Kuzaliwa kwa Samweli
1155 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Kulikuwepo na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ambaye jina lake aliitwa Elikana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu. 2 Alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto.
3 Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Bwana. 4 Kila mara ilipofika siku ya Elikana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote pamoja na binti zake. 5 Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 6 Kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi. 7 Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda katika nyumba ya Bwana, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha mpaka analia na kushindwa kula. 8 Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”
9 Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la Bwana. 10 Kwa uchungu wa rohoni Hana alilia sana na akamwomba Bwana. 11 Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa Bwana kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”
12 Alipokuwa anaendelea kumwomba Bwana, Eli alichunguza kinywa chake. 13 Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa 14 naye akamwambia, “Utaendelea kulewa mpaka lini? Achilia mbali mvinyo wako.”
15 Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Bwana. 16 Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa katika wingi wa uchungu mkuu na huzuni.”
17 Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.”
18 Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.
19 Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za Bwana na kisha wakarudi nyumbani kwao huko Rama. Elikana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye Bwana akamkumbuka. 20 Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa Bwana.”
21 Wakati huyo mtu Elikana alipanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa Bwana na kutimiza nadhiri yake, 22 Hana hakwenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za Bwana, naye ataishi huko wakati wote.”
23 Elikana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa mpaka utakapomwachisha kunyonya, Bwana na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe mpaka alipomwachisha kunyonya.
24 Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya Bwana huko Shilo. 25 Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli, 26 naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Bwana. 27 Niliomba mtoto huyu, naye Bwana amenijalia kile nilichomwomba. 28 Hivyo sasa ninamtoa kwa Bwana. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Bwana.” Naye akamwabudu Bwana huko.
2:1 Kisha Hana akaomba na kusema:
“Moyo wangu wamshangilia Bwana,
katika Bwana pembe yangu imeinuliwa juu.
Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,
kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
2 “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Bwana,
hakuna mwingine zaidi yako;
hakuna Mwamba kama Mungu wetu.
3 “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo
wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi,
kwa kuwa Bwana ndiye Mungu ajuaye,
na kwa yeye matendo hupimwa.
4 “Pinde za mashujaa zimevunjika,
lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.
5 Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe
ili kupata chakula,
lakini wale waliokuwa na njaa
hawana njaa tena.
Mwanamke yule aliyekuwa tasa
amezaa watoto saba,
lakini yule ambaye alikuwa na wana wengi
amedhoofika.
6 “Bwana huua na huleta uhai,
hushusha chini mpaka kaburini na hufufua.
7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha,
hushusha na hukweza.
8 Humwinua maskini kutoka mavumbini
na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;
huwaketisha pamoja na wakuu
na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.
“Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana;
juu yake ameuweka ulimwengu.
9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake,
lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza.
“Si kwa nguvu mtu hushinda;
10 wale wampingao Bwana
wataharibiwa kabisa.
Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni;
Bwana ataihukumu miisho ya dunia.
“Atampa nguvu mfalme wake,
na kuitukuza pembe
ya mpakwa mafuta wake.”
11 Kisha Elikana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za Bwana chini ya kuhani Eli.
12 Wana wa Eli walikuwa watu wabaya kabisa, hawakumheshimu Bwana. 13 Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake. 14 Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angalijichukulia mwenyewe chochote ambacho uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo. 15 Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na kusema kwa mtu ambaye alikuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.”
16 Kama mtu akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angalijibu, “Hapana, nipe sasa, kama huwezi nitaichukua kwa nguvu.”
17 Hii Dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Bwana, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya Bwana kwa dharau.
18 Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za Bwana, kijana akivaa kisibau cha kitani. 19 Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumchukulia wakati alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka. 20 Eli alikuwa akiwabariki Elikana na mkewe, akisema, “Bwana na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa Bwana.” Kisha wakawa wanakwenda nyumbani. 21 Bwana akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za Bwana.