.”

Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake. 6 Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.

7 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli, 8 wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 9 Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu. 10 Mimi mwenyewe nitakaa Mispa ili kuwawakilisha mbele ya Wakaldayo wanaotujia, lakini ninyi mtavuna divai, matunda ya kiangazi na mafuta, nanyi mtaweka katika vyombo vyenu vya kuhifadhia, na kuishi katika miji mliyojitwalia.”

11 Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, Edomu na nchi nyingine zote waliposikia kwamba mfalme wa Babeli ameacha mabaki ya watu katika Yuda na amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kuwa mtawala wao, 12 wakarudi wote katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mispa, kutoka nchi zote ambazo walikuwa wametawanywa. Nao wakavuna divai na matunda tele wakati wa kiangazi.

Ishmaeli Anapanga Njama Dhidi ya Gedalia

Yeremia 40:13–41:10

13 Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi wakamjia Gedalia huko Mispa 14 na kumwambia, “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini.

15 Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia Gedalia kwa siri huko Mispa, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, wala hakuna atakayejua. Kwa nini akuue na kusababisha Wayahudi wote waliokuzunguka watawanyike, na mabaki wa Yuda waangamie?”

16 Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo kama hilo! Unalosema kuhusu Ishmaeli si kweli.”

41:1 Katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme na pia alikuwa mmoja wa maafisa wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa. Walipokuwa wakila pamoja huko, 2 Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na wale watu kumi waliokuwa pamoja naye waliinuka na kumuua Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kwa upanga, wakamuua yule ambaye mfalme wa Babeli alikuwa amemteua awe mtawala wa nchi. 3 Ishmaeli akawaua pia Wayahudi wote waliokuwa na Gedalia huko Mispa, pamoja na askari wa Kikaldayo waliokuwa huko.

4 Siku moja baada ya kuuawa kwa siri kwa Gedalia, kabla mtu yeyote hajafahamu jambo hilo, 5 watu themanini waliokuwa wamenyoa ndevu zao, waliorarua nguo zao na kujikatakata walikuja kutoka Shekemu, Shilo na Samaria wakileta sadaka za nafaka na uvumba katika nyumba ya Bwana. 6 Ishmaeli mwana wa Nethania akaondoka Mispa ili kwenda kuwalaki, huku akilia alipokuwa akienda. Alipokutana nao, akasema, “Karibuni kwa Gedalia mwana wa Ahikamu.” 7 Walipoingia mjini, Ishmaeli mwana wa Nethania na wale watu waliokuwa pamoja naye wakawachinja na kuwatupa ndani ya kisima. 8 Lakini watu kumi miongoni mwao wakamwambia Ishmaeli, “Sisi usituue! Tuna ngano na shayiri, mafuta na asali, vilivyofichwa katika shamba.” Kwa hiyo akawaacha na hakuwaua pamoja na wale wengine. 9 Basi kile kisima ambacho alitupa zile maiti za watu aliowaua pamoja na Gedalia kilikuwa ni kile kisima ambacho Mfalme Asa alikifanya sehemu ya ulinzi wake dhidi ya Baasha mfalme wa Israeli. Ishmaeli mwana wa Nethania akakijaza kisima hicho kwa maiti.

10 Ishmaeli akawafanya mateka watu wote ambao Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme alikuwa amewaacha huko Mispa na kumweka Gedalia mwana wa Ahikamu juu yao: walikuwa binti za mfalme pamoja na watu wote aliokuwa amewaacha huko. Ishmaeli mwana wa Nethania akawachukua mateka na kuondoka nao, akavuka kwenda kwa Waamoni.