Mose Arudia Sheria ya Sherehe (continued)

1451 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Kumbukumbu 13–14

1 Kama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2 ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” 3 kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Bwana Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. 4 Ni Bwana Mungu wenu ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. 5 Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Bwana Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Bwana Mungu wenu aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

6 Kama ndugu yako hasa, au mwanao au binti yako, au mke umpendaye, au rafiki yako wa karibu sana akikushawishi kwa siri, akisema, “Na twende tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo ninyi wala baba zenu hamkuifahamu, 7 miungu ya watu wanaowazunguka, ikiwa karibu au mbali, kutoka mwisho mmoja wa nchi mpaka mwingine), 8 usikubali wala usimsikilize. Usimhurumie! Usimwache wala usimkinge. 9 Hakika ni lazima auawe. Ni lazima mkono wako uwe wa kwanza katika kumuua kisha mikono ya watu wengine wote. 10 Mpigeni kwa mawe mpaka afe, kwa sababu alijaribu kuwageuza mtoke kwa Bwana Mungu wenu ambaye aliwatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. 11 Kisha Israeli wote watasikia na kuogopa, wala hakuna mmoja miongoni mwenu atakayefanya uovu tena.

12 Kama mkisikia ikisemwa kwamba moja ya miji ambayo Bwana Mungu wenu anawapa mkae ndani yake 13 kuna wanaume waovu wameinuka miongoni mwenu na wamewapotosha watu wa mji, wakisema, “Twendeni tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo hamkuifahamu), 14 ndipo itakubidi kuuliza, kupima na kuchunguza kwa makini. Kama ni kweli, tena ikihakikishwa kwamba jambo hili lichukizalo limefanyika miongoni mwenu, 15 kwa hakika ni lazima mwaue kwa upanga wale wote wanaoishi katika mji ule. Uharibuni kabisa, pamoja na watu wake na mifugo yake. 16 Kusanyeni nyara zote za mji katika uwanja wa wazi na kuuchoma mji kabisa pamoja na nyara zake zote kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wenu. Utabaki kuwa magofu milele na hautajengwa tena. 17 Hakuna kimoja kati ya vitu vilivyolaaniwa kitakachokutwa mikononi mwenu, ili Bwana ageuze hasira yake kali. Atawahurumia na kuwa na rehema kwenu pia kuongeza idadi yenu, kama alivyowaahidi baba zenu, 18 kwa sababu mnamtii Bwana Mungu wenu, mkizishika amri zake zote zile ninazowapa leo na kufanya lile lililo jema machoni pake.

14:1 Ninyi ni watoto wa Bwana Mungu wenu. Msijichanje ama kujinyoa upara kwenye paji la uso kwa ajili ya aliyekufa, 2 kwa maana ninyi ni taifa takatifu kwa Bwana Mungu wenu. Bwana amewachagua ninyi kuwa taifa la kipekee kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia, mwe tunu yake.

3 Msile kitu chochote ambacho ni machukizo. 4 Hawa ndio wanyama mtakaokula: ngʼombe, kondoo, mbuzi, 5 kulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani. 6 Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua. 7 Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu kwa taratibu za kiibada. 8 Nguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.

9 Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula yeyote aliye na mapezi na magamba. 10 Lakini chochote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.

11 Mnaweza kula ndege yeyote aliye safi. 12 Lakini wafuatao msiwale: tai, furukombe, kipungu, 13 kengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yoyote, 14 kunguru wa aina yoyote, 15 mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga wa aina yoyote, 16 bundi, mumbi, bundi mkubwa, 17 mwari, nderi, mnandi, 18 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

19 Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale. 20 Lakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.

21 Msile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Bwana Mungu wenu.

Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

22 Hakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka. 23 Mtakula zaka za nafaka yenu, divai mpya, mafuta na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ngʼombe na ya kondoo na mbuzi mbele za Bwana Mungu wenu pale mahali atakapopachagua kama maskani kwa ajili ya Jina lake, ili kwamba mpate kujifunza kumheshimu Bwana Mungu wenu daima. 24 Lakini ikiwa mahali pale ni mbali sana nanyi mmebarikiwa na Bwana Mungu wenu na hamwezi kubeba zaka yenu (kwa sababu mahali pale Bwana atakapopachagua kuliweka Jina lake ni mbali sana), 25 basi badilisheni zaka yenu kuwa fedha, mkaichukue hiyo fedha mwende nayo mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua. 26 Tumieni hiyo fedha kununua chochote ukitakacho: ngʼombe, kondoo, divai au kinywaji chochote chenye chachu au chochote mnachotaka. Kisha ninyi na wa nyumbani mwenu mtaila mbele za Bwana Mungu wenu na kufurahi. 27 Msiache kuwajali Walawi waishio katika miji yenu, kwa kuwa hao hawana shamba wala urithi wao wenyewe.

28 Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29 ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Bwana Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.