Yuda Anajadiliana kuhusu Bei ya Kumsaliti Yesu
Yuda, akiwa ameumizwa na kemeo la Yesu katika karamu, anajadiliana na viongozi kuhusu bei ya kumsaliti.
Jumanne usiku huko Yerusalemu
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 26:14–16
26:14 Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani
15 na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha.
16 Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu.
Marko 14:10–11
14:10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao.
11 Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.
Luka 22:3–6
22:3 Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili.
4 Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu.
5 Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha.
6 Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu kwao, wakati ambapo hakuna umati wa watu.
Kuandaa Chakula cha Pasaka Nyumbani kwa Rafiki
Maandalizi ya mlo wa Pasaka nyumbani kwa rafiki (huenda ilikuwa nyumba ya baba na mama yake Yohana Marko).
Yerusalemu, Alhamisi alasiri. (Siku ya Maandalizi)
Mathayo 26:17–19
26:17 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
18 Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ”
19 Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.
Marko 14:12–16
14:12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
13 Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni.
14 Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’
15 Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.”
16 Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
Luka 22:7–13
22:7 Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa.
8 Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”
9 Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?”
10 Yesu akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia.
11 Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’
12 Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.”
13 Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
Yesu Anakula Pasaka pamoja na Wale Kumi na Wawili
Yesu anakula chakula cha Pasaka pamoja na mitume kumi na wawili na kukemea wivu wao.
Yerusalemu, Alhamisi jioni baada ya jua kutua (mwanzo wa Ijumaa kwa hesabu ya Wayahudi)
Mathayo 26:20
26:20 Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.
Marko 14:17
14:17 Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.
Luka 22:14–16, 24–30
22:14 Wakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wale mitume wake.
15 Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16 Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”
24 Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao. 25 Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ 26 Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. 27 Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye. 28 Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. 29 Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi, 30 ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”