Jeshi la Senakeribu Laangamizwa

710 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 19:8–19

8 Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.

9 Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Basi akatuma tena wajumbe kwa Hezekia na neno hili: 10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 11 Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa? 12 Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa, hiyo miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari? 13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”

14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana. 15 Naye Hezekia akamwomba Bwana akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. 16 Tega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.

17 “Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao. 18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 19 Sasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”

Zaburi 73

Zaburi ya Asafu.

1 Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,

kwa wale ambao mioyo yao ni safi.

2 Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza;

nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama.

3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna

nilipoona kufanikiwa kwa waovu.

4 Wao hawana taabu,

miili yao ina afya na nguvu.

5 Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine,

wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.

6 Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao,

wamejivika jeuri.

7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi,

majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.

8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi,

katika majivuno yao wanatishia kutesa.

9 Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu,

nazo ndimi zao humiliki duniani.

10 Kwa hiyo watu wao huwageukia

na kunywa maji tele.

11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua?

Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”

12 Hivi ndivyo walivyo waovu:

siku zote hawajali,

wanaongezeka katika utajiri.

13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure,

ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.

14 Mchana kutwa nimetaabika,

nimeadhibiwa kila asubuhi.

15 Kama ningesema, “Nitasema hivi,”

ningelikuwa nimewasaliti watoto wako.

16 Nilipojaribu kuelewa haya yote,

yalikuwa magumu kwangu kuelewa.

17 Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu,

ndipo nilipotambua mwisho wao.

18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi,

unawaangusha chini kwa uharibifu.

19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula,

wanatoweshwa kabisa na vitisho!

20 Kama ndoto mtu aamkapo,

hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana,

utawatowesha kama ndoto.

21 Wakati moyo wangu ulipohuzunishwa,

na roho yangu ilipotiwa uchungu,

22 nilikuwa mpumbavu na mjinga,

nilikuwa mnyama mkatili mbele yako.

23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote,

umenishika mkono wangu wa kuume.

24 Unaniongoza kwa shauri lako,

hatimaye utaniingiza katika utukufu.

25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe?

Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.

26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,

bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu

na fungu langu milele.

27 Wale walio mbali nawe wataangamia,

unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.

28 Lakini kwangu mimi,

ni vyema kuwa karibu na Mungu.

Nimemfanya Bwana Mwenyezi kimbilio langu;

nami nitayasimulia matendo yako yote.

2 Wafalme 19:20–35

20 Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru. 21 Hili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake:

“ ‘Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki.

Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.

22 Ni nani uliyemtukana na kumkufuru?

Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake,

na kumwinulia macho yako kwa kiburi?

Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!

23 Kupitia kwa wajumbe wako

umelundika matukano juu ya Bwana.

Nawe umesema,

“Kwa magari yangu mengi ya vita,

nimepanda juu ya vilele vya milima,

vilele vya juu sana katika Lebanoni.

Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu,

misunobari yake iliyo bora sana.

Nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana,

misitu yake iliyo mizuri sana.

24 Nimechimba visima katika nchi za kigeni

na kunywa maji yake.

Kwa nyayo za miguu yangu

nimekausha vijito vyote vya Misri.”

25 “ ‘Je, hujasikia?

Zamani sana niliamuru hili.

Siku za kale nilipanga hili;

sasa nimelifanya litokee,

kwamba umegeuza miji yenye ngome

kuwa malundo ya mawe.

26 Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu,

wanavunjika mioyo na kuaibishwa.

Wao ni kama mimea katika shamba,

kama machipukizi mororo ya kijani,

kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba,

ambayo hukauka kabla ya kukua.

27 “ ‘Lakini ninajua mahali ukaapo,

kutoka kwako na kuingia kwako,

na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.

28 Kwa sababu unaghadhibika dhidi yangu,

na ufidhuli wako umefika masikioni mwangu,

nitaweka ndoana yangu puani mwako

na hatamu yangu kinywani mwako,

nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.’

29 “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia:

“Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe,

na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake.

Lakini katika mwaka wa tatu, panda na uvune,

panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.

30 Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda

wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.

31 Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki,

na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika.

Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote ndio utatimiza jambo hili.

32 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru:

“Hataingia katika mji huu

wala hatapiga mshale hapa.

Hatakuja mbele yake akiwa na ngao,

wala kupanga majeshi kuuzingira.

33 Kwa njia ile aliyoijia, ndiyo atakayorudi;

hataingia katika mji huu,

asema Bwana.

34 Nitaulinda mji huu na kuuokoa,

kwa ajili yangu mwenyewe,

na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”

35 Usiku ule, malaika wa Bwana akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!

Zaburi 75–76

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Zaburi ya Asafu. Wimbo.

1 Ee Mungu, tunakushukuru,

tunakushukuru wewe,

kwa kuwa jina lako li karibu;

watu husimulia matendo yako ya ajabu.

2 Unasema, “Ninachagua wakati maalum;

ni mimi nihukumuye kwa haki.

3 Wakati dunia na watu wake wote inapotetemeka,

ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara.

4 Kwa wale wenye majivuno ninasema,

‘Msijisifu tena,’

kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu.

5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu;

msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’ ”

6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi

au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu.

7 Bali Mungu ndiye ahukumuye:

Humshusha huyu na kumkweza mwingine.

8 Mkononi mwa Bwana kuna kikombe

kilichojaa mvinyo unaotoka povu

uliochanganywa na vikolezo;

huumimina, nao waovu wote wa dunia

hunywa mpaka tone la mwisho.

9 Bali mimi, nitatangaza hili milele;

nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo.

10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote,

bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.

Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Asafu. Wimbo.

76:1 Katika Yuda, Mungu anajulikana,

jina lake ni kuu katika Israeli.

2 Hema lake liko Salemu,

makao yake katika Sayuni.

3 Huko alivunja mishale imetametayo,

ngao na panga, silaha za vita.

4 Wewe unangʼaa kwa mwanga,

mwenye fahari zaidi ya milima yenye utajiri wa wanyama pori.

5 Mashujaa hulala wametekwa nyara,

hulala usingizi wao wa mwisho;

hakuna hata mmoja wa watu wa vita

anayeweza kuinua mikono yake.

6 Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo,

farasi na gari la vita vilikaa kimya.

7 Wewe peke yako ndiye wa kuogopwa.

Ni nani awezaye kusimama mbele yako unapokasirika?

8 Kutoka mbinguni ulitamka hukumu,

nayo nchi ikaogopa, ikawa kimya:

9 wakati wewe, Ee Mungu, ulipoinuka kuhukumu,

kuwaokoa wote walioonewa katika nchi.

10 Hakika ghadhabu yako dhidi ya wanadamu inakuletea sifa,

na masalia ya ghadhabu yako unajifunga mshipi.

11 Wekeni nadhiri kwa Bwana Mungu wenu na kuzitimiza;

nchi zote za jirani na walete zawadi

kwa Yule astahiliye kuogopwa.

12 Huvunja roho za watawala;

anaogopwa na wafalme wa dunia.

2 Wafalme 19:36–37

36 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.

37 Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.