Mfukuzeni Mtu Anayefanya Uasherati na Jamaa Yake
Paulo anaamuru kwamba mtu aliyefanya uasherati na jamaa yake wa karibu atengwe na kanisa hadharani. Analaani kujivunia kwao ujuzi wa mwalimu wao wa uongo, ambaye amevumilia uovu huu wa kuchukiza, na anaonyesha jinsi dhambi inavyoenea kwa kuifananisha na chachu. Wanakatazwa kushirikiana na Wakristo wanaoishi waziwazi maisha yasiyomcha Mungu, ambao wanapaswa kukabidhiwa kwa kanisa ili waadhibiwe. Lakini wapagani waovu, kwa kuwa wako nje ya kanisa, wanapaswa kuachiwa hukumu ya Mungu.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Yamkini habari imeenea ya kuwa miongoni mwenu kuna uzinzi ambao haujatokea hata miongoni mwa watu wasiomjua Mungu: Kwamba mtu anaishi na mke wa baba yake. 2 Nanyi mwajivuna! Je, haiwapasi kuhuzunika na kumtenga na ushirika wenu mtu huyo aliyefanya mambo hayo? 3 Hata kama siko pamoja nanyi katika mwili, niko nanyi katika roho. Nami nimekwisha kumhukumu mtu huyo aliyetenda jambo hili, kama vile ningekuwepo. 4 Mnapokutana katika Jina la Bwana wetu Yesu nami nikiwepo pamoja nanyi katika roho na uweza wa Bwana Yesu ukiwepo, 5 mkabidhini mtu huyu kwa Shetani, ili mwili wake uharibiwe, ili roho yake iokolewe katika siku ya Bwana.
6 Majivuno yenu si mazuri. Je, hamjui ya kwamba chachu kidogo huchachusha donge zima la unga? 7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Kristo, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu. 8 Kwa hiyo, tusiiadhimishe sikukuu hii, kwa chachu ya zamani, chachu ya nia mbaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, ndio weupe wa moyo na kweli.
9 Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi. 10 Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyangʼanyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu. 11 Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.
12 Yanihusu nini kuwahukumu wale watu walio nje ya kanisa? Je, si mnapaswa kuwahukumu hao walio ndani? 13 Mungu atawahukumu hao walio nje. “Ninyi mwondoeni huyo mtu mwovu miongoni mwenu.”
Kesi Mbele ya Mahakama za Wapagani
Wakristo wanakemewa kwa kupeleka migogoro yao katika mahakama za wapagani, jambo linaloaibisha kukiri kwao kuwa Wakristo, badala ya kuipeleka mbele ya walimu wao waliovuviwa, ambao walitoa sheria za kuutawala ulimwengu wa sasa. Pia wanakemewa kwa kujaribu kuwatendea dhuluma na kuwalaghai ndugu zao Wakristo.
1 Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? 2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? 3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? 4 Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa. 5 Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio? 6 Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!
7 Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa? 8 Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.
Paulo Anakanusha Utetezi wa Ukosefu wa Maadili
Hapa Paulo anakanusha hoja za mwalimu wa uongo, ambaye inaonekana aliunga mkono maisha ya anasa na uasherati, na anatangaza kwamba hakuna mtu mchafu anayeweza kurithi baraka za injili. Kujifurahisha kupita kiasi kwa mambo ambayo yenyewe yanaruhusiwa ni dhambi kwa Wakristo, ambao ni mali ya Mungu kwa kuumbwa na kwa kukombolewa.
9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.
12 “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote. 13 “Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana na Bwana kwa ajili ya mwili. 14 Naye Mungu aliyemfufua Bwana kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake. 15 Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Kristo mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Kristo na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha! 16 Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 17 Lakini mtu aliyeungwa na Bwana anakuwa roho moja naye.
18 Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe. 19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
Kanuni kwa Walio Katika Ndoa na Wasio Katika Ndoa
Paulo anaendelea kujibu maswali ya Wakorintho. Anatoa kanuni za mwenendo kwa walio katika ndoa na wasio katika ndoa, kulingana na tofauti za tabia zao na hali ya kanisa wakati huo wa mateso.
1 Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke. 2 Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3 Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. 4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi. 6 Nasema haya kama ushauri na si amri. 7 Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.
8 Kwa wale wasiooa na kwa wajane, nasema hivi, ingekuwa vizuri wasioe. 9 Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
10 Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asitengane na mumewe. 11 Lakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.
12 Lakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache. 13 Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache. 14 Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu. 15 Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani. 16 Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume unajuaje kama utamwokoa mkeo?
17 Lakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana, yale Mungu aliyomwitia. Hii ni sheria ninayoiweka kwa makanisa yote.