Samweli Anaitawala Israeli

1116 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Samweli 7:2–8:22

2 Sanduku la Bwana lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, yaani jumla ya miaka ishirini, nao watu wa Israeli wakaomboleza na kumtafuta Bwana. 3 Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi na kujitoa wenyewe kwa Bwana na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi na mkono wa Wafilisti.” 4 Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi, nao wakamtumikia Bwana peke yake.

5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.” 6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Bwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa.

7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. 8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” 9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Akamlilia Bwana kwa niaba ya Israeli, naye Bwana akamjibu.

10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Bwana alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli. 11 Watu wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.

12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri, akisema, “Hata sasa Bwana ametusaidia.” 13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena.

Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya Wafilisti. 14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ile ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawepo amani kati ya Israeli na Waamori.

15 Samweli akaendelea kama mwamuzi juu ya Israeli siku zote za maisha yake. 16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli mpaka Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote. 17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani kwake, huko pia aliwaamua Israeli. Naye huko alimjengea Bwana madhabahu.

8:1 Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli. 2 Mzaliwa wa kwanza alikuwa Yoeli, na la wa pili lilikuwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba. 3 Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.

4 Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama. 5 Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”

6 Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba Bwana. 7 Naye Bwana akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao. 8 Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri mpaka siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe. 9 Sasa wasikilize, lakini waonye kwa makini na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”

10 Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Bwana. 11 Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. 12 Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake. 13 Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji. 14 Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. 15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. 16 Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. 17 Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. 18 Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye Bwana hatawajibu.”

19 Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala. 20 Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”

21 Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za Bwana. 22 Bwana akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.”

Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”