Yesu Anatabiri Kusulubiwa Kwake Baada ya Siku Mbili

Yesu anatabiri kusulubiwa kwake baada ya siku mbili kuanzia sasa (Ijumaa kwa hesabu ya Wayahudi).

Huenda ni Bethania Jumanne jioni (mwanzo wa Jumatano kwa hesabu ya Wayahudi). Viongozi huko Yerusalemu wanapanga njama ya kumuua

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 26:1–5

26:1 Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, 2 “Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”

3 Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa.

4 Wakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumuua.

5 Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”

Marko 14:1–2

14:1 Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Yesu kwa hila na kumuua.

2 Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.”

Luka 22:1–2

22:1 Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia.

2 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu.

Maria wa Bethania Anampaka Yesu Mafuta kwa Ajili ya Maziko

Katika karamu nyumbani kwa Simoni mwenye ukoma, Maria wa Bethania anampaka Yesu mafuta kwa ajili ya maziko yake.

Bethania (Jumanne jioni, Jumatano kwa hesabu ya Wayahudi)

Mathayo 26:6–13

26:6 Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma, 7 naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa; akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

8 Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini?

9 Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”

10 Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana.

11 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.

12 Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu.

13 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”

Marko 14:3–9

14:3 Yesu alikuwa Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu.

4 Baadhi ya watu waliokuwepo pale walikuwa wakisemezana wao kwa wao, “Upotevu huu wote ni wa nini?

5 Mafuta haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari 300, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.

6 Lakini Yesu akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana.

7 Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.

8 Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu.

9 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”

Yohana 12:2–8

12:2 Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu. 3 Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.

4 Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye angemsaliti Yesu, akasema,

5 “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300 na fedha hizo wakapewa maskini?”

6 Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi, kwani ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo.

7 Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu.

8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”