Sehemu ya 6: Utawala wa Sauli

Sauli Anafanywa Mfalme wa Israeli

1095 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Samweli 9–10

1 Kulikuwako Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini. 2 Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana anayevutia sana, hakuwepo aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli, alikuwa mrefu kuliko wengine wote.

3 Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.” 4 Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwepo huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata.

5 Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo, sisi na turudi, au baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda na kuanza kufadhaika kutuhusu sisi.”

6 Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho hutokea kweli. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.”

7 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Kama tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?”

8 Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli. Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia twende kwa njia ipi.” 9 (Zamani katika Israeli, kama mtu alikwenda kuuliza neno kwa Mungu, angalisema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.)

10 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwepo huyo mtu wa Mungu.

11 Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wanakuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?”

12 Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu. 13 Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula. Watu hawataanza kula mpaka atakapofika kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”

14 Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikokwenda mahali pa juu.

15 Basi siku moja kabla Sauli hajaja, Bwana alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili: 16 “Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umtie mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli, ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”

17 Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”

18 Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, waweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”

19 Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu mpaka mahali pa juu, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako. 20 Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”

21 Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo la namna hiyo?”

22 Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ndani ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini. 23 Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.”

24 Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’ ” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile.

25 Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake. 26 Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja. 27 Hata walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Lakini subiri hapa kwa kitambo kidogo, ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.”

10:1 Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, Bwana hakukutia mafuta uwe kiongozi juu ya watu wake Israeli? 2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’

3 “Kisha utakwenda mbele kutoka hapa mpaka uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwa Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai. 4 Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao.

5 “Baada ya hayo utakwenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii. 6 Roho wa Bwana atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. 7 Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.

8 “Tangulia kushuka mbele yangu mpaka Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.”

9 Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile. 10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao. 11 Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”

12 Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?” 13 Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alikwenda mahali pa juu.

14 Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?”

Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulikwenda kwa Samweli.”

15 Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.”

16 Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme.

17 Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa Bwana huko Mispa, 18 naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowaonea.’ 19 Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za Bwana kwa kabila zenu na kwa koo zenu.”

20 Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa. 21 Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana. 22 Wakazidi kuuliza kwa Bwana, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?”

Naye Bwana akasema, “Ndiyo, amejificha katikati ya mizigo.”

23 Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama katikati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote. 24 Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye Bwana amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.”

Ndipo watu wakapiga kelele, wakasema, “Mfalme na aishi maisha marefu.”

25 Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kuweka mbele za Bwana. Kisha Samweli akawaruhusu watu, kila mmoja aende nyumbani kwake.

26 Sauli pia akaenda nyumbani kwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao. 27 Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akanyamaza kimya.