Sanduku Linaondoka Nyumbani kwa Obed-Edomu
Kuhamishwa kwa sanduku kwa mara ya pili, kutoka nyumbani kwa Obed-Edomu.
1045 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Baada ya Daudi kujijengea nyumba zake katika Mji wa Daudi, akatengeneza sehemu kwa ajili ya Sanduku la Mungu, kisha akasimamisha hema kwa ajili yake. 2 Kisha Daudi akasema, “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulibeba Sanduku la Mungu isipokuwa Walawi peke yao, kwa sababu Bwana aliwachagua kulibeba Sanduku la Bwana na kuhudumu mbele zake milele.”
3 Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu ili kulipandisha Sanduku la Bwana na kulileta hadi kwenye sehemu aliyokuwa ametengeneza kwa ajili yake. 4 Kisha Daudi akawakusanya pamoja wazao wa Aroni na Walawi:
5 Kutoka wazao wa Kohathi,
Urieli kiongozi na ndugu zake 120,
6 Kutoka wazao wa Merari,
Asaya kiongozi na ndugu zake 220.
7 Kutoka wazao wa Gershoni,
Yoeli kiongozi na ndugu zake 130.
8 Kutoka wazao wa Elisafani,
Shemaya kiongozi na ndugu zake 200.
9 Kutoka wazao wa Hebroni,
Elieli kiongozi na ndugu zake 80.
10 Kutoka wazao wa Uzieli,
Aminadabu kiongozi na ndugu zake 112.
11 Kisha Daudi akawaita makuhani Sadoki na Abiathari, pamoja na Walawi Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu. 12 Akawaambia, “Ninyi ndio viongozi wa jamaa za Walawi. Ninyi pamoja na Walawi wenzenu inawapasa mjitakase na kulipandisha Sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli hadi mahali ambapo nimetengeneza kwa ajili yake. 13 Ilikuwa ni kwa sababu hii, ninyi Walawi, hamkulipandisha Sanduku la Bwana mara ya kwanza, hata ikasababisha Bwana Mungu wetu kuwaka hasira dhidi yetu. Hatukumuuliza jinsi ya kufanya ili tupate kulileta jinsi alivyoagiza.” 14 Kwa hiyo makuhani pamoja na Walawi wakajitakasa ili kulipandisha Sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli.
Zaburi Iliyoandikwa Kabla ya Kuhamishwa kwa Sanduku kwa Mara ya Pili
Zaburi iliyoandikwa wakati maandalizi yanafanywa ya kuhamisha sanduku kwa mara ya pili.
Wimbo wa kwenda juu.
1 Ee Bwana, mkumbuke Daudi
na taabu zote alizozistahimili.
2 Aliapa kiapo kwa Bwana
na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo:
3 “Sitaingia nyumbani mwangu
au kwenda kitandani mwangu:
4 sitaruhusu usingizi katika macho yangu,
wala kope zangu kusinzia,
5 mpaka nitakapompatia Bwana mahali,
makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
6 Tulisikia habari hii huko Efrathi,
tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara:
7 “Twendeni kwenye makao yake,
na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake;
8 inuka, Ee Bwana, uje mahali pako pa kupumzikia,
wewe na Sanduku la nguvu zako.
9 Makuhani wako na wavikwe haki,
watakatifu wako na waimbe kwa furaha.”
10 Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako,
usimkatae mpakwa mafuta wako.
11 Bwana alimwapia Daudi kiapo,
kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua:
“Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe
katika kiti chako cha enzi,
12 kama wanao watashika Agano langu
na sheria ninazowafundisha,
ndipo wana wao watarithi
kiti chako cha enzi milele na milele.”
13 Kwa maana Bwana ameichagua Sayuni,
amepaonea shauku pawe maskani yake:
14 “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele;
hapa ndipo nitakapoketi nikitawala, kwa sababu nimepaonea shauku:
15 Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele:
nitashibisha maskini wake kwa chakula.
16 Nitawavika makuhani wake wokovu,
nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha.
17 “Hapa nitamchipushia Daudi pembe,
na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu.
18 Adui zake nitawavika aibu,
bali taji kichwani pake itangʼaa sana.”
12 Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Bwana ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. 13 Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Bwana walipokuwa wametembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. 14 Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote, 15 wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Bwana kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
16 Ikawa Sanduku la Bwana lilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Bwana, akamdharau moyoni mwake.
17 Wakaleta Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. 18 Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote. 19 Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani kwao.
15 Nao Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu mabegani mwao wakitumia mipiko, kama vile Mose alivyoamuru sawasawa na neno la Bwana.
16 Daudi akawaambia viongozi wa Walawi kuwaweka ndugu zao waimbaji ili waimbe nyimbo za shangwe, wakiwa na vyombo vya uimbaji: zeze, vinubi na matoazi.
17 Basi Walawi wakawaweka Hemani mwana wa Yoeli; kutoka miongoni mwa ndugu zake, Asafu mwana wa Berekia; kutoka miongoni mwa ndugu zao Wamerari, Ethani mwana wa Kushaiya; 18 hawa ndio waliochaguliwa kuwa wasaidizi wao: Zekaria, Yaazieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu, Mikneya, pamoja na mabawabu Obed-Edomu na Yehieli.
19 Waimbaji Hemani, Asafu na Ethani walichaguliwa kupiga matoazi ya shaba; 20 Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya walikuwa wapiga zeze kufuatana na sauti ya alamothi, 21 na Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-Edomu, Yehieli na Azazia walikuwa wapiga vinubi, wakiongozwa kwa kufuata sauti ya sheminithi. 22 Kenania kiongozi wa Walawi alikuwa msimamizi wa uimbaji; huu ndio uliokuwa wajibu wake kwa sababu alikuwa stadi katika hilo.
23 Berekia na Elikana walikuwa mabawabu kwa ajili ya Sanduku. 24 Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, makuhani, walikuwa wapiga tarumbeta mbele ya Sanduku la Mungu. Obed-Edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa mabawabu wa Sanduku.
25 Basi Daudi pamoja na wazee wa Israeli na majemadari wa vikosi vya elfu wakaenda ili kulipandisha Sanduku la Agano la Bwana kutoka nyumba ya Obed-Edomu kwa shangwe. 26 Kwa sababu Mungu alikuwa amewasaidia Walawi waliokuwa wanalichukua Sanduku la Agano la Bwana, mafahali saba na kondoo dume saba walitolewa dhabihu. 27 Basi Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, kama walivyokuwa wamevaa Walawi wote waliokuwa wanalichukua lile Sanduku, waimbaji nao walivaa vivyo hivyo, pamoja na Kenania aliyekuwa anaongoza nyimbo za waimbaji. Daudi alivaa pia kisibau cha kitani safi. 28 Hivyo Israeli wote wakalipandisha Sanduku la Agano la Bwana kwa shangwe, wakipiga pembe za kondoo dume, tarumbeta, matoazi, wakipiga zeze na vinubi.
29 Sanduku la Agano la Bwana lilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akicheza na kusherehekea, akamdharau moyoni mwake.