Sehemu ya 2: Ujenzi wa Hekalu
1011 hadi 1005 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Ndipo Solomoni akaanza kujenga Hekalu la Bwana katika Yerusalemu juu ya Mlima Moria, pale ambapo Bwana alikuwa amemtokea Daudi baba yake. Ilikuwa katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi, mahali palipotolewa na Daudi.
1 Katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, ambao ndio mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Bwana.
2 Alianza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa utawala wake.
3 Msingi aliouweka Solomoni kwa ajili ya kulijenga Hekalu la Mungu ulikuwa urefu wa dhiraa sitini na upana dhiraa ishirini. 4 Ukumbi wa mbele wa Hekalu ulikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, yaani, kuanzia upande mmoja hadi upande mwingine wa upana wa nyumba hiyo na kimo chake dhiraa thelathini.
Akaufunika ndani kwa dhahabu safi. 5 Akaufunika ukumbi mkuu kwa mbao za miberoshi na kufunikwa kwa dhahabu safi na kuupamba kwa miti ya mitende na kuifanyizia kwa minyororo. 6 Alilipamba Hekalu kwa vito vya thamani. Hiyo dhahabu aliyotumia ilikuwa dhahabu ya Parvaimu. 7 Akazifunika boriti za dari, miimo na vizingiti vya milango, kuta na milango ya Hekalu kwa dhahabu, naye akatia nakshi ya makerubi kwenye kuta.
8 Akajenga Patakatifu pa Patakatifu, urefu na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini, sawasawa na upana wa Hekalu. Alifunika ndani kwa talanta 120 za dhahabu safi. 9 Misumari ya dhahabu ilikuwa na uzito wa shekeli hamsini. Alivifunika pia vyumba vya juu kwa dhahabu.
4 Akatengeneza madirisha membamba yenye vidirisha vidogo vya juu katika Hekalu. 5 Akafanyiza vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote vikishikamana na kuta za Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu. 6 Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano, ya kati ilikuwa dhiraa sita na ya tatu ilikuwa dhiraa saba. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.
7 Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika sauti yake katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.
8 Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu, ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutokea hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu.
15 Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mierezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari. 16 Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mierezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu. 17 Ukumbi mkubwa uliokuwa mbele ya chumba hiki ndio ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini. 18 Hekalu ndani ilikuwa ya mierezi iliyonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi, hakuna jiwe ambalo lilionekana.
19 Ndani ya Hekalu akatengeneza sehemu takatifu ya ndani, kwa ajili ya kuweka Sanduku la Agano la Bwana. 20 Sehemu takatifu ya ndani ilikuwa na upana, urefu na kimo cha dhiraa ishirini ndani kwa ndani. Akaifunika ndani kwa dhahabu safi, pia akaifunika madhabahu ya mierezi vivyo hivyo. 21 Solomoni akaifunika sehemu ya ndani ya Hekalu kwa dhahabu safi, naye akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande moja hadi ule mwingine mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, ambako palifunikwa kwa dhahabu. 22 Basi akafunika sehemu yote ya ndani kwa dhahabu. Pia akafunika madhabahu yale yaliyokuwa ndani ya Patakatifu pa Patakatifu kwa dhahabu.
23 Katika Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi kwenda juu. 24 Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. 25 Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, hivyo makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. 26 Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. 27 Aliwaweka makerubi hao ndani ya Patakatifu pa Patakatifu pa Hekalu, mabawa yake yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. 28 Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.
13 Mabawa ya makerubi hawa yalitanda dhiraa ishirini. Walisimama kwa miguu yao, nyuso zao zikielekea ukumbi mkubwa.
14 Akatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na za kitani safi, na kutarizi makerubi juu yake.
29 Juu ya kuta zote zilizozunguka Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi zilizokatwa za makerubi, miti ya mitende na maua yaliyochanua. 30 Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu.
31 Kwa ingilio la Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza milango ya mbao za mzeituni, zikiwa na miimo na vizingiti vyenye umbo la pembe tano. 32 Juu ya milango miwili ya mbao za mzeituni alinakshi makerubi, miti ya mitende pamoja na maua yaliyochanua na kufunika makerubi na miti ya mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. 33 Kwa njia iyo hiyo akatengeneza miimo yenye pande nne ya miti ya mizeituni, kwa ajili ya ingilio la ukumbi mkubwa. 34 Kulikuwa na milango miwili iliyoweza kukunjuka iliyotengenezwa kwa mbao za msunobari na kila mmoja ulikuwa na bawaba ambazo zingeuwezesha kujikunja kila kipande juu ya kingine. 35 Akanakshi makerubi, miti ya mitende na maua yaliyochanua juu yake na kufunika kwa dhahabu iliyonyooshwa vizuri juu ya michoro.
36 Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa na safu moja ya boriti za mierezi zilizorembwa.
13 Mfalme Solomoni akatuma watu Tiro kumleta Hiramu, 14 ambaye mama yake alikuwa mjane kutoka kabila la Naftali na baba yake alikuwa mtu wa Tiro tena fundi wa shaba. Hiramu alikuwa na ustadi wa hali ya juu na mzoefu katika aina zote za kazi ya shaba. Alikuja kwa Mfalme Solomoni na kufanya kazi zake zote alizopangiwa.
15 Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kila nguzo ikiwa na mzingo wa dhiraa kumi na mbili kwa mstari. 16 Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tano kwenda juu. 17 Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji. 18 Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo. 19 Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne 20 Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga 200 katika safu kuzunguka pande zote. 21 Hiramu akasimamisha nguzo kwenye baraza ya Hekalu. Nguzo ya upande wa kusini akaiita Yakini, na ile ya upande wa kaskazini Boazi. 22 Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika.
1 Mfalme Solomoni akatengeneza madhabahu ya shaba yenye urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini na kimo chake dhiraa kumi.
23 Hiramu akasubu Bahari ya chuma, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kimo cha dhiraa tano. Mzunguko wake ulikuwa dhiraa thelathini. 24 Chini ya ukingo, ilizungukwa na maboga, kumi kwenye kila dhiraa moja. Maboga yalikuwa yamesubiwa katika safu mbili ili kuwa kitu kimoja na hiyo bahari.
25 Bahari iliwekwa juu ya mafahali kumi na wawili, watatu wakielekea kaskazini, watatu wakielekea magharibi, watatu wakielekea kusini na watatu wakielekea mashariki. Bahari iliwekwa juu yao na sehemu zao za nyuma zilielekeana. 26 Ilikuwa na unene wa nyanda nne na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi iliyochanua. Iliweza kuchukua bathi 2,000.
27 Pia akatengeneza vitako kumi vya shaba vinavyoweza kuhamishika, kila kimoja kilikuwa na urefu wa dhiraa nne, upana dhiraa nne na kimo chake dhiraa tatu 28 Hivi ndivyo vile vitako vilivyotengenezwa: Vilikuwa na mbao za pembeni zilizoshikamanishwa na mihimili. 29 Juu ya mbao kati ya hiyo mihimili kulikuwa na simba, mafahali na makerubi, pia kwenye mihimili yake. Juu na chini ya simba na mafahali kulikuwa kumesokotewa taji za kufuliwa. 30 Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungusha hayo magurudumu na kila kimoja kilikuwa na sinia kwenye vishikizo vinne vya taji iliyosubiwa kila upande. 31 Ndani ya kitako kulikuwa na nafasi ya wazi iliyokuwa na umbile la mviringo lenye kina cha dhiraa moja. Nafasi hii ya wazi ilikuwa ya mviringo, pamoja na kitako chake ilikuwa dhiraa moja na nusu. Kuzunguka huo mdomo wake kulitiwa nakshi. Papi za vitako zilikuwa mraba na si za mviringo. 32 Magurudumu manne yalikuwa chini ya papi, na vyuma vya katikati vya kuzungushia magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa kwenye kitako. Kipenyo cha kila gurudumu kilikuwa dhiraa moja na nusu. 33 Magurudumu yalitengenezwa kama ya magari ya vita ya kukokotwa, vyuma vya katikati vya magurudumu, duara zake, matindi yake na vikombe vyake vyote vilikuwa vya kusubu.
34 Kila kitako kilikuwa na mikono minne, moja kwenye kila pembe, ukitokeza kutoka kwenye kitako. 35 Juu ya kitako kulikuwepo na utepe wa mviringo wenye kina cha nusu dhiraa. Vishikio na papi vilishikamana upande wa juu wa kitako. 36 Alitia nakshi za makerubi, simba na miti ya mitende juu ya uso wa vishikio na juu ya papi, katika kila nafasi iliyopatikana, pamoja na mataji yaliyosokotwa kuzunguka pande zote. 37 Hivi ndivyo Hiramu alivyotengeneza vile vitako kumi. Vyote vilikuwa vya kusubu kwenye kalibu za kufanana kwa vipimo na kwa umbo.
38 Kisha akatengeneza masinia kumi ya shaba, kila moja likiwa na ujazo wa bathi arobaini, yakiwa na kipenyo cha dhiraa nne kila sinia moja kwa kila kimoja ya vile vitako kumi. 39 Aliweka vitako vitano upande wa kusini wa Hekalu na vingine vitano upande wa kaskazini. Akaweka ile bahari upande wa kusini, katika pembe ya kusini ya Hekalu. 40 Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.
Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi zote katika Hekalu la Bwana kama vile Mfalme Solomoni alikuwa amemwagiza, yaani:
41 nguzo mbili;
mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;
nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;
42 makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);
43 vitako kumi pamoja na masinia yake kumi;
44 ile Bahari ya chuma na yale mafahali kumi na wawili chini yake;
45 masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.
Vyombo hivi vyote ambavyo Huramu alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu la Bwana vilikuwa vya shaba iliyongʼarishwa. 46 Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani. 47 Solomoni akaviacha vitu hivi vyote bila kupima uzani wake, kwa sababu vilikuwa vingi sana hivi kwamba uzito wa shaba haungekadirika.
48 Solomoni pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana:
madhabahu ya dhahabu;
meza ya dhahabu za kuweka mikate ya Wonyesho;
49 vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya Patakatifu pa Patakatifu);
kazi ya maua ya dhahabu na taa na makoleo;
50 masinia ya dhahabu safi, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo;
na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu.
8 Akatengeneza meza kumi na kuziweka hekaluni, tano upande wa kusini na tano upande wa kaskazini. Pia akatengeneza mabakuli 100 ya dhahabu ya kunyunyizia.
9 Akatengeneza ukumbi wa makuhani na ukumbi mwingine mkubwa na milango yake, naye akaifunika hiyo milango kwa shaba. 10 Akaweka ile Bahari upande wa kusini, kwenye pembe ya kusini mashariki ya nyumba.
9 Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mierezi. 10 Mfalme Solomoni akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mierezi.
11 Neno la Bwana likamjia Solomoni kusema: 12 “Kwa habari ya Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, kwa kupitia wewe nitatimiza ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. 13 Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”
14 Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha.
51 Hivyo Mfalme Solomoni alipomaliza kazi ya Hekalu la Bwana, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Bwana.
37 Msingi wa Hekalu la Bwana uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa tano. 38 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Solomoni. Alilijenga kwa miaka saba.
2 Hekalu hilo Mfalme Solomoni alilojenga kwa ajili ya Bwana lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini, upana wa dhiraa ishirini na kimo cha dhiraa thelathini kwenda juu. 3 Baraza ya mbele ya Hekalu ilienea dhiraa ishirini kulingana na upana wa Hekalu na kujitokeza dhiraa kumi mbele ya Hekalu.
10 Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akafanyiza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu. 11 Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano, nalo liligusa ukuta wa Hekalu, bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi lingine. 12 Vivyo hivyo bawa moja la kerubi wa pili lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na liligusa ukuta mwingine wa pili wa Hekalu na bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano nalo liligusa bawa la kerubi wa kwanza.
15 Mbele ya Hekalu Solomoni akatengeneza nguzo mbili, ambazo kwa pamoja zilikuwa na dhiraa thelathini na tano kwenda juu kwake, na urefu wa kila moja ilikuwa na taji juu yake yenye dhiraa tano. 16 Akatengeneza minyororo iliyosokotwa, na kuiweka juu ya zile nguzo. Pia akatengeneza makomamanga 100, na kuyashikamanisha kwenye minyororo. 17 Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya Hekalu, moja upande wa kusini na nyingine upande wa kaskazini. Ile moja ya upande wa kusini akaiita Yakini, na ya upande wa kaskazini akaiita Boazi.
2 Akatengeneza Bahari ya kusubu, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kimo cha dhiraa tano. Kamba ya urefu wa dhiraa thelathini ingeweza kuizunguka. 3 Chini ya huo ukingo, kulikuwa na mafahali kuizunguka, yaani mafahali kumi katika kila dhiraa moja. Hayo mafahali waliyasubu katika safu mbili yakiwa ya kitu kimoja na hiyo Bahari.
4 Bahari hiyo ilikaa juu ya mafahali kumi na wawili, mafahali watatu walielekeza nyuso zao kaskazini, watatu magharibi, watatu kusini na watatu mashariki. Bahari hiyo ilikaa juu ya hao mafahali, nazo sehemu zao za nyuma zilielekeana. 5 Unene wake ulikuwa nyanda nne, na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi iliyochanua. Iliweza kuchukua bathi 3,000.
6 Kisha akatengeneza masinia kumi kwa ajili ya kuoshea vifaa, naye akayaweka matano upande wa kusini na matano upande wa kaskazini. Ndani yake ndimo walioshea vifaa vya kutumika katika sadaka za kuteketezwa, lakini ile Bahari ilikuwa ni kwa ajili ya makuhani kunawia.
7 Akatengeneza vinara vya taa kumi vya dhahabu kama ilivyoainishwa kwao na kuviweka hekaluni, vinara vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini.
11 Pia akatengeneza masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.
Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi katika Hekalu la Mungu kama vile Mfalme Solomoni alikuwa amemwagiza, yaani:
12 zile nguzo mbili;
yale mataji mawili yaliyokuwa juu ya hizo nguzo,
zile nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli yaliyowekwa juu ya zile nguzo;
13 yale makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);
14 vishikio pamoja na masinia yake;
15 hiyo Bahari na hao mafahali kumi na wawili chini yake;
16 pia hayo masufuria, masepetu, uma za nyama na vyombo vingine vyote vilivyohusiana.
Vitu vyote ambavyo Huramu-Abi alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu la Bwana vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa. 17 Mfalme aliagiza wavisubu vitu hivi kwenye kalibu za udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani kati ya Sukothi na Sereda. 18 Vitu hivi vyote Mfalme Solomoni alivyotengeneza vilikuwa vingi sana hivi kwamba uzito wa shaba haungekadirika.
19 Solomoni pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu:
madhabahu ya dhahabu;
meza za kuweka mikate ya Wonyesho;
20 vinara vya taa vya dhahabu safi pamoja na taa zake ili ziwake mbele ya sehemu takatifu ya ndani kama ilivyoelekezwa;
21 maua ya dhahabu yaliyofanyizwa, taa na makoleo (vilikuwa vya dhahabu bora kabisa);
22 mikasi ya dhahabu safi, mabakuli ya kunyunyizia, masinia na vyetezo; milango ya dhahabu ya Hekalu: yaani milango ya ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, na milango ya ukumbi mkuu.