Sehemu ya 5: Safari ya Tatu ya Umishonari ya Paulo

Paulo Atembelea Tena Galatia na Frigia

Paulo anaondoka tena Antiokia ili kutembelea makanisa ya Galatia na Frigia.

55 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Matendo 18:23

23 Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.

Apolo Ahubiri huko Efeso

Habari ya Apolo, ambaye sasa alikuwa akilihubiria kanisa huko Efeso, ambalo Paulo alikuwa amelianzisha.

Matendo 18:24–28

24 Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Iskanderia. Yeye alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa hodari katika Maandiko. 25 Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana. 26 Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.

27 Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini. 28 Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.

Kutoka Frigia hadi Efeso

Paulo anaendelea kutoka Frigia hadi Efeso na kujadiliana na Wayahudi huko.

Matendo 19:1–10

1 Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa, 2 akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.” 3 Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”

4 Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.” 5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. 6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri. 7 Walikuwa kama wanaume kumi na wawili.

8 Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya Ufalme wa Mungu. 9 Lakini baadhi yao walikaidi. Walikataa kuamini, na wakakashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu. Basi Paulo aliachana nao. Akawachukua wanafunzi naye, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano. 10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.

Vitabu vya Uchawi Vyachomwa huko Efeso 56 BK

Paulo anakaa Efeso kwa miaka miwili. Watu wanachoma vitabu vyao vya uchawi.

Matendo 19:11–20

11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo, 12 hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.

13 Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” 14 Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. 15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” 16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.

17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana. 18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. 19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 za fedha. 20 Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.

Paulo Awatuma Timotheo na Erasto Makedonia na Akaya

Matendo 19:21–22

21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.” 22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.