Watu wa Mungu Waahidiwa Faraja

Ahadi ya faraja kwa watu wa Mungu. Kurejeshwa kwa Wayahudi hatimaye kunatabiriwa.

710 hadi 699 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 40–41

1 Wafarijini, wafarijini watu wangu,

asema Mungu wenu.

2 Sema na Yerusalemu kwa upole,

umtangazie

kwamba kazi yake ngumu imekamilika,

kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia,

kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Bwana

maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.

3 Sauti ya mtu aliaye:

“Itengenezeni jangwani njia ya Bwana,

nyoosheni njia kuu nyikani

kwa ajili ya Mungu wetu.

4 Kila bonde litainuliwa,

kila mlima na kilima kitashushwa;

penye mabonde patanyooshwa,

napo palipoparuza patasawazishwa.

5 Utukufu wa Bwana utafunuliwa,

nao wanadamu wote watauona pamoja.

Kwa maana kinywa cha Bwana kimenena.”

6 Sauti husema, “Piga kelele.”

Nami nikasema, “Nipige kelele gani?”

“Wanadamu wote ni kama majani,

nao utukufu wao wote

ni kama maua ya kondeni.

7 Majani hunyauka na maua huanguka,

kwa sababu pumzi ya Bwana huyapuliza.

Hakika wanadamu ni majani.

8 Majani hunyauka na maua huanguka,

lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”

9 Wewe uletaye habari njema Sayuni,

panda juu ya mlima mrefu.

Wewe uletaye habari njema Yerusalemu,

inua sauti yako kwa kupiga kelele,

inua sauti, usiogope;

iambie miji ya Yuda,

“Yuko hapa Mungu wenu!”

10 Tazameni, Bwana Mwenyezi anakuja na nguvu,

nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake.

Tazameni, ujira wake u pamoja naye,

nayo malipo yake yanafuatana naye.

11 Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo:

Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake

na kuwachukua karibu na moyo wake,

huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao.

12 Ni nani aliyepima maji ya bahari

kwenye konzi ya mkono wake,

au kuzipima mbingu kwa shibiri yake?

Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu,

au kupima milima kwenye kipimio

na vilima kwenye mizani?

13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana,

au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?

14 Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha,

naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa?

Ni nani aliyemfundisha maarifa

au kumwonyesha mapito ya ufahamu?

15 Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo,

ni kama vumbi jembamba juu ya mizani,

huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.

16 Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni,

wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa.

17 Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu,

yanaonekana yasio na thamani

na zaidi ya bure kabisa.

18 Basi, utamlinganisha Mungu na nani?

Utamlinganisha na kitu gani?

19 Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu,

naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu

na kuitengenezea mikufu ya fedha.

20 Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii

huuchagua mti usiooza.

Humtafuta fundi stadi

wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika.

21 Je, hujui?

Je, hujasikia?

Je, hujaambiwa tangu mwanzo?

Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia?

22 Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia,

nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi.

Huzitandaza mbingu kama chandarua,

na kuzitandaza kama hema la kuishi.

23 Huwafanya wakuu kuwa si kitu,

na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure.

24 Mara baada ya kupandwa,

mara baada ya kutiwa ardhini,

mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini,

ndipo huwapulizia nao wakanyauka,

nao upepo wa kisulisuli

huwapeperusha kama makapi.

25 “Utanilinganisha mimi na nani?

Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.

26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni:

Ni nani aliyeumba hivi vyote?

Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine

na kuziita kila moja kwa jina lake.

Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,

hakuna hata mojawapo inayokosekana.

27 Kwa nini unasema, ee Yakobo,

nanyi ee Israeli, kulalamika,

“Njia yangu imefichwa Bwana asiione,

Mungu wangu hajali shauri langu?”

28 Je wewe, hufahamu?

Je wewe, hujasikia?

Bwana ni Mungu wa milele,

Muumba wa miisho ya dunia.

Hatachoka wala kulegea,

wala hakuna hata mmoja

awezaye kuupima ufahamu wake.

29 Huwapa nguvu waliolegea

na huongeza nguvu za wadhaifu.

30 Hata vijana huchoka na kulegea,

nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

31 bali wale wamtumainio Bwana

atafanya upya nguvu zao.

Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

watapiga mbio wala hawatachoka,

watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

41:1 “Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa!

Mataifa na wafanye upya nguvu zao!

Wao na wajitokeze, kisha waseme,

tukutane pamoja mahali pa hukumu.

2 “Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki,

akimwita katika haki kwa utumishi wake?

Huyatia mataifa mikononi mwake,

na kuwatiisha wafalme mbele zake.

Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake,

huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake.

3 Huwafuatia na kuendelea salama,

katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita.

4 Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza,

akiita vizazi tangu mwanzo?

Mimi, Bwana, ni wa kwanza

nami nitakuwa pamoja na wa mwisho:

mimi Bwana ndiye.”

5 Visiwa vimeliona na kuogopa,

miisho ya dunia inatetemeka.

Wanakaribia na kuja mbele,

6 kila mmoja humsaidia mwingine

na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!”

7 Fundi humtia moyo sonara,

yeye alainishaye kwa nyundo

humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe,

Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.”

Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike.

8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu,

Yakobo, niliyemchagua,

ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu,

9 nilikuchukua toka miisho ya dunia,

nilikuita kutoka pembe zake za mbali.

Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’;

nimekuchagua, wala sikukukataa.

10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

Nitakutia nguvu na kukusaidia;

nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

11 “Wote walioona hasira dhidi yako

hakika wataaibika na kutahayarika,

wale wakupingao

watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

12 Ingawa utawatafuta adui zako,

hutawaona.

Wale wanaopigana vita dhidi yako

watakuwa kama vile si kitu kabisa.

13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

nikushikaye mkono wako wa kuume

na kukuambia, Usiwe na hofu,

nitakusaidia.

14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu,

ee Israeli uliye mdogo,

kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Bwana,

Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

15 “Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria,

kipya na chenye makali, chenye meno mengi.

Utaipura milima na kuiponda

na kuvifanya vilima kuwa kama makapi.

16 Utaipepeta, nao upepo utaichukua,

dhoruba itaipeperushia mbali.

Bali wewe utajifurahisha katika Bwana

na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

17 “Maskini na wahitaji wanatafuta maji,

lakini hayapo,

ndimi zao zimekauka kwa kiu.

Lakini Mimi Bwana nitawajibu,

Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

18 Nitaifanya mito itiririke juu ya vilima vilivyo kame,

nazo chemchemi ndani ya mabonde.

Nitaligeuza jangwa liwe mabwawa ya maji,

nayo ardhi iliyokauka kuwa chemchemi za maji.

19 Katika jangwa nitaotesha

mwerezi, mshita, mhadasi na mzeituni.

Nitaweka misunobari, mivinje na misanduku

pamoja huko nyikani,

20 ili kwamba watu wapate kuona na kujua,

wapate kufikiri na kuelewa,

kwamba mkono wa Bwana umetenda hili,

kwamba yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ndiye alilifanya.”

21 Bwana asema, “Leta shauri lako.

Toa hoja yako,” asema Mfalme wa Yakobo.

22 “Leteni sanamu zenu zituambie

ni nini kitakachotokea.

Tuambieni mambo ya zamani yalikuwa nini,

ili tupate kuyatafakari

na kujua matokeo yake ya mwisho.

Au tutangazieni mambo yatakayokuja,

23 tuambieni ni nini kitakachotokea baadaye,

ili tupate kujua kuwa ninyi ni miungu.

Fanyeni jambo lolote zuri au baya,

ili tupate kutishika na kujazwa na hofu.

24 Lakini ninyi ni zaidi ya bure kabisa,

na kazi zenu hazifai kitu kabisa;

yeye awachaguaye ni chukizo sana.

25 “Nimemchochea mtu mmoja kutoka kaskazini,

naye yuaja, mmoja toka mawio ya jua aliitaye Jina langu.

Huwakanyaga watawala kana kwamba ni matope,

kama mfinyanzi akanyagavyo udongo wa kufinyangia.

26 Ni nani aliyenena hili tokea mwanzoni, ili tupate kujua,

au kabla, ili tuweze kusema, ‘Alikuwa sawa’?

Hakuna aliyenena hili,

hakuna aliyetangulia kusema hili,

hakuna yeyote aliyesikia maneno kutoka kwenu.

27 Nilikuwa wa kwanza kumwambia Sayuni,

‘Tazama, wako hapa!’

Nilimpa Yerusalemu mjumbe wa habari njema.

28 Ninatazama, lakini hakuna yeyote:

hakuna yeyote miongoni mwao awezaye kutoa shauri,

hakuna yeyote wa kutoa jibu wakati ninapowauliza.

29 Tazama, wote ni ubatili!

Matendo yao ni bure;

vinyago vyao ni upepo mtupu na machafuko.