Yesu Anawaosha Wanafunzi Wake Miguu

Wakati wa mlo wa Pasaka, Yesu anawaosha wanafunzi wake miguu.

Jioni kabla ya kusulubiwa (Alhamisi kwetu, Ijumaa kwa kalenda ya Kiyahudi)

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yohana 13:1–20

13:1 Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho.

2 Wakati alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. 3 Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.

6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”

7 Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”

8 Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”

Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”

9 Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”

10 Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” 11 Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.

12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

18 “Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni ili Andiko lipate kutimia, kwamba, ‘Yeye aliyekula chakula changu, ameinua kisigino chake dhidi yangu.’

19 “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. 20 Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”

Yesu Anamtaja Yuda Kuwa Msaliti

Katika mlo wa Pasaka, Yesu anamtaja Yuda kuwa msaliti.

Alhamisi jioni (Ijumaa kwa Wayahudi)

Mathayo 26:21–25

26:21 Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22 Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”

23 Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti.

24 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”

25 Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?”

Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”

Marko 14:18–21

14:18 Walipoketi mezani wakila, Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.”

19 Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”

20 Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami.

21 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.”

Luka 22:21–23

22:21 Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami. 22 Mwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye.”

23 Wakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.

Yohana 13:21–30

13:21 Baada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22 Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani.

23 Mmoja wa wanafunzi wake ambaye Yesu alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu. 24 Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.”

25 Yule mwanafunzi akamwegemea Yesu, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?”

26 Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni.

27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.

Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.” 28 Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo. 29 Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini chochote. 30 Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.