Yesu Anawaonya Wanafunzi Wasimwache

Baada ya Yuda kuondoka, Yesu anawaonya wanafunzi (hasa Petro) wasimwache, huku wote wakisisitiza uaminifu wao kwake.

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 26:31–35

26:31 Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:

“ ‘Nitampiga mchungaji,

nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’

32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

33 Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

34 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

35 Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Marko 14:27–31

14:27 Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:

“ ‘Nitampiga mchungaji,

nao kondoo watatawanyika.’

28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

29 Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.”

30 Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.”

31 Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Luka 22:31–38

22:31 Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. 32 Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”

33 Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”

34 Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.”

35 Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?”

Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.”

36 Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. 37 Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.”

38 Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.”

Akawajibu, “Inatosha.”

Yohana 13:31–38

13:31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32 Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara.

33 “Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta, na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi. Niendako, ninyi hamwezi kuja.

34 “Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35 Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”

36 Simoni Petro akamuuliza, “Bwana, unakwenda wapi?”

Yesu akamjibu, “Ninakokwenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”

37 Petro akamuuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”

38 Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

Yesu Anaanzisha Ukumbusho wa Mkate na Divai

Yesu anaanzisha ukumbusho wa kula mkate na kunywa divai.

Yerusalemu. Jioni kabla ya kusulubiwa

Mathayo 26:26–29

26:26 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”

27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki.

28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

Marko 14:22–25

14:22 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.”

23 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo.

24 Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25 Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika Ufalme wa Mungu.”

Luka 22:17–20

22:17 Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18 Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”

19 Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

20 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu.