Vita vya Sauli

1095 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Samweli 11–13

1 Nahashi yule Mwamoni, akakwea kuuzunguka kwa jeshi mji wa Yabeshi-Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba na sisi, na tutakuwa chini yako.”

2 Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitangʼoa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.”

3 Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote, kama hakuna hata mmoja anayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.”

4 Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa juu ya masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa. 5 Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza jinsi watu wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.

6 Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira. 7 Akachukua jozi ya maksai na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha hofu ya Bwana ikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja. 8 Sauli alipowakusanya huko Bezeki, watu wa Israeli walikuwa 300,000 na watu wa Yuda 30,000.

9 Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni watu wa Yabeshi-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’ ” Wajumbe walipokwenda na kutoa taarifa hii kwa watu wa Yabeshi, wakafurahi. 10 Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.”

11 Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja mpaka mchana. Wale walionusurika wakasambaa, kiasi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja.

12 Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatawala juu yetu?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.”

13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii Bwana ameokoa Israeli.”

14 Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.” 15 Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele za Bwana. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Bwana, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa.

12:1 Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu. 2 Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini kwa habari yangu mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu mpaka siku hii ya leo. 3 Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni juu yangu mbele za Bwana na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Ni nani nimepata kumwonea? Ni kutoka kwenye mkono wa nani nimepokea rushwa ili kunifanya nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, mimi nitawarudishia.”

4 Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutuonea. Hujapokea chochote kutoka kwenye mkono wa mtu awaye yote.”

5 Samweli akawaambia, “Bwana ni shahidi juu yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.”

Wakasema, “Yeye ni shahidi.”

6 Kisha Samweli akawaambia watu, “Bwana ndiye alimchagua Mose na Aroni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri. 7 Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za Bwana wa matendo yote ya haki yaliyofanywa na Bwana kwenu na kwa baba zenu.

8 “Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia Bwana kwa ajili ya msaada, naye Bwana akawatuma Mose na Aroni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.

9 “Lakini wakamsahau Bwana Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao. 10 Wakamlilia Bwana na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha Bwana na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’ 11 Ndipo Bwana akawatuma Yerub-Baali, Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.

12 “Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa Bwana Mungu wenu alikuwa mfalme wenu. 13 Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, Bwana amemweka mfalme juu yenu. 14 Kama mkimcha Bwana na kumtumikia na kumtii nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayetawala juu yenu mkimfuata Bwana, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu! 15 Lakini kama hamkumtii Bwana, nanyi kama mkiasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.

16 “Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Bwana anakwenda kulifanya mbele ya macho yenu! 17 Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Bwana mlipoomba mfalme.”

18 Kisha Samweli akamwomba Bwana, na siku ile ile Bwana akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Bwana na Samweli.

19 Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”

20 Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa moyo wenu wote. 21 Msigeukie sanamu zisizofaa. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana. 22 Kwa ajili ya jina lake kuu Bwana hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza Bwana kuwafanya kuwa wake mwenyewe. 23 Kwa habari yangu, iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya Bwana kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na ya kunyooka. 24 Lakini hakikisheni mnamcha Bwana na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu. 25 Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!”

13:1 Sauli alikuwa na miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na miwili.

2 Sauli alichagua watu 3,000 kutoka Israeli; miongoni mwa hao watu 2,000 walikuwa pamoja naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli, nao watu 1,000 walikuwa pamoja na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao.

3 Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!” 4 Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, nao sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali.

5 Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita 3,000, waendesha magari ya vita 6,000 na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki ya Beth-Aveni. 6 Watu wa Israeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katikati ya miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki. 7 Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani mpaka nchi ya Gadi na Gileadi.

Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu. 8 Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika. 9 Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa. 10 Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki.

11 Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?”

Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi, 12 nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa Bwana.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.”

13 Samweli akasema, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya Bwana Mungu wako aliyokupa. Kama ungelitii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote. 14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya Bwana.”

15 Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu 600.

16 Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi. 17 Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali, 18 kikosi kingine kilielekea Beth-Horoni, nacho kikosi cha tatu kilielekea kwenye nchi ya mpakani ielekeayo Bonde la Seboimu linalotazamana na jangwa.

19 Hapakuwa na mhunzi ambaye angeweza kupatikana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walikuwa wamesema, “Waebrania wasije wakatengeneza panga au mikuki!” 20 Hivyo Waisraeli wote huteremka kwa Wafilisti ili kunoa majembe ya plau, majembe ya mkono, mashoka na miundu. 21 Bei ilikuwa fedha theluthi mbili za shekeli kunoa majembe ya plau na majembe ya mkono, na theluthi moja ya shekeli kwa nyuma, mashoka na michokoo.

22 Kwa hiyo siku ya vita hakuna askari yeyote aliyekuwa kambini na Sauli na Yonathani ambaye alikuwa na upanga wala mkuki mkononi mwake; Sauli tu na mwanawe Yonathani ndio waliokuwa navyo.

23 Basi kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimetoka kuelekea njia iendayo Mikmashi.