Samsoni Anaoa na Kupigana na Wafilisti (continued)

Ndoa ya Samsoni, na matendo yake ya kishujaa dhidi ya Wafilisti.

1136 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Waamuzi 15:1–19

1 Baada ya kitambo kidogo, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni akachukua mwana-mbuzi, kwenda kumzuru mkewe. Akasema, “Nataka kuingia chumbani kwa mke wangu.” Lakini baba yake huyo mwanamke hakumruhusu kuingia.

2 Huyo baba mkwe wake akamwambia, “Nilikuwa na hakika kwamba ulimkataa, hivyo mimi nikampa rafiki yako. Je, mdogo wake wa kike si mzuri zaidi kuliko yeye? Mchukue huyo badala yake.”

3 Samsoni akawaambia, “Wakati huu, nitakapowadhuru Wafilisti, sitakuwa na lawama.” 4 Hivyo Samsoni akatoka akawakamata mbweha 300 na kuwafunga wawili wawili kwa mikia yao kila mmoja kwa mwingine. Kisha akafungia mwenge wa moto, kwenye mikia ya kila jozi moja ya mbweha aliyokuwa ameifunga, 5 akawasha ile mienge na kuwaachia wale mbweha katika mashamba ya Wafilisti ya nafaka zilizosimamishwa katika matita. Akateketeza matita ya nafaka zilizosimama, pamoja na mashamba ya mizabibu na viunga vya mizeituni.

6 Ndipo Wafilisti wakauliza, “Ni nani aliyetenda jambo hili?” Wakaambiwa, “Ni Samsoni, yule mkwewe Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake.”

Hivyo Wafilisti wakapanda wakamteketeza kwa moto yeye huyo mwanamke pamoja na baba yake. 7 Samsoni akawaambia, “Kwa kuwa mmetenda hivyo, hakika sitatulia mpaka niwe nimelipiza kisasi juu yenu.” 8 Akawashambulia kwa ukali kwa mapigo makuu na kuwaua watu wengi sana. Kisha akateremka na kukaa katika ufa kwenye mwamba wa Etamu.

9 Wafilisti wakapanda na kupiga kambi huko Yuda na kuenea huko Lehi. 10 Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kupigana nasi?”

Wakawajibu, “Tumekuja ili kumkamata Samsoni na kumtenda kama alivyotutendea.”

11 Ndipo watu 3,000 toka Yuda walipoteremka na kwenda kwenye ufa wa mwamba huko Etamu, na kumwambia Samsoni, “Je, hujatambua kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hiki ulichotutendea?”

Akawajibu, “Mimi nimewatendea tu kile walichonitendea.”

12 Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga na kukutia mikononi mwa Wafilisti.”

Samsoni akawaambia, “Niapieni kuwa hamtaniua ninyi wenyewe.”

13 Wakamjibu, “Sisi hatutakuua, bali tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya. Wakamchukua toka huko kwenye ufa katika mwamba. 14 Alipokaribia Lehi, Wafilisti wakamjia wakipiga kelele. Roho wa Bwana akamjia juu yake kwa nguvu. Kamba zilizomfunga mikono yake zikawa kama kitani iliyochomwa kwa moto, na vifungo vyake vikaanguka chini toka mikononi mwake. 15 Ndipo akaona mfupa mpya wa taya la punda, akanyoosha mkono, akauchukua na kuua nao Wafilisti wapatao 1,000.

16 Ndipo Samsoni akasema,

“Kwa taya la punda

malundo juu ya malundo.

Kwa taya la punda

nimeua watu 1,000.”

17 Alipomaliza kusema, akautupa ule mfupa wa taya; na mahali pale pakaitwa Ramath-Lehi.

18 Kwa kuwa alikuwa amesikia kiu sana, akamlilia Bwana akisema, “Umempa mtumishi wako ushindi huu mkuu. Je, sasa nife kwa kiu na kuangukia mikononi mwa hawa watu wasiotahiriwa?” 19 Bwana akafunua shimo huko Lehi, pakatoka maji. Samsoni alipoyanywa, nguvu zikamrudia na kuhuika. Hivyo chemchemi ile ikaitwa En-Hakore, nayo iko mpaka leo huko Lehi.

Nabii Anatumwa kwa Eli 1117 KK

1 Samweli 2:22–36

22 Basi Eli, ambaye alikuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania. 23 Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote juu ya haya matendo yenu maovu. 24 Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ambayo ninasikia ikienea miongoni mwa watu wa Bwana. 25 Kama mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu Bwana alitaka kuwaua.

26 Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza Bwana na wanadamu.

27 Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao? 28 Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kisibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli. 29 Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka zile nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’

30 “Kwa hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa Bwana anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa. 31 Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika mbari yenu atakayeishi kuuona uzee 32 nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watafanyiwa mema, katika mbari yenu kamwe hapatakuwepo mtu atakayeishi hadi kuwa mzee. 33 Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi.

34 “ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja. 35 Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaifanya nyumba yake kuwa imara, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima. 36 Kisha kila mmoja aliyeachwa katika mbari yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.” ’ ”