Kuja kwa Kristo Kwatabiriwa

Unabii kuhusu kuja kwa Kristo, na kurejeshwa kwa Wayahudi.

710 hadi 699 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 42–43

1 “Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,

mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye;

nitaweka Roho yangu juu yake,

naye ataleta haki kwa mataifa.

2 Hatapaza sauti wala kupiga kelele,

wala hataiinua sauti yake barabarani.

3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

na utambi unaofuka moshi hatauzima.

Kwa uaminifu ataleta haki,

4 hatazimia roho wala kukata tamaa,

mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.

Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”

5 Hili ndilo asemalo Mungu, Bwana,

yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,

aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo,

awapaye watu wake pumzi,

na uzima kwa wale waendao humo:

6 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki;

nitakushika mkono wako.

Nitakulinda na kukufanya

kuwa Agano kwa ajili ya watu

na nuru kwa Mataifa,

7 kuwafungua macho wale wasioona,

kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,

na kuwafungua kutoka gerezani

wale wanaokaa gizani.

8 “Mimi ndimi Bwana; hilo ndilo Jina langu!

Sitampa mwingine utukufu wangu

wala sanamu sifa zangu.

9 Tazama, mambo ya kwanza yametokea,

nami natangaza mambo mapya;

kabla hayajatokea

nawatangazia habari zake.”

10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya,

sifa zake toka miisho ya dunia,

ninyi mshukao chini baharini,

na vyote vilivyomo ndani yake,

enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.

11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;

makao anamoishi Kedari na yashangilie.

Watu wa Sela waimbe kwa furaha,

na wapige kelele kutoka vilele vya milima.

12 Wampe Bwana utukufu,

na kutangaza sifa zake katika visiwa.

13 Bwana ataenda kama mtu mwenye nguvu,

kama shujaa atachochea shauku yake,

kwa kelele ataamsha kilio cha vita,

naye atashinda adui zake.

14 “Kwa muda mrefu nimenyamaza kimya,

nimekaa kimya na kujizuia.

Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua,

ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.

15 Nitaharibu milima na vilima

na kukausha mimea yako yote;

nitafanya mito kuwa visiwa

na kukausha mabwawa.

16 Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua,

kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza;

nitafanya giza kuwa nuru mbele yao,

na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini.

Haya ndiyo mambo nitakayofanya;

mimi sitawaacha.

17 Lakini wale wanaotumaini sanamu,

wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’

watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.

18 “Sikieni, enyi viziwi;

tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!

19 Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu,

na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?

Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu,

aliye kipofu kama mtumishi wa Bwana?

20 Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia;

masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.”

21 Ilimpendeza Bwana

kwa ajili ya haki yake

kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.

22 Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara,

wote wamenaswa katika mashimo,

au wamefichwa katika magereza.

Wamekuwa nyara,

wala hapana yeyote awaokoaye.

Wamefanywa mateka,

wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”

23 Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili,

au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?

24 Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka,

na Israeli kwa wateka nyara?

Je, hakuwa yeye, Bwana,

ambaye tumetenda dhambi dhidi yake?

Kwa kuwa hawakufuata njia zake,

hawakutii sheria zake.

25 Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka,

ukali wa vita.

Iliwazunguka kwa miali ya moto, lakini hata hivyo hawakuelewa;

iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni.

43:1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

“Usiogope kwa maana nimekukomboa,

nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

2 Unapopita kwenye maji makuu,

nitakuwa pamoja nawe,

unapopita katika mito ya maji,

hayatakugharikisha.

Utakapopita katika moto,

hutaungua,

miali ya moto haitakuunguza.

3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

Kushi na Seba badala yako.

4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,

nami kwa kuwa ninakupenda,

nitatoa watu badala yako

na mataifa badala ya maisha yako.

5 Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,

nitawaleta watoto wako kutoka mashariki,

na kukukusanya kutoka magharibi.

6 Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’

nayo kusini, ‘Usiwazuie.’

Walete wana wangu kutoka mbali,

na binti zangu kutoka miisho ya dunia:

7 kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu,

niliyemuumba kwa utukufu wangu,

niliyemhuluku na kumfanya.”

8 Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni,

wenye masikio lakini hawasikii.

9 Mataifa yote yanakutanika pamoja,

na makabila yanakusanyika.

Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya,

na kututangazia mambo yaliyopita?

Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi,

ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.”

10 “Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Bwana,

“na mtumishi wangu niliyemchagua,

ili mpate kunijua na kuniamini,

na kutambua kwamba Mimi ndiye.

Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa,

wala hatakuwepo mwingine baada yangu.

11 Mimi, naam mimi, ndimi Bwana,

zaidi yangu hakuna mwokozi.

12 Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza:

Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu.

Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Bwana,

“kwamba Mimi ndimi Mungu.

13 Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye.

Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa

kutoka mkononi wangu.

Mimi ninapotenda,

ni nani awezaye kutangua?”

14 Hili ndilo Bwana asemalo,

Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:

“Kwa ajili yenu nitatumana Babeli

na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi,

katika meli walizozionea fahari.

15 Mimi ndimi Bwana, yeye Aliye Mtakatifu wako,

Muumba wa Israeli, Mfalme wako.”

16 Hili ndilo asemalo Bwana,

yeye aliyefanya njia baharini,

mahali pa kupita kwenye maji mengi,

17 aliyeyakokota magari ya vita na farasi,

jeshi pamoja na askari wa msaada,

nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe,

wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi:

18 “Msiyakumbuke mambo yaliyopita,

wala msiyatafakari mambo ya zamani.

19 Tazama, nitafanya jambo jipya!

Sasa litachipuka, je, hamtalitambua?

Nitafanya njia jangwani

na vijito vya maji katika nchi kame.

20 Wanyama wa mwituni wataniheshimu,

mbweha na bundi,

kwa sababu ninawapatia maji jangwani,

na vijito katika nchi kame,

ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua,

21 watu wale niliowaumba kwa ajili yangu,

ili wapate kutangaza sifa zangu.

22 “Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo,

hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli.

23 Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa,

wala kuniheshimu kwa dhabihu zako.

Sikukulemea kwa sadaka za nafaka

wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba.

24 Hukuninunulia uvumba wowote wenye manukato,

wala hukunipa kwa ukarimu

mafuta ya wanyama wa dhabihu zako.

Lakini umenilemea kwa dhambi zako,

na kunitaabisha kwa makosa yako.

25 “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako,

kwa ajili yangu mwenyewe,

wala sizikumbuki dhambi zako tena.

26 Tafakari mambo yaliyopita,

njoo na tuhojiane,

leta shauri lako uweze kupewa haki yako.

27 Baba yako wa kwanza alitenda dhambi,

wasemaji wako wameasi dhidi yangu.

28 Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako,

nami nitamtoa Yakobo aangamizwe,

na Israeli adhihakiwe.