Uvamizi wa Pili wa Senakeribu kwa Kirefu

710 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 18:17–19:7

17 Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi, pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja Yerusalemu na kusimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. 18 Wakaagiza mfalme aitwe. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakawaendea.

19 Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia:

“ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako? 20 Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi? 21 Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. 22 Nawe kama ukiniambia, “Tunamtumainia Bwana Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya katika Yerusalemu”?

23 “ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao! 24 Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? 25 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa Bwana? Bwana mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”

26 Ndipo Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walioko juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”

27 Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mikojo yao wenyewe?”

28 Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 29 Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa mkononi mwangu. 30 Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Bwana kwa kuwaambia, ‘Hakika Bwana atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’

31 “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe, 32 mpaka nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu, nchi ya mizeituni na asali. Chagueni uzima, sio mauti!

“Msimsikilize Hezekia, kwa kuwa anawapotosha asemapo, ‘Bwana atatuokoa.’ 33 Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? 34 Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? 35 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Bwana aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”

36 Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”

37 Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia yale jemadari wa jeshi aliyoyasema.

19:1 Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu la Bwana. 2 Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa nguo za magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi. 3 Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa. 4 Yamkini Bwana, Mungu wako atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Bwana, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”

5 Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya, 6 Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo. 7 Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ”

Zaburi 44

Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.

1 Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu,

baba zetu wametueleza

yale uliyotenda katika siku zao,

siku za kale.

2 Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa

na ukawapanda baba zetu,

uliangamiza mataifa

na kuwastawisha baba zetu.

3 Sio kwa upanga wao waliipata nchi,

wala si mkono wao uliwapatia ushindi;

ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume,

na nuru ya uso wako,

kwa kuwa uliwapenda.

4 Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu,

unayeamuru ushindi kwa Yakobo.

5 Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu;

kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.

6 Siutumaini upinde wangu,

upanga wangu hauniletei ushindi;

7 bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,

unawaaibisha watesi wetu.

8 Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa,

nasi tutalisifu jina lako milele.

9 Lakini sasa umetukataa na kutudhili,

wala huendi tena na jeshi letu.

10 Umetufanya turudi nyuma mbele ya adui,

nao watesi wetu wametuteka nyara.

11 Umetuacha tutafunwe kama kondoo

na umetutawanya katika mataifa.

12 Umewauza watu wako kwa fedha kidogo,

wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao.

13 Umetufanya lawama kwa jirani zetu,

dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka.

14 Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa,

mataifa hutikisa vichwa vyao.

15 Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa,

na uso wangu umejaa aibu tele,

16 kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana,

kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi.

17 Hayo yote yametutokea,

ingawa tulikuwa hatujakusahau

wala hatujaenda kinyume na agano lako.

18 Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma;

nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako.

19 Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha,

na ukatufunika kwa giza nene.

20 Kama tungalikuwa tumelisahau jina la Mungu wetu

au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni,

21 je, Mungu hangaligundua hili,

kwa kuwa anazijua siri za moyo?

22 Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.

23 Amka, Ee Bwana! Kwa nini unalala?

Zinduka! Usitukatae milele.

24 Kwa nini unauficha uso wako

na kusahau taabu na mateso yetu?

25 Tumeshushwa hadi mavumbini,

miili yetu imegandamana na ardhi.

26 Inuka na utusaidie,

utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.