Mose Arudia Sheria ya Sherehe (continued)
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. 2 Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa. 3 Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. 4 Hata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, 5 ikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. 6 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi.
7 Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 Afadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9 Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10 Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11 Siku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.
12 Kama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru. 13 Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu. 14 Mpe kwa uhuru kutoka zizi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka na kutoka mashinikizo yako ya kukamulia divai. Mpe kama vile ambavyo Bwana Mungu wako alivyokubariki. 15 Kumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Bwana Mungu wenu aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo.
16 Lakini mtumishi wako akikuambia, “Sitaki kukuacha,” kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako naye anaridhika nawe, 17 ndipo utachukua chuma kidogo utoboe sikio lake mpaka hicho chuma kiingie kwenye ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako wa maisha. Ufanye vivyo hivyo kwa mtumishi wa kike.
18 Usifikiri kuwa kuna ugumu kumwacha mtumishi wako huru, kwa sababu utumishi wake kwako kwa miaka hii sita umekuwa wa thamani mara mbili ya ujira wa mtumishi wa kuajiriwa. Naye Bwana Mungu wenu atakubarikia kwa kila kitu utakachofanya.
19 Wekeni wakfu kwa Bwana Mungu wenu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa makundi yenu ya ngʼombe na ya mbuzi na kondoo. Maksai walio wazaliwa wa kwanza msiwafanyize kazi, wala msinyoe manyoya ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo. 20 Kila mwaka ninyi na jamaa zenu mtapaswa kuwala mbele za Bwana Mungu wenu pale mahali atakapopachagua. 21 Kama mnyama ana dosari, akiwa ni kilema au kipofu au kama ana kilema kibaya, kamwe usimtoe dhabihu kwa Bwana Mungu wenu. 22 Itawapasa kumla ninyi wenyewe katika miji yenu. Wote wasio safi na walio safi kwa desturi za kiibada mwaweza kula kama vile mnavyokula paa au kulungu. 23 Lakini kamwe msinywe damu; imwageni ardhini kama maji.
16:1 Shikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Bwana Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku. 2 Mtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Bwana Mungu wenu kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo au la ngʼombe, mahali pale ambapo Bwana atapachagua kama makao kwa ajili ya Jina lake. 3 Msile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili kwamba siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri. 4 Chachu isionekane katika mali zenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe mpaka asubuhi.
5 Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Bwana Mungu wenu amewapa, 6 isipokuwa mahali atakapopachagua kama makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo ndipo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni, jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri. 7 Okeni na mle mahali pale ambapo Bwana Mungu wenu atakapopachagua, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu. 8 Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Bwana Mungu wenu na msifanye kazi.
9 Mhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka. 10 Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Bwana Mungu wenu kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Bwana Mungu wenu amewapa. 11 Shangilieni mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua kama makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane waishio miongoni mwenu. 12 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.
13 Adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao yenu ya nafaka na kukamua zabibu. 14 Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu. 15 Kwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Bwana Mungu wenu katika mahali atakapopachagua Bwana. Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.
16 Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Bwana mikono mitupu: 17 Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki.
18 Wateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Bwana Mungu wenu anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa. 19 Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki. 20 Mfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa.
21 Msisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Bwana Mungu wenu, 22 wala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Bwana Mungu wenu anavichukia vitu hivi.
17:1 Msimtolee Bwana Mungu wenu dhabihu ya maksai au kondoo ambaye ana dosari yoyote au hitilafu ndani yake, kwa kuwa hilo litakuwa chukizo kwake.