Mfalme wa Babeli Anampongeza Hezekia
Mfalme wa Babeli anampongeza Hezekia kwa kupona kwake.
713 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
12 Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia. 13 Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonyesha vitu vyote vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.
14 Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”
Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”
15 Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”
Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”
16 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana: 17 Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. 18 Nao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
19 Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Lakini si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”
Uvamizi wa Pili wa Senakeribu kwa Ufupi 710 KK
Utangulizi wa uvamizi wa pili wa Senakeribu, au maelezo yake kwa ufupi.
9 Hatimaye Senakeribu mfalme wa Ashuru na majeshi yake yote walipokuwa wameuzunguka Lakishi, akawatuma maafisa wake kwenda Yerusalemu wakiwa na ujumbe huu kwa Hezekia mfalme wa Yuda, na kwa watu wote wa Yuda waliokuwako humo, kusema:
10 “Hili ndilo asemalo Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mmeweka tumaini lenu wapi, hata mnaendelea kukaa katika Yerusalemu, hali mmezungukwa na jeshi? 11 Hezekia asemapo, ‘Bwana Mungu wetu atatuokoa kutokana na mkono wa mfalme wa Ashuru,’ anawapotosha ninyi, naye atawaacha mfe kwa njaa na kiu. 12 Je, si Hezekia mwenyewe aliyeondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu pamoja na madhabahu zake, akiwaambia Yuda wa Yerusalemu, ‘Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu moja na kuteketeza dhabihu juu yake’?
13 “Je, hamjui yale mimi na baba zangu tuliyoyafanya kwa mataifa yote ya nchi zingine? Je, miungu ya mataifa hayo iliweza kuokoa nchi zao kutoka mkononi mwangu? 14 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya mataifa haya ambayo baba zangu waliyaangamiza ameweza kuwaokoa watu wake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mungu wenu kuwaokoa mkononi mwangu? 15 Sasa basi, msikubali Hezekia awadanganye na kuwapotosha namna hii. Msimwamini, kwa kuwa hakuna mungu wa taifa lolote wala wa ufalme wowote aliyeweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu au mkononi mwa baba zangu. Sembuse huyo mungu wenu atawaokoaje kutoka mkononi mwangu!”
16 Maafisa wa Senakeribu wakaendelea kunena dhidi ya Bwana aliye Mungu na dhidi ya mtumishi wake Hezekia. 17 Mfalme pia aliandika barua akimtukana Bwana, Mungu wa Israeli na kusema haya dhidi yake: “Kama vile miungu ya mataifa ya nchi nyingine ilivyoshindwa kuwaokoa watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu.” 18 Kisha wakawaita kwa Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa juu ya ukuta ili kuwatisha na kuwatia hofu ili waweze kuuteka mji. 19 Wakanena juu ya Mungu wa Yerusalemu kama vile walivyonena juu ya miungu ya mataifa mengine ya dunia ambayo ni kazi ya mikono ya wanadamu.
20 Mfalme Hezekia na nabii Isaya mwana wa Amozi wakalilia mbingu katika maombi kuhusu jambo hili. 21 Naye Bwana akamtuma malaika ambaye aliangamiza wanajeshi wote, na viongozi na maafisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Kwa hiyo, mfalme wa Ashuru akarudi nchini mwake kwa aibu. Naye alipokwenda katika hekalu la mungu wake, baadhi ya watoto wake wakamuua kwa upanga.
22 Hivyo Bwana akamwokoa Hezekia na watu wa Yerusalemu kutoka mkononi mwa Senakeribu mfalme wa Ashuru na kutoka mikononi mwa wengine wote. Bwana akawastarehesha kila upande. 23 Watu wengi wakaleta sadaka Yerusalemu kwa ajili ya Bwana na zawadi za thamani kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda. Tangu hapo na kuendelea, Hezekia aliheshimiwa sana na mataifa yote.