Vyakula Vinavyoruhusiwa na Manufaa ya Wengine
Paulo anathibitisha kwamba, ingawa chini ya Injili vyakula vyote viliruhusiwa, anapinga walimu wa uongo kwa kutangaza kwamba havifai, kwa kuwa kuwajenga wengine kunapaswa kutangulizwa. Wakorintho wanaweza kula chochote kilichouzwa sokoni mwa nyama au kilichowekwa mezani pa mpagani, isipokuwa ikiwa kwa kufanya hivyo wanakwaza dhamiri za ndugu walio dhaifu. Wakristo wanapaswa kutafuta utukufu wa Mungu na mema ya wengine badala ya matakwa yao wenyewe, hata katika matendo ambayo yenyewe si mema wala mabaya. Wanaitwa kuiga hali ya kutokuwa na ubinafsi ya Paulo, aliyemfuata Kristo.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga. 24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.
25 Kuleni chochote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lolote kwa ajili ya dhamiri. 26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”
27 Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri. 28 Lakini kama mtu yeyote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri. 29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?
31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. 32 Msiwe kikwazo kwa mtu yeyote, wawe Wayahudi au Wayunani, au kwa kanisa la Mungu, 33 kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa.
11:1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Kristo.
Paulo Anawakataza Wanawake Kuonekana Bila Vifuniko
Paulo anawasifu kwa kushika maagizo yake. Anaeleza asili ya maagizo hayo kwa kuonyesha kwamba wanaume wote wako chini ya Kristo, mwanamke chini ya mwanamume, na Kristo chini ya Mungu. Kwa kuwa shela ni alama ya kuwa na hadhi ya chini na ya kujitiisha, wanawake wanakatazwa kuonekana bila kuvaa shela.
2 Ninawasifu kwa kuwa mnanikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mafundisho niliyowapa.
3 Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu. 4 Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. 5 Naye kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele. 6 Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kukata au kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake. 7 Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu, lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. 8 Kwa maana mwanaume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume. 9 Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume. 10 Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka juu yake.
11 Lakini katika Bwana, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke. 12 Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu. 13 Hukumuni ninyi wenyewe: Je, inafaa kwa mwanamke kumwomba Mungu bila kufunika kichwa chake? 14 Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? 15 Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika. 16 Kama mtu anataka kubishana juu ya jambo hili, sisi wala makanisa ya Mungu hatutambui desturi nyingine.
Paulo Anakemea Machafuko Katika Meza ya Bwana
Paulo anawakemea kwa migawanyiko yao na makundi yao tofauti wanapokutana kushiriki Meza ya Bwana. Hawapaswi kukusanyika mahali pamoja tu, bali pia kushiriki Meza ya Bwana kama mwili mmoja, wakiungana kukumbuka kifo cha Kristo. Anawalaumu kwa kuleta chakula kanisani na kukiongeza kwenye Meza ya Bwana, jambo linalonajisi agizo hilo takatifu. Ili kurekebisha machafuko haya, Paulo anaeleza jinsi Ekaristi ilivyoanzishwa, pamoja na maagizo ya kuiadhimisha ipasavyo.
17 Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara. 18 Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. 19 Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. 20 Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, 21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. 22 Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha!
23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, 24 naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 25 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.” 26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo.
27 Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. 28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. 29 Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe. 30 Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. 31 Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa. 32 Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane. 34 Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani kwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa.
Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.