Paulo Awaandikia Wakorintho
Paulo anawaandikia Wakorintho barua yake ya kwanza ili kuthibitisha mamlaka yake kama mtume, kukemea mwenendo usiofaa na ukosefu wa utaratibu kanisani, na kujibu maswali ya waongofu kuhusu mambo mbalimbali ya mafundisho na nidhamu.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Paulo Awasalimu Wakorintho
Utangulizi wa Paulo, ambamo anathibitisha utume wake na umoja wa wale wanaomwamini Kristo Yesu.
1 Paulo, niliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Kristo Yesu, na Sosthene ndugu yetu.
2 Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu na walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:
3 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.
Paulo Afurahia Kuongoka Kwao na Karama Zao
Paulo anafurahia kuongoka kwao na karama za kiroho walizopokea kuwa ushuhuda wa ukweli wa Kristo.
4 Ninamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu kwa sababu ya neema yake mliyopewa katika Kristo Yesu. 5 Kwa kuwa katika Kristo mmetajirishwa kwa kila hali, katika kusema kwenu na katika maarifa yenu yote, 6 kwa sababu ushuhuda wetu kumhusu Kristo ulithibitishwa ndani yenu. 7 Kwa hiyo hamkupungukiwa na karama yoyote ya kiroho wakati mnangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. 8 Atawafanya imara mpaka mwisho, ili msiwe na hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu ni mwaminifu.
Paulo Ahimiza Umoja, Si Makundi
Paulo anawahimiza wawe na umoja katika jina la Yesu Kristo, ambaye ndani yake hakukuwa na mgawanyiko, badala ya kuwafuata viongozi ambao majina yao waliyatumia kujitambulisha kama wafuasi wao.
10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. 11 Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu. 12 Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.”
13 Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? 14 Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo. 15 Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu. 16 (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana. Lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.) 17 Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.
Msalaba Wazidi Hekima ya Wanadamu
Paulo anasisitiza kwamba alitumwa kuhubiri Injili, si kwa ufasaha wa kisomi na ustadi wa maneno, ili nguvu za Mungu zisipuuzwe. Anatangaza kwamba kweli za Injili haziwezi kugunduliwa kwa hekima au elimu ya wanadamu. Ingawa mahubiri ya msalaba yanaonekana kuwa upumbavu kwa wale wasioamini, yanazidi hekima ya wanadamu, nayo ni nguvu za Mungu ziletazo wokovu kwa Myahudi na Myunani walioongoka. Mungu amewachagua watu wanaodharauliwa zaidi ili awaaibishe wanafalsafa wasomi na wakuu wa Wayahudi wanaoipinga hekima ya Injili. Kwa kulinganisha, anaonyesha jinsi mafanikio yote ya wanadamu yalivyo duni, ili mtu yeyote asijisifu isipokuwa katika Bwana.
18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. 19 Kwa maana imeandikwa:
“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,
na kubatilisha akili ya wenye akili.”
20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.
26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”
Paulo Alihubiri Bila Ufasaha wa Kibinadamu
Paulo anasema kwamba alipowahubiria injili, tofauti na walimu wao wa uongo, hakuipamba kwa elimu wala ufasaha wa kibinadamu. Hoja zake zilitokana na ushuhuda wa ufunuo wa kimungu, uliothibitishwa kwa nguvu za miujiza. Kwa hiyo imani yao haipaswi kutegemea hekima wala falsafa ya wanadamu.
1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. 2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo aliyesulubiwa. 3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.
Hekima ya Mungu Iliyofichika Yafunuliwa na Roho
Kisha Paulo anaonyesha kwamba, ingawa hatumii hekima ya ulimwengu, Wakorintho hawana sababu ya kujivunia walimu wao wa uongo. Kwa maana ananena siri ya Mungu iliyofichika ambayo Roho amemfunulia, siri ambayo hakuna jitihada wala elimu ya binadamu ingeweza kuifikia. Kwa mahubiri ya Roho Mtakatifu anawatangazia mambo ya kina ya Mungu, ambayo yanaweza kufunuliwa na Roho wa Mungu pekee. Mambo hayo hayawezi hata kupokelewa na mtu wa tabia ya asili, asiye wa kiroho, ambaye hana msaada mwingine isipokuwa uwezo wake wa kibinadamu.
6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulubisha Bwana wa utukufu. 9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:
“Hakuna jicho limepata kuona,
wala sikio limepata kusikia,
wala hayakuingia moyoni wowote,
yale Mungu amewaandalia
wale wampendao”:
10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.
Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni. 15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.
16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Bwana
ili apate kumfundisha?”
Lakini sisi tunayo mawazo ya Kristo.