Paulo Anatetea Haki Zake Kama Mtume

Hapa Paulo anatetea utume wake kwa kutaja kuongoka kwao wenyewe kutoka upagani na vipawa vya kiroho alivyowapa. Anajibu pingamizi ambazo adui zake, ambao maoni na mwenendo wao ulikuwa kinyume kabisa na wake, walitoa dhidi ya hadhi yake kama mtume. Anasisitiza kwamba, ingawa alikataa kupokea msaada wa kujikimu kutoka kwa Wakorintho, alikuwa na haki kamili ya kuudai, kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dada yake, au mke wake, kama mitume wengine walivyokuwa nayo. Anatetea haki yake ya kupata msaada wa kujikimu kwa kutumia desturi ya kawaida ya wanadamu, Sheria ya Mose, na amri ya wazi ya Kristo.

57 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wakorintho 9:1–14

1 Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana? 2 Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni mhuri wa utume wangu katika Bwana.

3 Huu ndio utetezi wangu kwa hao wanaokaa kunihukumu. 4 Je, hatuna haki ya kula na kunywa? 5 Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana na Kefa? 6 Au ni mimi na Barnaba tu inatubidi kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu?

7 Ni askari yupi aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake. 8 Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, sheria haisemi vivyo hivyo? 9 Kwa maana imeandikwa katika Sheria ya Mose: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ngʼombe? 10 Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno. 11 Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu? 12 Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi?

Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Kristo. 13 Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni? 14 Vivyo hivyo, Bwana ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.

Paulo Anaachilia Haki Yake ya Kupata Msaada wa Kujikimu

Paulo anatoa sababu zake za kutodai haki yake ya kutegemezwa na kanisa la Kikristo huko Korintho: alihofia kwamba kwa kuwatwika mzigo angeweza kuzuia mafanikio ya injili. Anaeleza tamaa yake kubwa ya kufanya vyema zaidi katika huduma yake. Akiwa ameridhika na wajibu wa kuhubiri ambao hawezi kuuacha bila kuutimiza, anaonyesha jinsi anavyojishusha ili kuzingatia udhaifu na ubaguzi wa watu wa kila aina, apate kuwavuta kwa Kristo. Kuanzia mstari wa 24, Paulo anaonyesha kwamba anafanya jambo linalofaa kwa kujitia katika taabu na kazi ngumu zisizo za lazima, akitaja desturi ya watu wa nchi yao wenyewe, ambao wanatumaini kushinda taji linaloharibika tu. Anawaalika wote walioongoka kufuata mfano wake, wakitiwa moyo na tumaini la hakika la kupata taji lisiloharibika. Wanahimizwa kuishi maisha ya kujinyima na kujizuia daima.

1 Wakorintho 9:15–27

15 Lakini sijatumia hata mojawapo ya haki hizi. Nami siandiki haya nikitumaini kwamba mtanifanyia mambo hayo. Heri nife kuliko mtu yeyote kuninyima huku kujisifu kwangu. 16 Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili! 17 Nikihubiri kwa hiari, ninayo thawabu. Lakini kama si kwa hiari, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa. 18 Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.

19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadri iwezekanavyo. 20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. 21 Kwa watu wasio na sheria nilikuwa kama asiye na sheria (ingawa siko huru mbali na sheria ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao. 23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.

24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele. 26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa, 27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

Mfano wa Israeli Unawaonya Wakorintho

Kwa kutumia mwenendo wa Waisraeli wa kale, Paulo anataka kuwasadikisha Wakorintho kwamba, kama vile watu waliopendelewa na Mungu walivyoadhibiwa vikali kwa matendo yao maovu na ibada ya sanamu, vivyo hivyo Wakristo walio chini ya Injili wanaojitosa katika dhambi na anasa hizo hizo wataadhibiwa bila shaka, kama Waisraeli waliokuwa chini ya Sheria. Kwa mifano hiyo anawaonya waepuke makosa hayo hayo. Anawaonya wasijitumainie kupita kiasi kwa sababu wao ni washiriki wa kanisa la Kikristo, bali wajihadhari ili wao pia wasianguke katika dhambi.

1 Wakorintho 10:1–12

1 Ndugu zangu, sitaki mkose kufahamu ukweli huu kwamba baba zetu walikuwa wote chini ya wingu na kwamba wote walipita katikati ya bahari. 2 Wote wakabatizwa kuwa wa Mose ndani ya lile wingu na ndani ya ile bahari. 3 Wote walikula chakula kile kile cha roho, 4 na wote wakanywa kile kile kinywaji cha roho, kwa maana walikunywa kutoka ule mwamba wa roho uliofuatana nao, nao ule mwamba ulikuwa Kristo. 5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, kwa hiyo miili yao ilitapakaa jangwani.

6 Basi mambo haya yalitokea kama mifano ili kutuzuia tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya. 7 Msiwe waabudu sanamu, kama baadhi yao walivyokuwa, kama ilivyoandikwa, “Watu waliketi chini kula na kunywa, kisha wakainuka kucheza na kufanya sherehe za kipagani.” 8 Wala tusifanye uzinzi kama baadhi yao walivyofanya, wakafa watu 23,000 kwa siku moja. 9 Wala tusimjaribu Kristo, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka. 10 Msinungʼunike kama baadhi yao walivyofanya, wakaangamizwa na mharabu.

11 Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia. 12 Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke.

Wakorintho Lazima Waepuke Ibada ya Sanamu

Wakorintho, wanaokabili majaribu yaleyale yanayowapata wengine, wanahimizwa kujiepusha na ibada ya sanamu na kula vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Paulo anathibitisha, kwa kutumia Ushirika wetu wenyewe na sheria ya taratibu za ibada, kwamba tendo hilo lilikuwa namna ya nje ya kuwaabudu pepo, kwa kuwa watu hao walikula karamu za sadaka zilizotolewa kwa pepo hao na kujiunganisha nao. Ibada ya Mungu wa kweli na ibada ya sanamu haziwezi kwenda pamoja, na kufanya hivyo kunamvunjia Kristo heshima.

1 Wakorintho 10:13–22

13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

14 Kwa hiyo wapenzi wangu, zikimbieni ibada za sanamu. 15 Nasema watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo. 16 Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja.

18 Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? 19 Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yoyote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yoyote? 20 La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. 21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani pia. 22 Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?