Migawanyiko Kuhusu Wahudumu Huharibu Hali ya Kiroho
Paulo anaonyesha kwamba migawanyiko kanisani, inayotokana na maoni ya watu kuhusu vipawa mbalimbali vya wahudumu wao, huharibu hali ya kiroho.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo. 2 Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari. 3 Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida? 4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?
5 Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kupitia wao mliamini, kama vile Bwana alivyompa kila mtu huduma yake. 6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliikuza. 7 Hivyo mwenye kupanda na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ambaye huifanya ikue. 8 Apandaye mbegu ana lengo sawa na yule atiaye maji na kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake. 9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.
10 Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga.
Kristo Ndiye Msingi Pekee
Yesu Kristo ndiye msingi pekee wa Ukristo. Wale wanaojenga juu ya msingi huu wanaonywa wawe waangalifu, kwa kuwa lazima wapitie mtihani mkali. Mwalimu aliyeingiza mafundisho ya uongo atawaona waongofu wake wakiiacha imani wakati wa mateso, kama kuni, nyasi kavu na mabua motoni, naye mwenyewe ataponyoka kwa shida. Kwa upande mwingine, wale waliojenga mafundisho sahihi na mema juu ya msingi huu watawaona waongofu wao, kama fedha na dhahabu, wakipita katika jaribu la moto, naye mwalimu mwenyewe atapokea thawabu ya kazi zake.
11 Kwa maana hakuna mtu yeyote awezaye kuweka msingi mwingine wowote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo. 12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi, 13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake. 15 Kama kazi kitateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.
Hekima ya Ulimwengu Huu Ni Upumbavu
Paulo anatangaza kwamba mwalimu anayeingiza mafundisho ya uongo kanisani kwa makusudi ataangamizwa, hata awe amefanikiwa kiasi gani. Hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu machoni pa Mungu. Kwa hiyo hawapaswi kujivunia walimu wao au falsafa yao wanayoisifia sana, na hivyo kuleta migawanyiko kanisani. Utukufu wa kweli wa Mkristo uko katika Kristo, ambaye ni wa Mungu, na ambaye kupitia yeye pekee tunapokea ahadi za wokovu, ambazo wahubiri wa injili hawawezi kutoa.
16 Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu yeyote akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ndiyo hilo hekalu.
18 Msijidanganye. Kama mtu yeyote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima. 19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,” 20 tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.” 21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Vitu vyote ni vyenu, 22 ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefa au dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu 23 na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.
Mungu Pekee Ndiye Anayewahukumu Watumishi Wake
Mitume, wakiwa watumishi wa Kristo, wanatakiwa kufunua siri za injili kadiri watu wanavyokuwa tayari kuzipokea. Akijibu ukosoaji wa walimu wa uongo kwamba hakuwafundisha Wakorintho mafundisho ya kina zaidi ya Ukristo, Paulo anatangaza kwamba kuhukumiwa na wanadamu kuwa mwenye hatia si jambo la maana sana, kwa kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kuhukumu kwa haki, naye pekee ndiye anayejua siri za moyo. Kwa hiyo anawahimiza wasiwahukumu walimu wao wa kiroho.
1 Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu. 2 Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu. 3 Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu. 4 Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana ndiye anihukumuye. 5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.
Mitume Wanadharauliwa, Walimu wa Uongo Wanaheshimiwa
Paulo anasema kwamba ametumia jina lake mwenyewe na la Apolo ili wajifunze kutowathamini kupita kiasi viongozi wao mbalimbali, na hivyo kujaa kiburi, hasira na dharau wao kwa wao. Paulo na Apolo walikuwa watumishi wa Kristo tu, ambao kupitia huduma yao Wakristo walikuwa wameamini. Walikataa vyeo na heshima zote za kuwatofautisha kati yao, ili kwa mfano wao Wakorintho wajifunze kutowathamini walimu wao kupita yale aliyoyaandika. Kisha Paulo anawageukia walimu wa uongo. Mitume wanaitwa wajinga na wapumbavu kwa sababu wanahubiri fundisho la kwanza la imani ya Mkristo, ilhali walimu wa uongo, kwa sababu ya mawazo yao ya kubuni na mapokeo yao, wanaonwa kuwa watu wenye hekima na wanafalsafa. Mitume wanadharauliwa; walimu wa uongo wanaheshimiwa. Mitume wanakabiliwa na kila aina ya hatari, ilhali walimu wa uongo wanafurahia utajiri na kila aina ya starehe.
6 Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. 7 Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?
8 Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi! 9 Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia. 10 Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Kristo. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. 11 Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. 12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, 13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.
Paulo Anawaonya Kama Baba Yao
Paulo anasema kwamba haandiki mambo haya ili awaaibishe bali awafundishe, na kuwaonya dhidi ya walimu wa uongo, ambao hawatakuwa kwao kama alivyokuwa yeye, baba yao wa kiroho. Kwa hiyo anawasihi wamwige, na anamtuma Timotheo kwao ili awakumbushe mafundisho yake.
14 Siwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa. 15 Hata kama mnao walimu 10,000 katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Kristo Yesu kwa kuwaletea Injili. 16 Basi nawasihi igeni mfano wangu. 17 Kwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu njia za maisha yangu katika Kristo Yesu, ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha katika kila kanisa.
Paulo Atakuja Kuadhibu au kwa Upendo
Mwalimu wa uongo alikuwa amedai kwamba Paulo aliogopa kukabiliana na wapinzani wenye elimu na ufasaha kiasi hicho. Paulo anasema kwamba anakusudia kuwatembelea karibuni, ambapo hatachunguza maneno ya wapinzani wake bali nguvu zao zisizo za kawaida, kwa kuwa injili haithibitishwi na hekima inayojivuniwa ya wahubiri wake bali na nguvu za miujiza walizopewa ili kuithibitisha. Kisha anawauliza kama atumie nguvu zake mwenyewe zisizo za kawaida kuwaadhibu, au aje kwao kwa roho ya amani na upendo kwa sababu wamerekebisha makosa yao.
18 Baadhi yenu mmekuwa na jeuri mkidhani kuwa sitafika kwenu. 19 Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia kujua nguvu yao. 20 Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu. 21 Ninyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?