Solomoni Anajiandaa Kujenga Hekalu

Maandalizi ya kujenga hekalu. Kifo cha Shimei. Ndoa ya Solomoni.

1015 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 4:1–25

1 Basi Mfalme Solomoni akatawala Israeli yote. 2 Hawa ndio waliokuwa maafisa wake wakuu:

Kuhani: Azaria mwana wa Sadoki;

3 Elihorefu na Ahiya, wana wa Shisha: waandishi;

Yehoshafati mwana wa Ahiludi: karani;

4 Benaya mwana wa Yehoyada: jemadari mkuu wa jeshi;

Sadoki na Abiathari: makuhani;

5 Azaria mwana wa Nathani: kiongozi wa maafisa wa wilaya;

Zabudi mwana wa Nathani: kuhani na mshauri binafsi wa mfalme;

6 Ahishari: msimamizi wa jumba la kifalme;

Adoniramu mwana wa Abda: msimamizi wa kazi za kulazimisha.

7 Pia Solomoni alikuwa na watawala kumi na wawili wa wilaya katika Israeli yote, walioleta mahitaji kwa mfalme na kwa watu wa nyumbani kwa mfalme. Kila mmoja alitoa chakula kwa mwezi mmoja katika mwaka. 8 Majina yao ni haya:

Ben-Huri: katika nchi ya vilima ya Efraimu;

9 Ben-Dekeri: katika Makasi, Shaalbimu, Beth-Shemeshi na Elon-Bethhanani;

10 Ben-Hesedi: katika Arubothi (Soko na nchi yote ya Heferi zilikuwa zake);

11 Ben-Abinadabu: katika Nafoth-Dori (alimwoa Tafathi binti Solomoni);

12 Baana mwana wa Ahiludi: katika Taanaki na Megido, na katika Beth-Shani yote karibu na Sarethani chini ya Yezreeli, kuanzia Beth-Shani hadi Abel-Mehola kupita hadi Yokmeamu;

13 Ben-Geberi: katika Ramoth-Gileadi (makao ya Yairi mwana wa Manase katika Gileadi ilikuwa miji yake, pamoja na wilaya ya Argobu katika Bashani na miji yake mikubwa sitini yenye kuzungukwa na kuta zenye makomeo ya shaba);

14 Ahinadabu mwana wa Ido: katika Mahanaimu;

15 Ahimaasi: katika Naftali (alikuwa amemwoa Basemathi binti Solomoni);

16 Baana mwana wa Hushai: katika Asheri na katika Bealothi;

17 Yehoshafati mwana wa Parua: katika Isakari;

18 Shimei mwana wa Ela: katika Benyamini;

19 Geberi mwana wa Uri: katika Gileadi (nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani). Naye alikuwa ndiye mtawala pekee katika eneo hilo.

20 Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi. 21 Mfalme Solomoni akatawala katika falme zote kuanzia Mto Frati hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Solomoni, siku zote za maisha yake.

22 Mahitaji ya Solomoni ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida. 23 Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. 24 Kwa kuwa Solomoni alitawala falme zote magharibi ya mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. 25 Wakati wa maisha ya Solomoni Yuda na Israeli, kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba, wakaishi salama kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.

2 Nyakati 2:1–2

1 Solomoni akatoa amri kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe. 2 Solomoni akaandika watu 70,000 kuwa wachukuzi wa mizigo, na watu 80,000 kuwa wachonga mawe vilimani, na watu 3,600 kuwa wasimamizi wao.

1 Wafalme 5:1–12

1 Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kuwa Solomoni ametiwa mafuta awe mfalme mahali pa Daudi baba yake, akatuma wajumbe kwa Solomoni, kwa sababu Hiramu siku zote alikuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na Daudi. 2 Solomoni akapeleka ujumbe huu kwa Hiramu:

3 “Unajua kwamba kwa sababu ya vita vilivyopiganwa dhidi ya baba yangu Daudi kutoka pande zote, hakuweza kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wake, hadi Bwana alipowaweka adui zake chini ya miguu yake. 4 Lakini sasa Bwana Mungu wangu amenipa utulivu kila upande hakuna adui wala maafa. 5 Kwa hiyo, ninakusudia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana, Mungu wangu, kama Bwana alivyomwambia baba yangu Daudi, wakati aliposema, ‘Mwanao nitakayemweka kwenye kiti cha ufalme mahali pako, ndiye atajenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’

6 “Hivyo toa amri ili mierezi ya Lebanoni ikatwe kwa ajili yangu. Watu wangu watafanya kazi na watu wako, nami nitawalipa watu wako kwa ujira wowote utakaoupanga. Unajua kwamba hatuna mtu yeyote mwenye ustadi katika kukata miti kama Wasidoni.”

7 Hiramu aliposikia ujumbe wa Solomoni, akafurahishwa sana akasema, “Ahimidiwe Bwana leo, kwa kuwa amempa Daudi mwana mwenye hekima kutawala juu ya taifa hili kubwa.”

8 Hiramu akatuma neno kwa Solomoni:

“Nimepokea ujumbe ulionipelekea na nitafanya yote unayohitaji katika kukupatia magogo ya mierezi na misunobari. 9 Watu wangu watayakokota kutoka Lebanoni hadi kwenye bahari, nami nitayafunga mafungu mafungu yaelee juu ya maji hadi utakapoelekeza. Huko nitayatenganisha, nawe utaweza kuyachukua. Wewe utakidhi haja yangu kwa kunipatia chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.”

10 Kwa njia hii Hiramu akampa Solomoni miti yote ya mierezi na magogo ya misunobari kama alivyohitaji, 11 naye Solomoni akampa Hiramu kori 20,000 za ngano kama chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, pamoja na mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa bathi 20,000. Solomoni aliendelea kumfanyia Hiramu hivyo mwaka baada ya mwaka. 12 Bwana akampa Solomoni hekima, kama alivyomwahidi. Palikuwepo na uhusiano wa amani kati ya Hiramu na Solomoni, na wote wawili wakafanya mkataba.

2 Nyakati 2:3–16

3 Solomoni akapeleka ujumbe huu kwa Mfalme Hiramu wa Tiro:

“Unitumie magogo ya mierezi kama ulivyomfanyia baba yangu Daudi wakati ulipompelekea mierezi ya kujenga jumba lake la kifalme la kuishi. 4 Sasa ninakaribia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wangu na kuliweka wakfu kwake kwa ajili ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri mbele zake, mahali pa kuweka mikate ya Wonyesho kwa kufuata utaratibu na kwa ajili ya mahali pa kutolea sadaka za kuteketezwa kila siku asubuhi na jioni, siku za Sabato na Mwezi Mwandamo pia katika sikukuu zilizoamriwa za Bwana Mungu wetu. Hili ni agizo la kudumu kwa ajili ya Waisraeli.

5 “Hekalu nitakalolijenga litakuwa kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu mingine yote. 6 Lakini ni nani awezaye kumjengea Hekalu, maadamu mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kumtosha? Mimi ni nani basi hata nimjengee Hekalu, isipokuwa liwe tu mahali pa kutolea dhabihu za kuteketezwa mbele zake?

7 “Hivyo basi nitumie mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi ya kutengeneza dhahabu na fedha, shaba na chuma, nyuzi za rangi ya zambarau, nyekundu na buluu, mwenye uzoefu wa kutia nakshi, ili afanye kazi Yuda na Yerusalemu pamoja na mafundi wangu wenye ustadi, ambao baba yangu Daudi aliwaweka.

8 “Pia nitumie magogo ya mierezi, miberoshi na misandali kutoka Lebanoni kwa maana najua kwamba watu wako wanao ujuzi wa kupasua mbao huko. Watu wangu watafanya kazi pamoja na watu wako 9 ili wanipatie mbao kwa wingi kwa sababu Hekalu nitakalojenga lazima liwe kubwa na zuri kabisa. 10 Nitawapa watumishi wako, yaani, maseremala wakatao mbao, kori 20,000 za unga wa ngano, kori 20,000 za shayiri, bathi 20,000 za mvinyo, na bathi 20,000 za mafuta ya zeituni.”

11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akamjibu Solomoni kwa barua:

“Kwa sababu Bwana anawapenda watu wake, amekufanya wewe kuwa mfalme wao.”

12 Naye Hiramu akaongeza kusema:

“Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli aliyezifanya mbingu na nchi! Amempa Mfalme Daudi mwana mwenye hekima, aliyejaliwa maarifa na ufahamu, ambaye atajenga Hekalu kwa ajili ya Bwana, na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe.

13 “Mimi nitamtuma kwako Huramu-Abi, mtu mwenye ustadi mwingi, 14 ambaye mama yake alitoka Dani na baba yake alitoka Tiro. Yeye ni stadi wa kutengeneza vitu, kufanya kazi zote za dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe na mbao pamoja na kufuma. Ni stadi katika kutia rangi ya zambarau, buluu, nyekundu na nguo za kitani safi. Yeye ana ujuzi katika aina zote za kutia nakshi na anaweza kufuatiliza mchoro wowote wa kazi anayopewa. Atafanya kazi na mafundi wako na wale wa bwana wangu, Daudi baba yako.

15 “Sasa basi bwana wangu na awapelekee watumishi wake ngano, shayiri, mafuta ya zeituni na mvinyo kama alivyoahidi, 16 nasi tutakata magogo yote yale unayohitaji kutoka Lebanoni nasi tutayafunga pamoja na kuyaweka yaelee baharini mpaka Yafa. Kisha utaweza kuyachukua mpaka Yerusalemu.”

1 Wafalme 5:13–18

13 Mfalme Solomoni akakusanya wafanyakazi 30,000 kutoka Israeli yote. 14 Akawapeleka Lebanoni kwa zamu za watu 10,000 kwa mwezi, hivyo walikaa Lebanoni kwa mwezi mmoja na miezi miwili nyumbani. Adoniramu ndiye alikuwa kiongozi wa shokoa. 15 Solomoni alikuwa na wachukuzi wa mizigo 70,000 na wachonga mawe 80,000 huko vilimani, 16 pamoja na wasimamizi 3,300 ambao walisimamia kazi hiyo na kuwaongoza wafanyakazi. 17 Kwa amri ya mfalme walitoa kwenye machimbo ya mawe, mawe makubwa, yaliyo bora kwa kujengea msingi wa nyumba yaliyochongwa kwa ajili ya Hekalu. 18 Mafundi wa Solomoni, wa Hiramu na watu wa Gebali walikata na kuandaa mbao na mawe kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu.

2 Nyakati 2:17–18

17 Ndipo Solomoni akaamuru ifanyike hesabu ya wageni wote waliokuwa katika Israeli, baada ya ile hesabu iliyofanywa na Daudi; wakapatikana watu 153,600. 18 Akawaweka watu 70,000 miongoni mwao kuwa wachukuzi wa mizigo, na 80,000 kuwa wachonga mawe vilimani, na 3,600 wakiwa wasimamizi juu yao ili wawahimize watu kufanya kazi.

Kifo cha Shimei 1011 KK

1 Wafalme 2:39–46

39 Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.” 40 Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.

41 Solomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi, 42 mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa Bwana na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’ 43 Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa Bwana na kutii amri niliyokupa?”

44 Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa Bwana atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda. 45 Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele za Bwana milele.”

46 Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumuua.

Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.

Ndoa ya Solomoni

1 Wafalme 3:1–2

1 Solomoni akafanya urafiki na Mfalme Farao wa Misri na kumwoa binti yake. Akamleta huyo binti katika Mji wa Daudi mpaka alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Bwana, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu. 2 Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye vilima, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Bwana.