Sehemu ya 12: Katika Kivuli pamoja na Yesu

Kuanzia Jumanne alasiri hadi Alhamisi usiku katika Juma la Mateso, mwaka 30 (au 29) BK. Yerusalemu

Sasa Yesu anatafuta kuwaandaa wanafunzi kwa msiba wa kifo chake na kwa kuendeleza kazi yake baada ya kuondoka kwake.

Hotuba Kuu Kuhusu Nyakati za Mwisho

Akiwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, Yesu anazungumza na wanafunzi wake, kwa lugha ya mafunuo, kuhusu kuangamizwa kwa Yerusalemu na kuja kwake kwa mara ya pili. Hotuba kuu kuhusu mambo ya mwisho.

(Jumanne alasiri)

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 24:1–25:46

24:1 Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2 Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”

3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”

4 Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye.

5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi.

6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado.

7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.

8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu.

10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa,

13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.

15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu),

16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.

17 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba.

18 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.

19 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!

20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. 21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe. 22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa.

23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki.

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa.

25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.

26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

“ ‘jua litatiwa giza,

nao mwezi hautatoa nuru yake;

nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

na nguvu za anga zitatikisika.’

30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.

31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

32 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

33 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.

34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.

35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

36 “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. 39 Nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. 40 Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.

42 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. 44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.

45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

25:1 “Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi. 2 Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. 3 Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba, 4 lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo. 5 Bwana arusi alipokawia kuja wale wanawali wote wakasinzia na kulala.

6 “Usiku wa manane pakawa na kelele: ‘Tazameni, huyu hapa bwana arusi! Tokeni nje mkamlaki!’

7 “Ndipo wale wanawali wote wakaamka na kuzitengeneza taa zao. 8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupatieni mafuta yenu kidogo; taa zetu zinazimika.’

9 “Lakini wale wenye busara wakawajibu, ‘Sivyo, hayatutoshi sisi na ninyi pia. Afadhali mwende kwa wauzao mkajinunulie mafuta yenu.’

10 “Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa.

11 “Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’

12 “Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’

13 “Kwa hiyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.

14 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao. 15 Mmoja akampa talanta tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri. 16 Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi. 17 Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi. 18 Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake.

19 “Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao. 20 Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’

21 “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

22 “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’

23 “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

24 “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu. 25 Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’

26 “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu. 27 Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.

28 “ ‘Basi mnyangʼanyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi. 29 Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. 30 Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.

34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

Marko 13:1–37

13:1 Yesu alipokuwa akitoka Hekaluni, mmojawapo wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa, na majengo haya yalivyo mazuri!”

2 Ndipo Yesu akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali yote yatabomolewa.”

3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani,

4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”

5 Yesu akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye.

6 Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi.

7 Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.

8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao. 10 Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia. 11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.

12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.

14 “Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.

15 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote.

16 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.

17 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!

18 Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi. 19 Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka leo, na wala haitakuwako tena kamwe. 20 Kama Bwana asingelifupisha siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu yeyote. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo.

21 Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki.

22 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule.

23 Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.

24 “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki,

“ ‘jua litatiwa giza

nao mwezi hautatoa nuru yake;

25 nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

na nguvu za anga zitatikisika.’

26 “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.

27 Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.

28 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

29 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.

30 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.

31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

32 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.

33 Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia. 34 Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe.

35 “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko. 36 Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala. 37 Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”

Luka 21:5–36

21:5 Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonyesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Yesu akawaambia, 6 “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”

7 Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?”

8 Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate.

9 Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”

10 Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine. 11 Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.

12 “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu.

13 Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. 14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.

16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua. 17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.

20 “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia.

21 Wakati huo, wale walio Uyahudi wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo, nao wale walioko mashambani wasiingie mjini.

22 Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa.

23 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu.

24 Wataanguka kwa makali ya upanga, na wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote. Nao mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa Mataifa hadi muda wa hao watu wa Mataifa utimie.

25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika.

27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu.

28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”

29 Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote. 30 Inapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua wenyewe ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia.

31 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.

32 “Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.

33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”

34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo. 35 Kwa maana kama vile mtego unasavyo, ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote waishio katika uso wa dunia yote.

36 Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”