Daudi Anafanywa Mfalme wa Israeli Yote

1048 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Samweli 5:1–3

1 Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu nyama yako na damu yako hasa. 2 Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye Bwana alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”

3 Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Bwana, nao wakamtia Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.

1 Nyakati 13:1–4

1 Daudi alishauriana na kila afisa wake, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. 2 Ndipo Daudi akaliambia kusanyiko lote la Israeli, “Kama mkiona ni vyema, na kama ni mapenzi ya Bwana Mungu wetu, tupeleke ujumbe kwa ndugu zetu wengine walio mbali na walio karibu katika nchi yote ya Israeli, pia kwa makuhani na Walawi walio pamoja nao katika miji yao na katika sehemu zao za malisho yao, waje waungane na sisi. 3 Sisi na tulirudishe Sanduku la Mungu wetu kwetu kwa maana hatukujali wakati wa utawala wa Sauli.” 4 Kusanyiko lote likakubaliana kufanya hivyo, kwa sababu ilionekana vyema kwa watu wote.

Zaburi 139

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Bwana, umenichunguza

na kunijua.

2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka;

unatambua mawazo yangu tokea mbali.

3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;

unaelewa njia zangu zote.

4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,

wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana.

5 Umenizunguka nyuma na mbele;

umeweka mkono wako juu yangu.

6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,

ni ya juu sana kwangu kuyafikia.

7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako?

Niende wapi niukimbie uso wako?

8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;

nikifanya vilindi kuwa kitanda changu,

wewe uko huko.

9 Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko,

kama nikikaa pande za mbali za bahari,

10 hata huko mkono wako utaniongoza,

mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.

11 Kama nikisema, “Hakika giza litanificha

na nuru inayonizunguka iwe usiku,”

12 hata giza halitakuwa giza kwako,

usiku utangʼaa kama mchana,

kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.

13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

kazi zako ni za ajabu,

ninajua hayo kikamilifu.

15 Umbile langu halikufichika kwako,

nilipoumbwa mahali pa siri.

Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

Siku zangu zote ulizonipangia

ziliandikwa katika kitabu chako

kabla haijakuwepo hata moja.

17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu!

Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!

18 Kama ningezihesabu,

zingekuwa nyingi kuliko mchanga.

Niamkapo,

bado niko pamoja nawe.

19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu!

Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!

20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya,

adui zako wanatumia vibaya jina lako.

21 Ee Bwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia?

Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?

22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao,

ninawahesabu ni adui zangu.

23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,

nijaribu na ujue mawazo yangu.

24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,

uniongoze katika njia ya milele.

1 Nyakati 12:23–40

23 Hawa ndio watu waliojiandaa kwa ajili ya vita waliokuja kwa Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Sauli, kama Bwana alivyokuwa amesema:

24 watu wa Yuda, wanaochukua ngao na mikuki walikuwa 6,800 wote wakiwa tayari kwa vita.

25 Watu wa Simeoni, mashujaa waliokuwa tayari kwa vita walikuwa 7,100.

26 Watu wa Lawi walikuwa 4,600, 27 pamoja na Yehoyada, kiongozi wa jamaa ya Aroni, aliyekuwa pamoja na watu 3,700, 28 na Sadoki, kijana shujaa na hodari, aliyekuwa pamoja na maafisa ishirini na wawili kutoka jamaa yake.

29 Watu wa Benyamini, ndugu zake Sauli, walikuwa 3,000; wengi wao walikuwa wameendelea kuwa waaminifu kwa Sauli mpaka wakati huo.

30 Watu wa Efraimu, mashujaa hodari 20,800, watu waliokuwa maarufu katika koo zao.

31 Watu wa nusu ya kabila la Manase, waliotajwa kwa majina ili waje kumweka Daudi kuwa mfalme, watu 18,000.

32 Watu wa Isakari, waliofahamu majira na kujua kile ambacho Israeli inapasa kufanya, walikuwa viongozi 200, pamoja na jamaa zao wote chini ya uongozi wao.

33 Watu wa Zabuloni, askari wenye uzoefu mkubwa walioandaliwa tayari kwa vita wakiwa na silaha za kila aina, ili kumsaidia Daudi kwa uaminifu thabiti, walikuwa 50,000.

34 Watu wa Naftali, maafisa 1,000, pamoja na watu 37,000 waliochukua ngao na mikuki.

35 Watu wa Dani 28,600 waliokuwa tayari kwa vita.

36 Watu wa Asheri, askari 40,000 wenye uzoefu mkubwa waliondaliwa kwa ajili ya vita.

37 Na pia watu kutoka mashariki ya Yordani, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakiwa na kila aina ya silaha, watu 120,000.

38 Wote hawa walikuwa watu wapiganaji waliojitolea kutumika katika safu zao. Walikuja Hebroni wakiwa wameamua kikamilifu kumfanya Daudi mfalme juu ya Israeli yote. Waisraeli wengine wote walikuwa pia na nia hiyo moja ya kumfanya Daudi kuwa mfalme. 39 Watu hawa wakakaa huko na Daudi siku tatu, wakila na kunywa, kwa sababu jamaa zao zilikuwa zimewapatia mahitaji yao. 40 Pia, majirani zao hata wale walio mbali hadi Isakari, Zabuloni na Naftali, walikuja wakiwaletea vyakula walivyovibeba kwa punda, ngamia, nyumbu na maksai. Kulikuwepo na wingi wa unga, maandazi ya tini, maandazi ya zabibu kavu, divai, mafuta, ngʼombe na kondoo, kwa maana kulikuwa na furaha katika Israeli.

2 Samweli 23:8–12

8 Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi:

Yosheb-Bashebethi, Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu 800, ambao aliwaua katika pambano moja.

9 Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai, Mwahohi. Akiwa mmojawapo wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha watu wa Israeli wakarudi nyuma, 10 lakini yeye alisimama imara akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na ukagandamana na upanga. Bwana akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari, kuteka tu nyara za waliokufa.

11 Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia. 12 Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalitetea na kuwaua Wafilisti, naye Bwana akawapa ushindi mkubwa.

1 Nyakati 11:20–47

20 Abishai, ndugu yake Yoabu ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300, ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. 21 Alitunukiwa heshima maradufu ya wale Watatu, akawa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.

22 Benaya, mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. 23 Alimuua Mmisri aliyekuwa na urefu kama dhiraa tano. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi mwake, Benaya alimwendea na rungu. Akamnyangʼanya Mmisri mkuki wake na kumuua nao. 24 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. 25 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu: Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.

26 Wale watu mashujaa walikuwa:

Asaheli nduguye Yoabu,

Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu,

27 Shamothi Mharori,

Helesi Mpeloni,

28 Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa,

Abiezeri kutoka Anathothi,

29 Sibekai Mhushathi,

Ilai Mwahohi,

30 Maharai Mnetofathi,

Heledi mwana wa Baana, Mnetofathi,

31 Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini,

Benaya Mpirathoni,

32 Hurai kutoka mabonde ya Gaashi,

Abieli Mwaribathi,

33 Azmawethi Mbaharumi,

Eliaba Mshaalboni,

34 wana wa Hashemu Mgiloni,

Yonathani mwana wa Shagee Mharari,

35 Ahiamu mwana wa Sakari Mharari,

Elifale mwana wa Uru,

36 Heferi Mmekerathi,

Ahiya Mpeloni,

37 Hezro Mkarmeli,

Naarai mwana wa Ezbai,

38 Yoeli nduguye Nathani,

Mibhari mwana wa Hagri,

39 Seleki Mwamoni,

Naharai Mbeerothi, mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya,

40 Ira Mwithiri,

Garebu Mwithiri,

41 Uria Mhiti,

Zabadi mwana wa Alai,

42 Adina mwana wa Shiza Mreubeni, ambaye alikuwa mkuu wa Wareubeni, akiwa pamoja na watu thelathini,

43 Hanani mwana wa Maaka,

Yoshafati Mmithni,

44 Uzia Mwashterathi,

Shama na Yeieli wana wa Hothamu Mwaroeri,

45 Yediaeli mwana wa Shimri,

nduguye Yoha Mtizi,

46 Elieli Mmahawi,

Yeribai na Yoshavia wana wa Elnaamu,

Ithma Mmoabu,

47 Elieli, na Obedi na Yaasieli Mmesobai.

2 Samweli 5:4–10

4 Daudi alikuwa na miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli miaka arobaini. 5 Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na mitatu.

6 Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.” 7 Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.

8 Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”

9 Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani. 10 Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.

1 Nyakati 11:1–14

1 Israeli yote walimjia Daudi kwa pamoja huko Hebroni wakamwambia, “Sisi ni nyama yako na damu yako. 2 Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani, naye Bwana Mungu wako alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”

3 Wazee wote wa Israeli walipokuwa wamewasili kwa Mfalme Daudi huko Hebroni, alifanya mapatano nao huko Hebroni mbele za Bwana, nao wakamtia Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli, sawasawa na Bwana alivyoahidi kupitia kwa Samweli.

4 Daudi na Waisraeli wote wakaenda Yerusalemu (ndio Yebusi). Nao Wayebusi walioishi humo 5 wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.

6 Daudi alikuwa amesema, “Yeyote aongozaye mashambulizi dhidi ya Wayebusi, atakuwa jemadari mkuu.” Yoabu mwana wa Seruya akawa wa kwanza kukwea, naye akawa mkuu.

7 Daudi akafanya makao yake kwenye ngome, hivyo ukaitwa Mji wa Daudi. 8 Akajenga mji pande zote, kuanzia kwenye mito hadi kwenye ukuta kuzunguka, wakati huo huo Yoabu akajenga sehemu zingine zilizobaki za Yerusalemu. 9 Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu Bwana Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.

10 Hawa ndio waliokuwa wakuu wa mashujaa wa Daudi: wao pamoja na Israeli wote wakauimarisha ufalme wake ili kuenea katika nchi yote, kama Bwana alivyoahidi. 11 Hii ndio orodha ya mashujaa wa Daudi:

Yashobeamu, Mhakmoni, alikuwa mkuu wa maafisa; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300, ambao aliwaua katika pambano moja.

12 Aliyefuata alikuwa Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu. 13 Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-Damimu, wakati Wafilisti walikusanyika huko kwa ajili ya vita. Huko ambapo kulikuwa na shamba lililokuwa limejaa shayiri, vikosi vya Israeli vikawakimbia Wafilisti. 14 Lakini Eleazari na Daudi wakasimama imara katikati ya lile shamba, nao wakalishindania na wakawaua Wafilisti. Naye Bwana akawapa ushindi mkubwa.

2 Samweli 23:18–39

18 Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300 ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. 19 Je, hakupata heshima kubwa zaidi kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.

20 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. 21 Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe. 22 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. 23 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.

24 Miongoni mwa wale Thelathini walikuwepo:

Asaheli ndugu wa Yoabu;

Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu;

25 Shama, Mharodi;

Elika, Mharodi;

26 Helesi, Mpalti;

Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa;

27 Abiezeri kutoka Anathothi;

Mebunai, Mhushathi;

28 Salmoni, Mwahohi;

Maharai, Mnetofathi;

29 Heledi mwana wa Baana, Mnetofathi;

Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini;

30 Benaya Mpirathoni;

Hidai kutoka mabonde ya Gaashi;

31 Abi-Alboni, Mwaribathi;

Azmawethi, Mbarhumi;

32 Eliaba, Mshaalboni;

wana wa Yasheni;

Yonathani 33 mwana wa Shama, Mharari;

Ahiamu mwana wa Sharari, Mharari;

34 Elifeleti mwana wa Ahasbai, Mmaakathi;

Eliamu mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;

35 Hezro, Mkarmeli;

Paarai, Mwarbi;

36 Igali mwana wa Nathani kutoka Soba;

Bani, Mgadi;

37 Seleki, Mwamoni;

Naharai, Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha za Yoabu mwana wa Seruya;

38 Ira, Mwithiri;

Garebu, Mwithiri;

39 na Uria, Mhiti.

Jumla yao wote walikuwa watu thelathini na saba.