Maagizo ya Daudi kwa Solomoni
1015 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.
2 Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, 3 shika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, 4 ili kwamba Bwana aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’
5 “Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. 6 Shughulika naye kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani.
7 “Lakini uwaonyeshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu.
8 “Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, ambaye alinilaani kwa laana kali siku niliyokwenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa Bwana: ‘Sitakuua kwa upanga!’ 9 Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.”
Maneno ya Mwisho ya Daudi
1 Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi:
“Neno la Daudi mwana wa Yese,
neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana,
mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo,
mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:
2 “Roho wa Bwana alinena kupitia kwangu,
neno lake lilikuwa ulimini mwangu.
3 Mungu wa Israeli alinena,
mwamba wa Israeli akaniambia:
‘Mtu anatawala watu kwa haki,
wakati anapotawala
akiwa na hofu ya Mungu,
4 yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo
asubuhi isiyo na mawingu,
kama mwanga baada ya mvua
uchipuzao majani kutoka ardhini.’
5 “Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu
mbele za Mungu?
Je, hajafanya Agano la milele nami,
lililopangwa na kuimarishwa
kila sehemu?
Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu
na kunijalia matakwa yangu yote?
6 Lakini watu waovu wote
watatupwa kando kama miiba,
ambayo haikusanywi kwa mkono.
7 Yeyote agusaye miiba
hutumia chombo cha chuma
au mpini wa mkuki,
nayo huchomwa pale ilipo.”
Kifo cha Daudi
26 Daudi mwana wa Yese alikuwa mfalme wa Israeli yote. 27 Alitawala Israeli kwa miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.
28 Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Solomoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
29 Kuhusu matukio ya utawala wa Mfalme Daudi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kumbukumbu za mwonaji Samweli, na kumbukumbu za nabii Nathani na kumbukumbu za mwonaji Gadi, 30 pamoja na habari zote za utawala wake, nguvu zake na matukio yaliyompata yeye, na Israeli, na falme za nchi nyingine zote.
10 Kisha Daudi akapumzika pamoja na baba zake naye akazikwa katika Mji wa Daudi. 11 Daudi alikuwa ametawala juu ya Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.