Mose Arudia Sheria ya Mahakama
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
2 Ikiwa mwanaume au mwanamke anayeishi kati ya mojawapo ya miji akupayo Bwana, anakutwa anafanya uovu mbele za Bwana Mungu wenu, kwa kuvunja Agano lake, 3 naye amekwenda kinyume na agizo langu kuabudu miungu mingine na kuisujudia, kama vile jua, mwezi au nyota za angani, 4 hili likiwa limeletwa mbele yenu, ni lazima kulichunguza kikamilifu. Ikiwa ni kweli na kuwa limehakikishwa kwamba hili ni chukizo lililofanyika katika Israeli, 5 mchukueni huyo mwanaume au mwanamke ambaye amelifanya tendo hili ovu kwenye lango la mji wenu na kumpiga mawe mtu huyo mpaka afe. 6 Kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu mtu huyo atauawa, bali hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu. 7 Ni lazima kwanza mikono ya mashahidi itangulie kumuua huyo mtu, kisha mikono ya watu wote. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
8 Kama mashauri yanaletwa katika mahakama zenu ambayo ni magumu zaidi kwenu kuyaamua, ikiwa ni umwagaji wa damu, madai au mashambulio, yapelekeni mahali ambapo Bwana Mungu wenu atapachagua. 9 Nendeni kwa makuhani, ambao ni Walawi, na kwa mwamuzi ambaye atakuwa kazini wakati huo. Ulizeni kwao nao watawapa maamuzi. 10 Ni lazima mtende sawasawa na maamuzi watakayowapa mahali Bwana atakapopachagua. Kuweni waangalifu kufanya kila kitu watakachowaongoza kufanya. 11 Fanyeni sawasawa na sheria wanayowafundisha na maamuzi wanayowapa. Msigeuke mkono wa kuume au kushoto kuacha kufanya yale wanayowaambia. 12 Mwanaume atakayeonyesha dharau kwa mwamuzi au kwa kuhani ambaye amewekwa kumtumikia Bwana Mungu wenu lazima auawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli. 13 Watu wote watasikia na kuogopa, nao hawatakuwa wenye kudharau tena.
14 Wakati utakapoingia katika nchi anayowapa Bwana Mungu wenu kuimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, “Na tumweke mfalme juu yetu kama mataifa yanayotuzunguka,” 15 kuweni na uhakika wa kumweka mfalme juu yenu ambaye Bwana Mungu wenu atamchagua. Ni lazima atoke miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msimweke mgeni juu yenu ambaye si ndugu wa Kiisraeli. 16 Hata hivyo, kamwe mfalme asijipatie hesabu kubwa ya farasi kwa ajili yake mwenyewe, au kuwafanya watu warudi Misri ili kupata farasi zaidi, kwa maana Bwana amekuambia, “Hamtairudia njia ile tena.” 17 Kamwe asioe wake wengi, la sivyo moyo wake utapotoka. Kamwe asijilimbikizie kiasi kikubwa cha fedha na dhahabu.
18 Atakapokuwa amekalia kiti cha ufalme wake, ajiandikie kwenye kitabu nakala ya sheria kwa ajili yake mwenyewe kutoka zile sheria za makuhani ambao ni Walawi. 19 Atakuwa na nakala hiyo, naye ataisoma siku zote za maisha yake ili kwamba ajifunze kumheshimu Bwana Mungu wake na kufuata kwa uangalifu maneno yote ya sheria hii na amri hizi, 20 naye asijifikirie kuwa ni bora kuliko ndugu zake na kuipotosha sheria. Ndipo yeye na wazao wake watatawala katika ufalme wake kwa muda mrefu katika Israeli.
18:1 Makuhani ambao ni Walawi, yaani kabila lote la Lawi, hawatakuwa na mgawo wala urithi pamoja na Israeli. Wataishi kwa sadaka zitolewazo kwa ajili ya Bwana za kuteketezwa kwa moto, kwa maana huo ndio urithi wao. 2 Hawatakuwa na urithi miongoni mwa ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.
3 Hili ndilo fungu la makuhani kutoka kwa watu watakaotoa dhabihu ya fahali au kondoo: mguu wa mbele, mataya na matumbo. 4 Mtawapa malimbuko ya nafaka zenu, divai mpya, mafuta na sufu ya kwanza kutoka manyoya ya kondoo zenu, 5 kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewachagua pamoja na wazao wao kutoka makabila yenu kusimama na kuhudumu katika jina la Bwana siku zote.
6 Ikiwa Mlawi atahama kutoka mmojawapo ya miji yenu popote katika Israeli ambapo anaishi, akaja kwa moyo wote mahali ambapo Bwana atapachagua, 7 anaweza akahudumu katika jina la Bwana Mungu wake kama Walawi wenzake wote wanaohudumu hapo mbele za Bwana. 8 Atashiriki sawa katika mafao yao, hata kama amepokea fedha kutoka mauzo ya mali ya jamaa yake.
9 Wakati mtakapoingia katika nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msijifunze kuiga njia za machukizo za mataifa ya huko. 10 Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi, 11 wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu. 12 Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Bwana, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Bwana Mungu wenu atayafukuza mataifa hayo mbele yenu. 13 Kamwe msilaumiwe mbele za Bwana Mungu wenu.
14 Mataifa mtakayowafukuza husikiliza wale wafanyao ulozi na uaguzi. Lakini kwenu ninyi, Bwana Mungu wenu hajawaruhusu kufanya hivyo. 15 Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msikilizeni yeye. 16 Kwa kuwa hivi ndivyo mlivyomwomba Bwana Mungu wenu kule Horebu siku ile ya kusanyiko, wakati mliposema, “Na tusiisikie sauti ya Bwana Mungu wetu, wala kuuona moto huu mkubwa tena, ama sivyo tutakufa.”
17 Bwana akaniambia: “Wanachosema ni vyema. 18 Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zao; nitaweka maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia kila kitu nitakachomwamuru. 19 Kama mtu yeyote hatasikiliza maneno yangu ambayo huyo nabii atayasema kwa Jina langu, mimi mwenyewe nitamwajibisha. 20 Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu chochote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”
21 Mnaweza kuulizana wenyewe, “Tutawezaje kujua wakati ujumbe haukusemwa na Bwana?” 22 Ikiwa kile nabii anachotangaza kwa jina la Bwana hakikutokea au kutimia, huo ni ujumbe ambao Bwana hakusema. Nabii huyo amesema kwa ujuaji. Msimwogope huyo.