Ukristo Haubadili Mahusiano ya Maisha

Paulo anafundisha kwamba Ukristo haubadili mahusiano ya kawaida na wajibu wa asili wa maisha.

57 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wakorintho 7:18–24

18 Je, mtu alikuwa tayari ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe. 19 Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu. 20 Basi kila mmoja wenu na abaki katika hali aliyoitwa nayo. 21 Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Ingawaje unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wowote. 22 Kwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Kristo. 23 Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu. 24 Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.

Mabikira na Wajane Wanashauriwa Kubaki Bila Ndoa

Paulo anawashauri mabikira na wajane wabaki bila ndoa wakati wa mateso. Ili kupunguza kuhangaikia kwao mahitaji na raha za maisha ya sasa, anawakumbusha jinsi maisha yalivyo mafupi na yasivyo na umuhimu mkubwa.

1 Wakorintho 7:25–40

25 Basi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana. 26 Kwa sababu ya shida iliyoko kwa sasa, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo. 27 Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke. 28 Lakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo.

29 Lakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake; 30 nao wanaoomboleza, kama ambao hawaombolezi; wenye furaha kama wasiokuwa nayo; wale wanaonunua, kama vile vitu walivyonunua si mali yao; 31 nao wale wanaoshughulika na vitu vya dunia hii, kama ambao hawahusiki navyo. Kwa maana dunia hii kama tunavyoiona sasa inapita.

32 Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, jinsi ya kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe, 34 na mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe. 35 Ninasema haya kwa faida yenu wenyewe, sio ili kuwawekea vizuizi bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana.

36 Kama mtu yeyote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane. 37 Lakini mwanaume ambaye ameamua moyoni mwake kutooa bila kulazimishwa na mtu yeyote, bali anaweza kuzitawala tamaa zake kutomwoa huyo mwanamwali, basi anafanya ipasavyo. 38 Hivyo basi, mwanaume amwoaye mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.

39 Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima awe katika Bwana. 40 Lakini kwa maoni yangu, angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.

Chakula Kilichotolewa kwa Sanamu na Walio Dhaifu

Akiwajibu waongofu, Paulo anafundisha kwamba ingawa kula vitu vilivyotolewa kwa sanamu hakukuwa jambo jema wala baya lenyewe, desturi hiyo ilipaswa kuepukwa, kwa kuwa mfano wao ungeweza kuwaingiza ndugu walio dhaifu zaidi katika dhambi kwa kuwatia moyo kufikiri kwamba sanamu yao ni mungu halisi.

1 Wakorintho 8

1 Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. 2 Mtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua. 3 Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu.

4 Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu: Tunajua kwamba “Sanamu si kitu chochote kabisa duniani,” na kwamba “Kuna Mungu mmoja tu.” 5 Kwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa miungu, kama wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi), 6 kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.

7 Lakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea sanamu kuwa halisi hivi kwamba wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, dhamiri yao inanajisika. 8 Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote kama tukila.

9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu. 10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. 13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.