Kuitwa kwa Samweli
1143 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Kijana Samweli alihudumu mbele za Bwana chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwepo na maono mengi.
2 Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida. 3 Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala Hekaluni mwa Bwana, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwako. 4 Kisha Bwana akamwita Samweli.
Samweli akajibu, “Mimi hapa.” 5 Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”
Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala.
6 Bwana akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”
Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.”
7 Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua Bwana. Neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”
Ndipo Eli akatambua kuwa Bwana alikuwa akimwita kijana. 9 Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale, na kama akikuita, sema, ‘Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake.
10 Bwana akaja akasimama hapo, akiita kama mara zile nyingine, “Samweli! Samweli!”
Kisha Samweli akasema, “Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”
11 Naye Bwana akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. 12 Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. 13 Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. 14 Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”
15 Samweli akalala mpaka asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya Bwana. Aliogopa kumwambia Eli yale maono, 16 lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.”
Samweli akamjibu, “Mimi hapa.”
17 Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. Bwana na ashughulike nawe, tena kwa ukali, kama utanificha chochote alichokuambia.” 18 Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu, bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Bwana; na afanye lile lililo jema machoni pake!”
19 Bwana alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha hata moja ya maneno yake lianguke chini. 20 Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa Bwana. 21 Bwana akaendelea kutokea huko Shilo, na huko kujidhihirisha kwa Samweli kwa njia ya neno lake.
Samsoni Anaoa na Kupigana na Wafilisti 1136 KK
Ndoa ya Samsoni, na matendo yake ya kishujaa dhidi ya Wafilisti.
1 Samsoni akateremkia Timna, akamwona mwanamke wa Kifilisti. 2 Alipopanda kutoka huko, akawaambia baba yake na mama yake, “Nimemwona mwanamke wa Kifilisti huko Timna; basi mnipe ili awe mke wangu.”
3 Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa ndugu zako, hata ulazimike kwenda kujitwalia mwanamke kutoka kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa?”
Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye alinipendeza.” 4 (Baba yake na mama yake hawakujua kuwa jambo hili limetoka kwa Bwana, kwani alikuwa akitafuta sababu ya kukabiliana na Wafilisti; kwa kuwa wakati huo walikuwa wakiwatawala Waisraeli.) 5 Samsoni akateremkia Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia. 6 Roho wa Bwana akaja juu yake kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono yake bila silaha yoyote kama vile mtu ampasuavyo mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake aliyoyafanya. 7 Basi akateremka na kuongea na yule mwanamke, naye akampendeza Samsoni.
8 Baada ya muda aliporudi ili akamwoe, akatazama kando ili kuutazama mzoga wa yule simba, na tazama, kulikuwa na kundi la nyuki ndani ya ule mzoga wa simba na kulikuwa na asali; 9 akachukua asali mkononi mwake akaendelea huku akila. Alipowafikia baba yake na mama yake, akawapa ile asali nao wakala. Lakini hakuwaambia kuwa alitwaa asali kutoka kwenye mzoga wa simba.
10 Basi baba yake akateremka kumwona huyo mwanamke. Samsoni akafanya karamu huko, kama ilivyokuwa desturi ya vijana. 11 Watu walipomwona, wakaleta vijana wenzake thelathini ili kuwa pamoja naye.
12 Samsoni akawaambia, “Niwape kitendawili, mkiweza kunipa jibu katika muda wa siku hizi saba za karamu, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini. 13 Lakini msipoweza kufumbua, ndipo ninyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.”
Wakamwambia, “Tuambie hicho kitendawili, hebu na tukisikie.”
14 Akawaambia,
“Ndani ya mlaji,
kulitoka kitu cha kuliwa,
ndani ya mwenye nguvu,
kulitoka kitu kitamu.”
Kwa muda wa siku tatu hawakuweza kutoa jibu.
15 Siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atueleze hicho kitendawili, la sivyo tutakuchoma moto wewe na wa nyumba ya baba yako. Je, mmetualika ili mpate kutunyangʼanya kile tulicho nacho?”
16 Basi mke wa Samsoni akalia mbele yake na kumwambia, “Unanichukia! Hunipendi kabisa. Umewategea watu wangu kitendawili, lakini mimi hujaniambia jibu.”
Samsoni akamwambia, “Wala sijamweleza baba yangu wala mama yangu, kwa nini nikufumbulie?” 17 Mkewe akalia kwa muda wa zile siku zote saba za karamu. Hivyo siku ile ya saba Samsoni akamweleza, kwa kuwa aliendelea kumsisitiza sana. Naye akawaeleza watu wake kile kitendawili.
18 Siku ya saba kabla ya jua kutua, watu wa mji wakamwambia Samsoni,
“Ni nini kitamu kama asali?
Ni nini chenye nguvu kama simba?”
Samsoni akawaambia,
“Kama hamkulima na mtamba wangu,
hamngeweza kufumbua
kitendawili changu.”
19 Ndipo Roho wa Bwana akamjia Samsoni kwa nguvu. Akateremka mpaka Ashkeloni, akawaua watu waume thelathini miongoni mwa watu wa mji, akatwaa mali zao na nguo zao, akawapa watu wale waliofumbua kile kitendawili. Akiwa na hasira, akakwea kurudi nyumbani kwa baba yake. 20 Lakini huyo mke wa Samsoni akakabidhiwa kwa rafiki yake Samsoni ambaye alikuwa rafiki yake msaidizi siku ya arusi.