Sanduku Linahamishiwa Yerusalemu

Sanduku Linaletwa kutoka Kiriath-Yearimu

1045 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Samweli 6:1–11

1 Tena Daudi akakusanya watu 30,000 wa Israeli waliochaguliwa. 2 Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, ambaye anaketi katika kiti cha enzi kati ya makerubi walioko juu ya hilo Sanduku. 3 Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa 4 likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake. 5 Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za Bwana kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi.

6 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa. 7 Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.

8 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Bwana ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza.

9 Daudi akamwogopa Bwana siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la Bwana litakavyoweza kunijia?” 10 Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la Bwana kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti. 11 Sanduku la Bwana likabaki katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye Bwana akambariki pamoja na nyumba yake yote.

Zaburi Iliyoandikwa Sanduku Linapohamishwa kwa Mara ya Kwanza

Zaburi 68

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo.

1 Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike,

adui zake na wakimbie mbele zake.

2 Kama vile moshi upeperushwavyo na upepo,

vivyo hivyo uwapeperushe mbali,

kama vile nta iyeyukavyo kwenye moto,

vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu.

3 Bali wenye haki na wafurahi,

washangilie mbele za Mungu,

wafurahi na kushangilia.

4 Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake,

mtukuzeni yeye aendeshwaye juu ya mawingu:

jina lake ni Bwana,

furahini mbele zake.

5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,

ni Mungu katika makao yake matakatifu.

6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa,

huwaongoza wafungwa wakiimba,

bali waasi huishi katika nchi kame.

7 Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako,

ulipopita nyikani,

8 dunia ilitikisika,

mbingu zikanyesha mvua,

mbele za Mungu, Yule wa Sinai,

mbele za Mungu, Mungu wa Israeli.

9 Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi

na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka.

10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko,

nawe kwa wingi wa utajiri wako

uliwapa maskini mahitaji yao.

11 Bwana alitangaza neno,

waliolitangaza neno hilo walikuwa kundi kubwa:

12 “Wafalme na majeshi walikimbia upesi,

watu waliobaki kambini waligawana nyara.

13 Hata ulalapo katikati ya mioto ya kambini,

mabawa ya njiwa wangu yamefunikwa kwa fedha,

manyoya yake kwa dhahabu ingʼaayo.”

14 Wakati Mwenyezi alipowatawanya wafalme katika nchi,

ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Salmoni.

15 Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka,

milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka.

16 Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka,

kwa nini mnakazia macho kwa wivu,

katika mlima Mungu anaochagua kutawala,

ambako Bwana mwenyewe ataishi milele?

17 Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu,

na maelfu ya maelfu;

Bwana amekuja kutoka Sinai

hadi katika patakatifu pake.

18 Ulipopanda juu, uliteka mateka,

ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu,

hata kutoka kwa wale walioasi,

ili wewe, Ee Bwana Mungu, upate kuishi huko.

19 Sifa apewe Bwana, Mungu Mwokozi wetu,

ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu.

20 Mungu wetu ni Mungu aokoaye,

Bwana Mwenyezi hutuokoa na kifo.

21 Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake,

vichwa vya hao waendao katika njia za dhambi.

22 Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani;

nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,

23 ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako,

huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.”

24 Ee Mungu, maandamano yako yameonekana,

maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu,

yakielekea patakatifu pake.

25 Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda,

pamoja nao wako wanawali wakipiga matari.

26 Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa,

msifuni Bwana katika kusanyiko la Israeli.

27 Liko kabila dogo la Benyamini likiwaongoza,

wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda,

hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali.

28 Ee Mungu, amuru uwezo wako,

Ee Mungu tuonyeshe nguvu zako,

kama ulivyofanya hapo awali.

29 Kwa sababu ya Hekalu lako Yerusalemu

wafalme watakuletea zawadi.

30 Mkemee mnyama aliyeko kwenye manyasi,

kundi la mafahali katikati ya ndama za mataifa.

Na walete minara ya madini ya fedha wakinyenyekea.

Tawanya mataifa yapendayo vita.

31 Wajumbe watakuja kutoka Misri,

Kushi atajisalimisha kwa Mungu.

32 Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia,

mwimbieni Bwana sifa,

33 mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu,

yeye angurumaye kwa sauti kuu.

34 Tangazeni uwezo wa Mungu,

ambaye fahari yake iko juu ya Israeli,

ambaye uwezo wake uko katika anga.

35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako,

Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu.

Mungu Asifiwe!