Ezekieli Anatabiri Dhidi ya Farao na Misri

Unabii dhidi ya Misri.

589 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 29:1–16

1 Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote. 3 Nena, nawe useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri,

joka kubwa ulalaye katikati ya vijito vyako.

Unasema, “Mto Naili ni wangu mwenyewe;

niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.”

4 Lakini nitatia ndoana katika mataya yako

nami nitawafanya samaki wa vijito vyako

washikamane na magamba yako.

Nitakutoa katikati ya vijito vyako,

pamoja na samaki wote

walioshikamana na magamba yako.

5 Nitakutupa jangwani,

wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako.

Utaanguka uwanjani,

nawe hutakusanywa au kuchukuliwa.

Nitakutoa uwe chakula

kwa wanyama wa nchi

na ndege wa angani.

6 Ndipo wale wote waishio Misri watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.

“ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli. 7 Walipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao; walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka.

8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao. 9 Misri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.

“ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Naili ni wangu; mimi niliufanya,” 10 kwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa isiyolimwa wala kukaliwa na watu kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpakani wa Ethiopia. 11 Hakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna yeyote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini. 12 Nitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi nyingine.

13 “ ‘Lakini hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka mataifa walikotawanywa. 14 Nitawarudisha hao Wamisri kutoka kwenye kutekwa kwao na kuwaweka katika Pathrosi, nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu. 15 Utakuwa ufalme dhaifu kuliko zote na kamwe Misri haitajikweza tena juu ya mataifa mengine. Nitaufanya ufalme wake dhaifu sana kiasi kwamba kamwe hautatawala tena juu ya mataifa mengine. 16 Misri haitakuwa tena tumaini la watu wa Israeli bali itakuwa kumbukumbu ya dhambi yao kwa kuigeukia kuomba msaada. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.’ ”

Ezekieli: Misri Itaanguka Kama Ashuru 588 KK

Unabii dhidi ya Misri.

Ezekieli 30:20–31:18

20 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa kwanza, siku ya saba, neno la Bwana likanijia kusema: 21 “Mwanadamu, nimevunja mkono wa Farao mfalme wa Misri. Haukufungwa ili upone au kuwekewa kipande cha ubao ili upate nguvu za kuweza kuchukua upanga. 22 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na Farao mfalme wa Misri. Nitavunja mikono yake yote miwili, ule mkono ulio mzima pia na ule uliovunjika na kuufanya upanga uanguke toka mkononi mwake. 23 Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi zote. 24 Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli na kuutia upanga wangu mkononi mwake, lakini nitavunja mikono ya Farao, naye atalia kwa huzuni mbele yake kama mtu aliyetiwa jeraha la kumfisha. 25 Nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, lakini mikono ya Farao italegea. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, nitakapoutia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye ataunyoosha dhidi ya Misri. 26 Nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi mbalimbali. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.”

31:1 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la Bwana likanijia, kusema: 2 “Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake ya wajeuri:

“ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa

na wewe katika fahari.

3 Angalia Ashuru, wakati fulani ilikuwa mwerezi huko Lebanoni,

ukiwa na matawi mazuri ukitia msitu kivuli;

ulikuwa mrefu sana,

kilele chake kilipita majani ya miti yote.

4 Maji mengi yaliustawisha,

chemchemi zenye maji mengi ziliufanya urefuke;

vijito vyake vilitiririka pale

ulipoota pande zote

na kupeleka mifereji yake

kwenye miti yote ya shambani.

5 Hivyo ukarefuka

kupita miti yote ya shambani;

vitawi vyake viliongezeka

na matawi yake yakawa marefu,

yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji.

6 Ndege wote wa angani

wakaweka viota kwenye vitawi vyake,

wanyama wote wa shambani

wakazaana chini ya matawi yake,

mataifa makubwa yote

yaliishi chini ya kivuli chake.

7 Ulikuwa na fahari katika uzuri,

ukiwa na matawi yaliyotanda,

kwa kuwa mizizi yake ilikwenda chini

mpaka kwenye maji mengi.

8 Mierezi katika bustani ya Mungu

haikuweza kushindana nao,

wala misunobari haikuweza

kulingana na vitawi vyake,

wala miaramoni

haikulinganishwa na matawi yake,

wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu

wa kulinganisha na uzuri wake.

9 Niliufanya kuwa mzuri

ukiwa na matawi mengi,

ulionewa wivu na miti yote ya Edeni

katika bustani ya Mungu.

10 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake, 11 niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye aushughulikie sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali, 12 nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kwenye kivuli chake na kuuacha. 13 Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake. 14 Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale waendao shimoni.

15 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika siku ile mwerezi uliposhushwa chini kaburini nilizifunika chemchemi zenye maji mengi kwa maombolezo: Nilivizuia vijito vyake na wingi wa maji yake nikauzuia. Kwa sababu yake niliivika Lebanoni huzuni, nayo miti yote ya shambani ikanyauka. 16 Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa kishindo cha kuanguka kwake wakati nilipoushusha chini kaburini pamoja na wale washukao shimoni. Ndipo miti yote ya Edeni, miti iliyo bora kuliko yote na iliyo mizuri sana ya Lebanoni, miti yote ile iliyokunywa maji vizuri, ilifarijika hapa duniani. 17 Wale walioishi katika kivuli chake, wale walioungana naye miongoni mwa mataifa, nao pia walikuwa wamezikwa pamoja naye, wakiungana na wale waliouawa kwa upanga.

18 “ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa chini pamoja na miti ya Edeni mpaka kuzimu, utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.

“ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote ya wajeuri, asema Bwana Mwenyezi.’ ”