Hiramu Anampongeza Daudi

Hiramu anampongeza Daudi. Wafilisti wanavamia.

1047 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Samweli 5:11–25

11 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mierezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi. 12 Naye Daudi akafahamu kuwa Bwana amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake.

13 Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana na binti wengi walizaliwa kwake. 14 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, 15 Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia, 16 Elishama, Eliada na Elifeleti.

17 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome. 18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai, 19 kwa hiyo Daudi akamuuliza Bwana, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

Bwana akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”

20 Ndipo Daudi akaenda mpaka Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yafurikavyo, Bwana amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu. 21 Wafilisti wakaiacha miungu yao huko, naye Daudi na watu wake wakaichukua.

22 Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai. 23 Kwa hiyo Daudi akamuuliza Bwana, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi. 24 Mara utakaposikia sauti ya kutembea kutoka kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa Bwana ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.” 25 Basi Daudi akafanya kama Bwana alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.

1 Nyakati 14:17

17 Hivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, naye Bwana akayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.

1 Nyakati 14:1–16

1 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mierezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme. 2 Naye Daudi akatambua kwamba Bwana amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake.

3 Huko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana na mabinti wengi. 4 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, 5 Ibihari, Elishua, Elpeleti, 6 Noga, Nefegi, Yafia, 7 Elishama, Beeliada na Elifeleti.

8 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli yote, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao. 9 Basi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai, 10 Hivyo Daudi akamuuliza Mungu: “Je, niende kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

Bwana akamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.”

11 Hivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea mpaka Baal-Perasimu, akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yafurikavyo, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu. 12 Wafilisti walikuwa wameacha miungu yao huko, Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto.

13 Kwa mara nyingine Wafilisti wakavamia lile bonde; 14 hivyo Daudi akamuuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwapandie moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi. 15 Mara usikiapo sauti ya kwenda juu ya hiyo miti ya miforosadi, hapo ndipo utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonyesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.” 16 Kwa hiyo Daudi akafanya kama alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri.