Upumbavu wa Ibada ya Sanamu na Kuongoka kwa watu wa Mataifa

710 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 44–45

1 “Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu,

Israeli, niliyemchagua.

2 Hili ndilo asemalo Bwana,

yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni,

yeye atakayekusaidia:

Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu,

Yeshuruni, niliyekuchagua.

3 Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu,

na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka;

nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako,

nayo baraka yangu juu ya wazao wako.

4 Nao watachipua kama manyasi katika shamba la majani,

kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo.

5 Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa Bwana’;

mwingine atajiita kwa jina la Yakobo;

vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa Bwana,’

na kujiita kwa jina la Israeli.

6 “Hili ndilo asemalo Bwana,

Mfalme wa Israeli na Mkombozi,

Bwana Mwenye Nguvu Zote:

Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho;

zaidi yangu hakuna Mungu.

7 Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze.

Yeye atangaze na kuweka mbele yangu

ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,

tena ni nini kitakachotokea:

naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.

8 Msitetemeke, msiogope.

Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani?

Ninyi ni mashahidi wangu.

Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi?

Hasha, hakuna Mwamba mwingine;

mimi simjui mwingine.”

9 Wote wachongao sanamu ni ubatili,

navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.

Wale ambao wanazitetea ni vipofu,

ni wajinga, nao waaibika.

10 Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,

ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?

11 Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,

mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.

Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,

watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.

12 Muhunzi huchukua kifaa

na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,

hutengeneza sanamu kwa nyundo,

huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.

Huona njaa na kupoteza nguvu zake,

asipokunywa maji huzimia.

13 Seremala hupima kwa kutumia kamba

na huuchora mstari kwa kalamu;

huchonga kwa patasi

na kutia alama kwa bikari.

Huifanyiza katika umbo la binadamu,

la mwanadamu katika utukufu wake wote,

ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.

14 Hukata miti ya mierezi,

huchukua mtiriza au mwaloni.

Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,

au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.

15 Ni kuni ya binadamu:

yeye huchukua baadhi yake na kuota moto,

huwasha moto na kuoka mkate.

Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,

huitengeneza sanamu na kuisujudia.

16 Sehemu ya kuni huziweka motoni,

akapikia chakula chake,

hubanika nyama na kula hadi ashibe.

Huota moto na kusema,

“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”

17 Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;

yeye huisujudia na kuiabudu.

Huiomba na kusema,

“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”

18 Hawajui chochote, hawaelewi chochote,

macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona,

akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.

19 Hakuna anayefikiri,

hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,

“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;

hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,

nikabanika nyama na kuila.

Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?

Je, nisujudie gogo la mti?”

20 Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;

hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,

“Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”

21 “Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,

ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.

Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu.

Ee Israeli, sitakusahau.

22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu,

dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.

Nirudie mimi,

kwa kuwa nimekukomboa wewe.”

23 Enyi mbingu, imbeni kwa furaha,

kwa maana Bwana amefanya jambo hili.

Ee vilindi vya dunia, piga kelele.

Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,

enyi misitu na miti yenu yote,

kwa maana Bwana amemkomboa Yakobo,

ameuonyesha utukufu wake katika Israeli.

24 “Hili ndilo asemalo Bwana,

Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni:

“Mimi ni Bwana,

niliyeumba vitu vyote,

niliyezitanda mbingu peke yangu,

niliyeitandaza nchi mwenyewe,

25 “mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo,

na kuwatia upumbavu waaguzi,

niyapinduaye maarifa ya wenye hekima,

na kuyafanya kuwa upuzi,

26 niyathibitishaye maneno ya watumishi wake,

na kutimiza utabiri wa wajumbe wake,

“niambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’

niambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’

na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’

27 niambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka,

nami nitakausha vijito vyako,’

28 nisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu,

naye atatimiza yote yanipendezayo;

atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,”

na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’

45:1 “Hili ndilo asemalo Bwana kwa mpakwa mafuta wake,

Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume

kutiisha mataifa mbele yake

na kuwavua wafalme silaha zao,

kufungua milango mbele yake

ili malango yasije yakafungwa:

2 Nitakwenda mbele yako

na kusawazisha milima;

nitavunjavunja malango ya shaba

na kukatakata mapingo ya chuma.

3 Nitakupa hazina za gizani,

mali zilizofichwa mahali pa siri,

ili upate kujua ya kwamba Mimi ndimi Bwana,

Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.

4 Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu,

Israeli niliyemchagua,

nimekuita wewe kwa jina lako,

na kukupa jina la heshima,

ingawa wewe hunitambui.

5 Mimi ndimi Bwana, wala hakuna mwingine,

zaidi yangu hakuna Mungu.

Nitakutia nguvu,

ingawa wewe hujanitambua,

6 ili kutoka mawio ya jua

mpaka machweo yake,

watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi.

Mimi ndimi Bwana wala hakuna mwingine.

7 Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza,

ninaleta mafanikio na kusababisha maafa.

Mimi, Bwana, huyatenda haya yote.

8 “Enyi mbingu juu, nyesheni haki,

mawingu na yaidondoshe.

Dunia na ifunguke sana,

wokovu na uchipuke,

haki na ikue pamoja nao.

Mimi, Bwana, ndiye niliyeiumba.

9 “Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake,

yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi.

Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi,

‘Unatengeneza nini wewe?’

Je, kazi yako husema,

‘Hana mikono’?

10 Ole wake amwambiaye baba yake,

‘Umezaa nini?’

Au kumwambia mama yake,

‘Umezaa kitu gani?’

11 “Hili ndilo asemalo Bwana,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake:

Kuhusu mambo yatakayokuja,

je, unaniuliza habari za watoto wangu,

au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?

12 Mimi ndiye niliyeumba dunia

na kumuumba mwanadamu juu yake.

Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,

nikayapanga majeshi yake yote ya angani.

13 Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu:

nitazinyoosha njia zake zote.

Yeye atajenga mji wangu upya,

na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni,

lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi,

asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

14 Hili ndilo asemalo Bwana:

“Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi,

nao wale Waseba warefu,

watakujia na kuwa wako,

watakujia wakijikokota nyuma yako,

watakujia wamefungwa minyororo.

Watasujudu mbele yako

wakikusihi na kusema,

‘Hakika Mungu yu pamoja nawe,

wala hakuna mwingine;

hakuna Mungu mwingine.’ ”

15 Hakika wewe u Mungu unayejificha,

Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli.

16 Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika;

wataenda kutahayarika pamoja.

17 Lakini Israeli ataokolewa na Bwana

kwa wokovu wa milele;

kamwe hutaaibika wala kutatahayarika,

milele yote.

18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana,

yeye aliyeumba mbingu,

ndiye Mungu;

yeye aliyeifanya dunia na kuiumba,

yeye ndiye aliiwekea misingi imara,

hakuiumba ili iwe tupu,

bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.

Anasema:

“Mimi ndimi Bwana,

wala hakuna mwingine.

19 Sijasema sirini,

kutoka mahali fulani katika nchi ya giza;

sijawaambia wazao wa Yakobo,

‘Nitafuteni bure.’

Mimi, Bwana, nasema kweli;

ninatangaza lililo sahihi.

20 “Kusanyikeni pamoja mje,

enyi wakimbizi kutoka mataifa.

Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili,

wale waombao miungu isiyoweza kuokoa.

21 Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo,

wao na wafanye shauri pamoja.

Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani,

aliyetangaza tangu zamani za kale?

Je, haikuwa Mimi, Bwana?

Wala hapana Mungu mwingine

zaidi yangu mimi,

Mungu mwenye haki na Mwokozi;

hapana mwingine ila mimi.

22 “Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe,

enyi miisho yote ya dunia;

kwa maana mimi ndimi Mungu,

wala hapana mwingine.

23 Nimeapa kwa nafsi yangu,

kinywa changu kimenena katika uadilifu wote

neno ambalo halitatanguka:

Kila goti litapigwa mbele zangu,

kwangu mimi kila ulimi utaapa.

24 Watasema kuhusu mimi,

‘Katika Bwana peke yake

ndiko kuna haki na nguvu.’ ”

Wote ambao wamemkasirikia Mungu

watamjia yeye, nao watatahayarika.

25 Lakini katika Bwana wazao wote wa Israeli

wataonekana wenye haki na watashangilia.