Kipindi cha 5: Utawala wa Solomoni

Sehemu ya 1: Utawala wa Solomoni Kabla ya Kuwekwa Wakfu kwa Hekalu

Sadaka ya Solomoni huko Gibeoni na Hukumu Yake

Sadaka ya Solomoni huko Gibeoni. Hukumu ya Solomoni. Kifo cha Adoniya. Hadadi anarudi.

1015 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 2:12

12 Kwa hiyo Solomoni akaketi katika kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana.

2 Nyakati 1:1

1 Solomoni mwana wa Daudi alijiimarisha kwenye milango yote! Katika ufalme wake, kwa kuwa Bwana Mungu wake alikuwa pamoja naye, naye akamfanya mkuu mno.

1 Wafalme 3:3

3 Solomoni akaonyesha upendo wake kwa Bwana kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu.

2 Nyakati 1:2–6

2 Ndipo Solomoni akasema na Israeli wote, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, waamuzi na viongozi wote katika Israeli, pamoja na wakuu wa jamaa. 3 Naye Solomoni na kusanyiko lote wakakwea mpaka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kwa kuwa huko ndiko Hema la Kukutania la Mungu lilipokuwa, ambalo Mose mtumishi wa Bwana alikuwa amelitengeneza huko jangwani. 4 Basi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu mpaka mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu. 5 Lakini yale madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza yalikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani ya Bwana Mungu, hivyo Solomoni na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko. 6 Solomoni akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za Bwana katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu 1,000 za sadaka za kuteketezwa juu yake.

1 Wafalme 3:5–28

5 Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”

6 Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.

7 “Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8 Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9 Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”

10 Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili. 11 Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, 12 nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako. 13 Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14 Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.” 15 Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto.

Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.

16 Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake. 17 Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami. 18 Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili.

19 “Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia. 20 Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu. 21 Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa.”

22 Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.”

Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme.

23 Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ”

24 Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga. 25 Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.”

26 Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!”

Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!”

27 Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimuue; ndiye mama yake.”

28 Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.

2 Nyakati 1:13

13 Ndipo Solomoni akaenda mpaka Yerusalemu kutoka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kutoka mbele ya Hema la Kukutania. Naye akatawala Israeli.

1 Wafalme 2:13–38

13 Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?”

Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” 14 Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.”

Akajibu, “Waweza kulisema.”

15 Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, ufalme umekwenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Bwana. 16 Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.”

Bathsheba akasema, “Waweza kuliomba.”

17 Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Solomoni, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.”

18 Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.”

19 Bathsheba alipokwenda kwa Mfalme Solomoni kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akaketi mkono wake wa kuume.

20 Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.”

Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.”

21 Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.”

22 Mfalme Solomoni akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi, Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Ungeweza pia kuomba ufalme kwa ajili yake, kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa kuhani Abiathari na Yoabu mwana wa Seruya!”

23 Mfalme Solomoni akaapa kwa Bwana, akasema: “Mungu na aniulie mbali, tena bila huruma, ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! 24 Basi sasa, hakika kama Bwana aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” 25 Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.

26 Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la Bwana Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.” 27 Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa Bwana, akilitimiza neno la Bwana alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.

28 Habari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la Bwana na kushika pembe za madhabahu. 29 Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la Bwana naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!”

30 Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la Bwana na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ”

Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.”

Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”

31 Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga. 32 Bwana atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye. 33 Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya Bwana milele.”

34 Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa. 35 Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.

36 Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote. 37 Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”

38 Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.

1 Wafalme 11:21–22

21 Alipokuwa huko Misri, Hadadi alisikia kwamba Daudi amepumzika na baba zake na ya kwamba pia Yoabu aliyekuwa jemadari wa jeshi amekufa. Ndipo Hadadi akamwambia Farao, “Niruhusu niende ili niweze kurudi katika nchi yangu.”

22 Farao akauliza, “Umekosa nini hapa, kwamba unataka kurudi katika nchi yako?”

Hadadi akajibu, “Hakuna, lakini niruhusu niende!”

1 Wafalme 3:4

4 Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia, naye Solomoni akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu.

2 Nyakati 1:7–12

7 Usiku ule Mungu akamtokea Solomoni na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.”

8 Solomoni akamjibu Mungu, “Umemwonyesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake. 9 Sasa, Bwana Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi. 10 Nakuomba unipe mimi hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?”

11 Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, 12 kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”